IDARA YA USALAMA WA TAIFA YAITIKISA BUNGE,YATAJWA KUHUSIKA KATIKA MASUALA UTEKAJI,BASHE NA ZITTO WACHACHAMAA,SOMA HAPO KUJUA
WAKATI matukio ya utekaji yakiwa yameshika kwa kasi nchini kwa sasa,Wabunge wa Jamhuri wa Muungano leo bila kujali itikadi zao za Vyama wameishukia Idara hiyo kwa kutaja kuhusika na kwake na vitendo vya Utekaji kwa watu mbali mbali nchini.
Wabunge hao wakiongozwa na Mbunge wa Kigoma Mjini,Zitto Kabwe na Mbunge wa Nzega hussen Bashe wakati wa kuchangia hutuba ya Waziri mkuu wameitaja idara hiyo kwenye masuala utekaji huku wakiitaka serikali kutoa tamko.
HUTUBA YA ZITTO KABWE AKIHITUHUMU IDARA HIYO
Kuna kijana wa kitanzania, ndugu Ben Saanane amepotea kwa zaidi ya miezi mitano sasa. Hajulikani alipo. Wazazi wake na rafiki zake wamemtafuta na kutoa malalamiko bila mafanikio. Wamefikisha taarifa kwa jeshi la polisi na wamepaza sauti bila kuchoka. Kuna nyakati suala hili lilionekana la siasa na ndio maana wengine tulikaa pembeni. Lakini sasa ni miezi 6, kuna taarifa juu ya suala hili, nimeona nisikae kimya juu ya hili.
Taarifa zinatoka chini chini, sio rasmi, kwamba huyu kijana 'ametoweshwa'. Kwamba alishikiliwa na watu wa Idara ya Usalama na amepotezwa. Jeshi la Polisi wana taarifa za mawasiliano ya mwisho ya Ben Saanane kwa kutumia simu yake ya mkononi, ambayo inaonekana simu ilipoteza mawasiliano akiwa maeneo ya Buguruni siku aliyotekwa tarehe 15/16 Novemba 2016 na tangu siku hiyo hapakuwa na mawasiliano tena.
Siku hiyo simu yake ilisoma maeneo ya Tabata asubuhi, kisha Mikocheni na Mwenge muda mwingi wa mchana. Saa mbili usiku alikuwa Mburahati na saa nne usiku ilizimwa akiwa Buguruni. Polisi wanajua kuwa wenzao wa Usalama wa Taifa ndio waliomteka kijana huyu lakini hawawezi kuchukua hatua dhidi yao. Hivyo wameamua kukaa kimya wakiamini kuwa Watanzania tutasahau.
Jambo hili linasikitisha na kuumiza sana, Ben ni kijana wa kitanzania, ni mtoto, mjomba, baba, kaka, anayo familia, siwezi hata kufikiria ni namna gani familia yake inaumia kwa miezi hii sita bila kumuona ndugu yao, bila kujua alipo, bila kujua hatma yake. Inaumiza sana, inaumiza mno, ni jambo gumu sana kulivumilia, si jambo rahisi kulipuuzia na kusahau tu. Watanzania hatupaswi kukalia kimya kuhusu jambo hili, tukisahau hili hakuna atakayepona.
Kumekuwa na matukio ya namna hii mabaya kabisa huko nyuma; ndugu Absalom Kibanda, aliyekuwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri alivamiwa na kuumizwa vibaya sana na leo jicho lake moja halioni mwaka 2013. Pia ndugu Yona wa Temeke alitekwa na kuumizwa na kutupwa huko mbweni jijini Dar es salaam na hakuna mtu yeyote aliyekamatwa juu ya matukio yote hayo. Orodha ya matukio ya namna hii ni ndefu.
Watanzania wamesahaulishwa yote haya, Polisi mpaka Leo hawajamkamata hata mtu mmoja juu ya yote hayo. Sababu kubwa ni ukimya wetu. Sisi wabunge tumepewa ridhaa na wananchi wenzetu kuyasema haya, tumepewa mamlaka ya kuihoji serikali juu ya mambo ya wananchi, na Usalama wao na mali zao ni jambo la kwanza la msingi kabisa, wananchi wetu wakiwa na mashaka juu ya usalama wao, shughuli za uzalishaji mali zitakuwa duni, uchumi wa Taifa utadorora zaidi. Tunao wajibu wa kuhakikisha Usalama wa wananchi wetu, ni wakati wa kuibana Serikali juu ya hili.
