JINSI TANZANIA ILIVYOAZIMISHA SIKU YA QUDS...PROF LIPUMBA ATOA NENO
![]() |
MAANDAMANO YAKIENDELEA...WAKAZI WA JIJI LA DARESALAAM WAKISHIRIKI KATIKA MATEMBEZI HAYO YA AMANI YALIANZIA ILALA BOMA NA KUISHIA VIWANJA VYA KIGOGO |
Waislamu nchini Tanzania na wapenda amani
katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki leo wameungana na wapigania haki
duniani kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Quds ambayo ni Ijumaa ya mwisho
ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani ikiwa ni katika kuonyesha mshikamano wao
na muqawama wa wananchi wa Palestina mbele ya maghasibu Wazayuni.
Akizungumza
na waandishi wa habari katika maandamano hayo jijini Dar es Salaam,
Sheikh Hemedi Jalala Mkuu wa Chuo cha Kidini cha Imam Swadiq (as) cha
Dar es Salaam Tanzania ameyataja maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds
kwamba, yana umuhimu katika kufikisha ujumbe wa amani na kupinga dhulma
za utawala vamizi wa Israel dhidi ya wananchi wa Palestina.
Sheikh Jalala mmoja wa wanaharakati wa Kiislamu nchini Tanzania
amesema kuwa, Imam Khomeini (MA) muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya
Iran aliitangaza Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani iwe ni
siku ya kukumbuka vitu viwili. Kitu cha kwanza ni kuukumbuka msikiti
mtakatifu wa al-Aqswa kibla cha kwanza cha Waislamu. Sheikh Hemedi
Jalala ameongeza kuwa, jambo la pili ni kwamba, Imam Khomeini alitaka
siku hii iwe ni maalumu kwa ajili ya kuwakumbuka wanyonge wote na watu
wote wanaodhulumiwa duniani wakiwemo wananchi wa Palestina.
Sheikh Jalala ameashiria dhulma na ukandamizaji unaofanywa katika
maeneo mbalimbali duniani na akasisitiza kuwa, dhulma dhidi ya
Wapalestina ni kubwa kuliko dhulma yoyote inayoshuhudiwa katika maeneo
mengine ulimwenguni.
Sheikh
Jalala ambaye pia ni Imam Mkuu wa Msikiti wa al-Ghadir wa Kigogo Post
jijini Dar es Salaam amewataka Waislamu wa Tanzania na Waislamu wa dunia
kwa ujumla wasiusahau msikiti wao na wasisahahu kibla chao cha kwanza
yaani Masjidul Aqswa ambacho leo kiko hatarini kutokana na siasa za
kivamizi za utawala wa Kizayuni wa Israel.
Ameutaka
Umoja wa Mataifa kushughulikia kadhia ya Palestina ili Wapalestina nao
waishi kwa amani kama wanavyoishi watu wa maeneo mengine duniani.