Zinazobamba

Mbunge aliyetemwa CUF azuiwa kuingia kwenye kikao cha madiwani

Mbunge wa Viti Maalumu (CUF) aliyevuliwa ubunge hivi karibuni Salma Mwasa amesikitishwa na kitendo cha askari wa Manispaa ya Ubungo cha kutaka kumzuia asikanyage kwenye halmashauri hiyo.

Mwasa ni miongoni mwa wabunge kumi waliovuliwa uanachama sanjari na madiwani wawili wa CUF kwa madai ya kukihujumu chama hicho, hali iliyosababisha kukosa fursa za kuwa wabunge.

Akisimulia tukio hilo lililotokea leo Jumatatu, Julai 31, Mwasa amesema aliitwa na askari hao na kuambiwa hatakiwi kuonekana katika eneo hilo la manispaa na kwamba, hiyo ni amri kutoka juu kwa wakubwa.

“Mimi ninachojua amri zipo kumi tu, sasa hiyo 11 inatoka wapi? Lakini niliwaeleza kwamba mimi ni mkazi wa Ubungo sasa mnaponizuia nisije hapa hamnitendei haki kwa sababu nakuja kufanya mahitaji mbalimbali,” amesema. 

“Mimi nimekuja kama mwananchi wa kawaida. Naomba umma utambue mimi bado ni mbunge hapa nilipo nina barua ya uteuzi na sina barua ya utenguzi,” anasema Mwasa.

Hata hivyo, haikuwa rahisi askari hao wa manispaa kumtambua Mwasa badala yake walikuwa na karatasi yenye majina mawili yaliyoandikiwa Salma Mwasa na diwani wa viti maalumu Leila Hussein, ambao hakutakiwa kuonekana eneo hilo wakati kikao cha Baraza Madiwani kikiendelea.

Askari hao walitumia njia za kuwauliza watu mbalimbali wakiwamo waandishi kama wanawafahamu kina Mwasa na Leila na walipowauliza wanashida nao gani walijibu hawatakiwi kuingia ndani ya ukumbi wa mikutano.

Mwananchi: