Zinazobamba

SHIA ITHNASHERIYA YAWAKUTANISHA WANATAALUMA, VIJANA



Sehemu ya vijana waliohudhuria katika semina wakisikiliza kwa makini mada zinazowasilishwa katika mkutano huo.

Mwanafalsafa kutoka chuo kikuu cha Dar es salaam Dr Josephat Muhoza akifafanua jambo mbele ya waandishi wa habari kuhusu umuhimu wa vijana kusoma dini zao ili waweze kuwa na ufahamu wa mafundisho sahihi ya Muumba wao.

Kiongozi Mkuu wa kiroho wa Waislam wa dhehebu la Shia ITHNASHERIYA Tanzania Sheikh Hemed Jalala akizungumza na Waandishi wa habari
Waislamu wa dhehebu la Shia ITHNASHERIYA Tanzania wameweza kuwakutanisha vijana pamoja na wanataaluma, dhamira ikiwa ni kujadili kwa pamoja namna ya kumuunganisha Mwanadamu na dini yake pamoja na kumfanya kijana kufahamu tunu zilizopo katika dini zao.

Akizungumza katika ukumbi wa Nkuruma, uliopo chuo kikuu cha Daresalaam, Kiongozi Mkuu wa kiroho wa Waislam wa dhehebu la Shia ITHNASHERIYA Tanzania Sheikh Hemed Jalala amesema semina hiyo inadhamira moja tu ya kuwafanya vijana kutambua dini yao vizuri ikiwamo tunu zilizomo ili kuweza kuendeleza amani iliyopo Nchini.
 

"Vijana  wanatakiwa kutumia dini zao kama viungo vya kudumisha Amani,utulivu,na upendo  uliopo badala ya kutumia dini zao kutengeneza migogoro na mifarakano katika jamii jambo ambalo lina madhara makubwa katika ustawi wa taifa kwa Ujumla" Alisema

Sheikh Jalala amesema kuwa  Dunia kwa sasa inakabiliwa na vita ya wenyewe kwa wenyewe ambayo katika nchi nyingi dini imekuwa kichocheo kikubwa cha migogoro na migongano hiyo jambo ambalo amesema semina hiyo imeamua kuwakutanisha Vijana Pamoja na wataalam mbalimbali kuwakumbusha namna bora ya kuitumia dini yao kulinda Amani na kuepuka migogoro kama hiyo.

“Tanzania inasifa ya Amani, upendo, utulivu, kuheshimiana, kutokubaguana, hivyo vijana tunahitajika kuhakikisha kuwa tunaenzi Tunu hizi kwa hali na mali ili tuendelee kuwa na sifa ya kisiwa cha Amani duniani”alisema Kiongozi huyo wa Dhehebu la Shia nchini.

Kwa upande wake mwanafalsafa wa chuo kikuu cha Dar es salaam Dr Josephat Muhoza amewataka vijana kusoma dini zao vizuri ili waweze kutambua maelekezo sahihi ya Muumba wao, akisisitiza kuwa bila kusoma haitakuwa rahisi kufahamu kusudio la kuubwa kwa mwanadamu na hivyo kupelekea watu kuishi wanavyotaka, hali inayopelekea binadamu kuwa katika hasara.