WIKI YA MAJI MKOA WA DSM: RC MAKONDA ATAJA MAFANIKIO, AWAPONGEZA DAWASA
Imeelezwa kuwa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASA) imejipanga vizuri kuhakikisha wanatumia wiki ya Maji iliyoanza 16-22 March,2017 kwa kuhakikisha kuwa wanatoa elimu juu ya ujenzi wa miradi ya maji pamoja na mipango ya baadae.
lengo likiwa ni kuwafanya wakazi wa jiji hilo kufahamu mafanikio ya miradi mbalimbali iliyokamilika na pia hatua ambazo zimefikiwa juu ya upatikanaji wa huduma za maji safi na maji taka katika Mkoa wa Dar es salaam.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wakati
akizungumza na waandishi wa habari,
Ameongeza kusema kuwa katika kuadhimisha Wiki
ya Maji, Mkoa wa Dar es Salaam umelenga kuwahamasisha na kuwa elimisha
Wananchi, Viongozi wa Serikali za Mitaa pamoja na Kamati za Maji kuhusu
namna bora ya usimamizi wa shughuli za maji katika maeneo yao ikiwemo na
taratibu za umiliki wa visima.
Amesema kuwa, lengo la maadhimisho hayo ni kuongeza upatikanaji wa
maji, uzalishaji na usambazaji wa maji safi na salama ambayo yatatumika
kwa uangalifu ili kupunguza kiwango cha matumizi yake.
Ameongeza kuwa, hali ilivyo sasa, kiwango kikubwa cha Majitaka kutoka
viwandani na majumbani kinaachwa kutiririka bila kutibiwa na kurudishwa
kutumika tena ambapo jambo hilo husababisha virutubisho vingi vilivyomo
katika maji hayo kupotea.
“Katika kuhakikisha maendeleo endelevu na mzunguko wa uchumi,
Majitaka ni rasilimali muhimu na hivyo kuyasindika, kuyasafisha kwa
kuyatibu na kuyatumia tena ni jambo la lazima”, Amesema Makonda.
Aidha, ameongeza kuwa, katika maadhimisho ya Wiki ya Maji, shughuli
za usafi na upandaji miti katika maeneo ya vyanzo vya maji zitafanyika,
miradi mitatu ya maji katika maeneo ya Mbagala pamoja na Pugu
itazinduliwa na pia miradi 20 ya Jamii itakabidhiwa rasmi DAWASCO.
Hata hivyo, Makondaa ameongeza kuwa, hali ya upatikanaji wa huduma ya
maji kwa Wakazi wa Dar es Salaam ni asilimia 75 ambapo uzalishaji wa
maji hayo kwa sasa ni lita Milioni 390 kwa siku wakati mahitaji ya maji
hayo kwa sasa ni ni lita Milioni 510 kwa siku.
Kwa upande wake Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maji Safi na
Majitaka Dar es Salaam (DAWASCO) Kiula Kingu amesema kuwa, DAWASCO
pamoja na DAWASA wamefanikiwa kuzuia upotevu wa maji kwa kiasi kikubwa
ambapo kwa mwaka jana ulikuwa ni asilimia 47 na mwaka huu umepungua na
kufikia asilimia 38.6.
Naye Meneja Mahusiano ya Jamii Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar
es Salaam (DAWASA) Neli Msuya amesema kuwa, maeneo yote ya Dar es Salaam
yasiyo na mtandao wa maji yamekuwa yakitengenezewa ramani (design) ili
yawekewe mitandao hiyo ya maji ili maji yaweze kupatikanakwa wakazi wa
maeneo hayo