Zinazobamba

KESI YA MWANAHARAKATI LUSAKO BADO NGUMU,SOMA HAPO KUJUA

KESI ya Alphonce Lusako, mwanafunzi wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anayehangaikia haki yake ya kikatiba ya kujiendeleza kielimu baada ya kunyimwa na chuo hicho, imekwama, anaandika Hellen Sisya.
Lusako amefungua kesi Mahakama Kuu kuomba kusikilizwa malalamiko yake ya kunyimwa fursa ya kusoma Shahada ya Sheria katika chuo hicho kwa sababu ambazo kwake hazina msingi hata kisheria.
Kesi hiyo ingali kwenye hatua ya kutafuta kibali cha mahakama hiyo kumruhusu kufungua malalamiko yake hayo. Leo ilikuwa ni siku ya kutolewa uamuzi mdogo wa maombi yake Na. 39 ya mwaka huu.
Hata hivyo, imelazimu uamuzi huo kuahirishwa mpaka Julai 30 kutokana na Jaji Pelagia Khaday kueleza kuwa anahitaji muda zaidi wa kupitia kesi hiyo.
Hatua hiyo imekuja wakati uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam umeweka pingamizi kama njia ya kumzuia Lusako kufungua malalamiko yake rasmi ya kuonewa kuhusu dhamira yake ya kusoma katika chuo cha serikali na kwa mkopo unaotolewa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu nchini (HESLB).
Msingi wa malalamiko ya Lusako hasa ni kuwa chuo hicho kimemfukuza kinyume cha kanuni na sheria za nchi.
“Ninakishtaki chuo kwa sababu sikutendewa haki. Kikatiba nina haki ya msingi ya kusoma. Lakini pia nina vigezo vya kusoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na nilikidhi vigezo vya kudahiliwa katika chuo hiki kwa ajili ya shahada ya sheria, baada ya kuidhinishwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU),” anasema.