Zinazobamba

NGELEJA AJITETA KUHUSU HELA ZA RUGEMALIRA,SOMA HAPO KUJUA

Siku chache baada ya kutangaza kuwasilisha shilingi milioni 40 katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja amefafanua sababu za kutomrejeshea fedha huyo mfanyabiashara, James Rugemalira ambaye alimpa awali kama msaada.

Fedha hizo ni sehemu ya shilingi bilioni 306 zilizotolewa katika akaunti maalum ya Tegeta Escrow mwaka 2014 iliyofunguliwa Benki Kuu ya Tanzania, fedha zizotolewa kimakosa wakati kesi ya mgogoro wa kati ya Tanesco na Kampuni ya kufua umeme ya IPTL ikiwa bado haijatolewa maamuzi.

Kwa mujibu wa taratibu, fedha hizo zilipaswa kutolewa baada ya kesi husika kukamilika na pande zote mbili kukaa pamoja kukokotoa kiasi cha fedha ambacho kila upande ungepaswa kupata kwa mujibu wa maamuzi.

“Kwa mazingira halisi yanayomkabili aliyenipa msaada, mahali salama pa kurejesha hizo fedha sasa ni serikalini. Serikali itajua kuwa fedha hizo zinastahili kwenda kwa Rugemalira sasa au wasubiri hatima ya kesi,” Ngeleja anakaririwa na Gazeti la Mwananchi .

“Ningerudisha kwa Rugemarila watu wangeweza kuibua hoja kwamba labda napiga changa la macho tu,” aliongeza.

Mfanyabiashara huyo maarufu ambaye kampuni yake ya VIP Engineering ilikuwa inamiliki asilimia 30 ya IPTL, pamoja na Mwenyekiti wa Pan African Power Solution (PAP), Harbinder Singh Seth wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi na bado wako mahabusu.

Mgao wa fedha hizo pia uliwafikia Anna Tibaijuka aliyekuwa waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Andrew Chenge ambaye ni Mbunge wa Bariadi Magharibi, Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki, Methodiu Kilaini, Jaji John Ruhangisa na wengine.