BUNGE LIPITISHA MUSWAADA HUU LEO,SOMA HAPO KUJUA
Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo, Mjini
Dodoma limepisha Muswada wa Sheria ya Huduma ya Msaada wa Kisheria wa Mwaka
2016 (The Legal Aid Bill, 2016).
Waziri wa Mambo ya Katiba na Sheria Dkt. Harrison
Mwakyembe alipokuwa akitoa taarifa wakati wa kuwasilisha muswada huo amesema
kuwa muswada huo wa sheria umepitia hatua nyingi na umechukua muda mrefu hadi
kufikia hatua ya kujadiliwa na Bunge tukufu.
Aliendelea kwa kusema kuwa muswada huo unapendekeza
kutungwa kwa sheria ya msaada wa kisheria kwa lengo la kuanzisha (kwa mara ya
kwanza katika histori ya nchi) mfumo wa kisheria wa kusimamia, kuratibu,
kurasimisha na kutambua utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria katika mashauri
yote ya Jinai na Madai kwa mahitaji.
Aidha utaratibu uliokuwepo kwa miaka mingi kwa
upande wa Serikali unahusu baadhi tu ya makosa ya Jina, makosa yenye adhabu
kubwa kama vile ya kunyongwa hadi kufa na vifungo virefu. Ambapo huduma hiyo imekuwa
ikitolewa katika ngazi ya Mahakama Kuu pekee na kwa wigo mdogo tu pale
inapohitajika kwa maslahi ya haki na kwa maelekezo ya Jaji Mkuu au yeyote
aliyekasimiwa mamlaka ya kutoa maelekezo hayo.
“Kumekuwepo na ongezeko kubwa la mahitaji ya huduma
ya msaada wa kisheria na wasaidizi wa kisheria. Kutokana na hali hiyo, Serikali
imeona ulazima wa kuanzisha mfumo wa kusimamia na kuratibu utoaji wa huduma
hiyo ili kuhakikisha inatolewa na watu wenye sifa, kwa wahitaji halisi na kwa
taratibu zinazofahamika ili iendane na matakwa ya kikatiba,” alifafanua Dkt.
Mwakyembe.
Vile vile ameeleza kuwa muswada huo unalenga
kuwatambua wasaidizi wa kisheria, kufuta sheria ya msaada wa kisheria (katika
mashauri ya Jinai).
Kwa upande wake Mbunge Selemani Zedi amesema kuwa,
muswada huo utawasaidia wananchi ambao hawana uwezo wa kuwalipa Mawakili
wanapohitaji msaada wa Kisheria.
Aidha, Naibu Spika Dkt. Tulia Ackson ameipongeza
Serikali kwa muswada huo muhimu ambao Bunge umeipitisha unasuobiria kutiwa
saini na Mhe. Rais ili kuwa Sheria.