WAZIRI MKUU AWASHUKIA WATUMISHI WA HALMASHAURI,SOMA HAPO KUJUA
WAZIRI MKUU Kassm Majaliwa amesema wakati umefika wa
kuwa na watumishi wenye weledi wa kutosha kwenye Halmashauri zote nchini na pia
hazitakiwi kuwa pango la wezi, wazembe au jalala la kutupa wabadhilifu
walioshindikana kwingineko.
Aidha, Waziri Mkuu amesemma Serikali za Mitaa na
Halmashauri zote nchini zinatakiwa zianze kujitathmini na kujipanga vizuri
zaidi kuona ni kwa namna gani zitakuwa chachu ya maendeleo ya viwanda
vinavyotarajiwa.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumatatu, Januari
30, 2017) wakati akifungua Kikao cha Baraza la Mashauriano (RCC) mkoani Dodoma.
Amesema kikao ni chombo muhimu na endapo kitatumika vizuri kitaweza kusaidia
kusukuma maendeleo ya Mkoa na kupunguza migogoro kwenye Halmashauri.
Amesema Serikali itaendelea kuongeza kiwango cha
ruzuku kwa Halmashauri zote nchini kwa kadiri uwezo utakavyoruhusu na
kusisitiza kwamba fedha hizo lazima zisimamiwe vizuri na zielekezwe kwenye
miradi ya maendeleo inayowagusa wananchi.
“Endapo itabainika kwamba kuna baadhi ya Sheria
zinazokwamisha utendaji katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, hatutasita
kuzifanyia mapitio na hatimaye kuzibadili ili ziendane na azma yetu ya kutoa
huduma bora kwa wananchi,” amesema.
Amesema Serikali ina maslahi makubwa kwa Serikali za
Mitaa, sio tu kwa kuwa ni Serikali kamili katika ngazi hiyo, bali pia kutokana
na ukweli kwamba kero nyingi za wananchi ziko katika ngazi hiyo.
Waziri Mkuu amesema vyanzo vingi vya mapato ya
Serikali vinapatikana kwenye Halmashauri huku changamoto kubwa ikiwa ni kulegalega
kwa Halmashauri nyingi katika ukusanyaji wa mapato ya kodi na yasiyo ya
kodi jambo linalozorotesha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Hivyo Waziri Mkuu ametoa rai kwa Halmashauri hizo
kuendelea kuboresha huduma kwa wananchi na kutatua kero zao kikamilifu na kwa
wakati pamoja na kubuni vyanzo vipya vya mapato na kuongeza kasi ya ukusanyaji
wa mapato.
Pia zihakikishe malipo yote yanafanyika kwa njia za
kielektoniki na zihamasishe vijana na akina mama wajiunge kwenye vikundi vya
uzalishaji mali na kuwapatia stadi za kazi na mikopo yenye masharti nafuu ili
waweze kuwa chanzo cha mapato hapo baadaye.
Amesema watendaji wa Halmashauri wanatakiwa
kujiepusha na vitendo vya rushwa na ubadhilifu wa mali za umma na uzembe kazini
na watakaobainika kufanya vitendo hivyo wachukuliwe hatua kali za
kisheria na kinidhamu.
“Someni taarifa ya CAG (Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa
Hesabu za Serikali) na kutoa majibu ya kina ya namna mtakavyodhibiti mianya ya
rushwa na ubadhilifu kama ilivyoainishwa kwenye ripoti hizo,” amesema.
Hata hivyo amesema kila Halmashauri iandae mpango wa
utekelezaji wa Ilani ya CCM kwenye maeneo makubwa ya kipaumbele kama vile
ujenzi wa miundombinu ya shule, maboresho kwenye sekta ya afya (ujenzi wa
hospitali, zahanati na vituo vya afya).
“Endeleeni kuwa na mahusiano mazuri miongoni mwenu,
mfanye kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu. Kila mmoja kwa
nafasi aliyonayo atimize wajibu wake na kuzingatia mipaka ya nafasi yake.
Punguzeni migogoro, matusi, dharau, bezo na vitisho. Mshirikiane na jamii ione
mpo wamoja,” amesema.