Zinazobamba

BAADA YA JALI YA TRENI,UONGOZI WA KAMPUNI YA RELI YATOA TAARIFA HII MPYA,SOMA HAPO KUJUA



 
Uongozi wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) umetoa taarifa kuwa kuanzia saa 9 alasiri leo Januari 30, 2017 njia ya reli kati ya Kituo Kikuu cha Dar es salaam na Ruvu imefunguliwa rasmi kwa shughuli za uendeshaji wa reli.

Taarifa hiyo imesema kuwa kazi ya ufunguaji njia imewezekana baada ya Wahandisi na Mafundi wa reli kuyaondoa Mabehewa yaliopata ajali  kutoka relini na pia kuikarabati sehemu iliyoharibika . Kazi hiyo imefanyika kuanzia usiku wa Januari 29, 2017 hadi mchana wa Januari 30, 2017.

Aidha treni ya abiria iliyoahirisha safari ya kuondoka kwenda bara jana imeondoka leo saa 9:05 alasiri kutoka kituo kikuu cha Dar es Salaam kwenda bara..

Wakati huo huo imefahamika kuwa msafiri mmoja aliyetambulikana kama Nd Basekena O. Bango kutoka Bujumbura Burundi akiwa anasafiri kutoka Kigoma amelazwa katika Hospitali ya Tumbi Kibaha mkoani wa Pwani kwa ajili ya matibabu zaidi. Aligunduliwa kuwa amechanika mguu wake wa kulia hivyo basi kuhitaji kushonwa mguu wake huo.

Taarifa kutoka Muhimbili zinaeleza kulazwa kwa majeruhi wawili waliopokelewa hospitalini hapo usiku wa Januari 29, 2017. Majeruhi wamefahamika kuwa ni Nd. Stephania Mbona (46) kutoka Kigoma alikuwa amekuja Muhimbili kuendelea na matibabu ya ugonjwa wa tumbo, hata hivyo alitibiwa majeraha ya kawaida na anaendelea kulazwa kwa ajili ya matibabu ya ugonjwa wake wa tumbo.

Mgonjwa wa pili Nd Alice Jovin (37) mkazi wa Salasala Dar es Salaam alikuwa anatoka Kigoma kuja Dar es Salaam amepata majeraha ya kawadia ametibiwa na alitarajiwa kuruhusiwa leo asubuhi.

Kuhusu idadi ya wasafiri treni ya Deluxe yenye uwezo wa kusafirisha abiria zaidi ya 1000 wakati inapata ajali ilikuwa na abiria 480.

Aidha imefahamika kuwa ili kufahamika hasara na sababu za ajali hiyo taarifa rasmi itatolewa baada ya uchunguzi wa Kamati maalum inayoundwa kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni za uendeshaji reli za kimataifa. Taarifa hiyo itatolewa baada ya wiki mbili.

Imetolewa na Afisi ya Uhusiano:
Kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TRL
Ndugu Masanja Kungu Kadogosa
Januari 30, 2017
DAR ES SALAAM