TUNDU LISSU ANAISHI KWA MASHAKA,SOMA HAPO KUJUA
MWANASHERIA wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu leo ametumia zaidi ya saa nne akiwa katika mahakama ya wilaya Dodoma akigoma kutoka humo akihofia kukamatwa, anaandika Dany Tibason.
Lissu akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma amesema jana majira ya asubuhi mke wake alimpigia simu na kumueleza kuwa askari kanzu wapatao sita walifika nyumbani kwake Dar es salaam wakimtafuta.
Hata hivyo, Lissu amesema akiwa mjini Dodoma akiendelea na kesi ya walimu ambao ni wateja wake alipokea taarifa kuwa wapo askari nje ya mahakama wanamsubiri wamkamate.
Kutokana na taarifa hiyo Lissu aligoma kutoka mahakamani hapo hatua ambayo ilisababisha kamanda wa polisi mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa kwenda kumuona na kumhakikisha kwamba hakuna mtu anayemtafuta.
Kauli hiyo ya Mambosasa ilimpa uhakika Lissu na hivyo kuamua kutoka nje ya Mahakama na kuendelea na shughuli zake.