Mheshimiwa Spika,
Naomba kulikumbusha Bunge lako Tukufu na wananchi Kwa ujumla kwamba Usalama wa Taifa hawana mamlaka yeyote kisheria kukamata mtu yeyote yule Kwa mujibu wa kifungu cha 5(2) cha sheria ya usalama wa Taifa ya mwaka 1996 Kama ilivyofanyiwa marekebisho mara kadhaa. Kwa hiyo Askari wa Usalama wa Taifa waliokwenda Clouds Media na silaha, Askari wa Usalama aliyemtolea silaha Mbunge wa Mtama, ndugu Nape, na kikosi cha utekaji na utesaji cha Usalama wa Taifa kinachohusishwa na utekaji wa watu wanavunja sheria ya usalama wa Taifa.
Hata askari wa Usalama wa Taifa waliomkamata Mbunge wa Geita Vijijini, ndugu Msukuma, Mbunge wa Nzega, ndugu Bashe na Mbunge mstaafu, ndugu Malima walivunja sheria ya Usalama wa Taifa. Kuna viashiria vyote kuwa hali si nzuri kabisa.
Lakini kuna jambo moja muhimu sana juu ya jambo hili, MTAZAMO HASI wa Watanzania juu ya Idara ya Usalama wa Taifa. Idara Nyeti, Muhimu na ya Kuheshimiwa mno kwa Taifa letu, inaniuma leo kusimama hapa Bungeni kuisema Idara ya Usalama wa Taifa. Mimi niko Bungeni mwaka wa 12 huu, hatuzungumzii mambo ya Usalama wa Taifa humu bungeni, jambo hilo ni 'Taboo', lakini kwa hali ilivyo sasa imenibidi niseme.
Mambo haya maovu yanayohusishwa na Idara hii yanaondoa uhalali wa Taasisi hii kwa wananchi, yanaondoa heshima, hadhi na uaminifu juu ya idara hii, yanajenga chuki na taswira hasi ya Wananchi kwa idara hii, hili si jambo jema kwa Taifa. Ni wakati sasa wa kuchukua hatua. Ni lazima Bunge liamke na kukomesha hali hii.
Kwa mujibu wa Kanuni ya 120(2) ya Kanuni za Bunge natoa Taarifa kwamba nitatoa hoja binafsi kutaka Bunge lako Tukufu kuunda Kamati Teule kufanya uchunguzi kuhusu vitendo vya utekaji, uteswaji na hata mauaji dhidi ya raia (suala la Ben Saanane likiwemo).
Pamoja na mambo mengine, Kamati teule hiyo pia nitapendekeza iangalie namna ya kufanya mabadiliko makubwa kwa Idara ya Usalama wa Taifa ili kuiondoa kuwa Idara ya utesaji na badala yake kuwa idara ya kulinda Wananchi, Rasilimali za nchi na Ulinzi wa Katiba ya nchi.
Naamini wabunge wenzangu mtaniunga mkono kwenye hili.
Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Mbunge - Kigoma Mjini (ACT Wazalendo)
Dodoma
Aprili 11, 2017
MBUNGE BASHE NAYE AWARUSHIA KOMBORA IDARA HIYO
Mbunge wa Nzega Mjini(CCM) Hussein Bashe amewataka wabunge wa CCM kuacha unafiki kuhusu kuwateka watu na kwamba yeye ni mmoja wa watu waliokamatwa na usalama wa taifa wakati wa mkutano Mkuu wa CCM.
"CCM acheni unafiki mimi nimeshakamatwa na watu wa usalama mnasema hawakamati, kwa hili nipo tayari mniondoe kwenye chama". Amesema Bashe
Bashe alikuja juu baada Waziri wa Tamisemi, George Simbachawene kumtaka Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe kuthibitisha kuwa matukio ya ukamataji yanafanywa na usalama wa Taifa