UTUMBUAJI MAJIPU KWA WAFANYAKAZI WA SERIKALI ZA MITAA WAWACHUKIZA TALGWU,SOMA HAPO KUJUA
CHAMA cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania
(TALGWU) kimevunja ukimya na kuwataka viongozi wa Serikali, hasa wakuu wa
mikoa na wilaya kuacha mara moja kutumia madaraka yao vibaya dhidi ya
wafanyakazi.
TALGWU imesema kuwa viongozi hao wamekuwa wakitumia
kile wanachodai utumbuaji kwa watendaji kiuonevu na ukiukwaji sheria za nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es
Salaam, Katibu Mkuu wa TALGWU, Rashid Mtima, alisema baadhi ya viongozi wa
kisiasa wamekuwa wakitumia nafasi hiyo kama njia ya kujipatia sifa ama
kuonyesha mabavu ya mamlaka yao.
Alisema viongozi hao wamethubutu kutumia vibaya
nafasi zao kwa kuendeleza manyanyaso kwa wafanyakazi wa kada ya watendaji wa
vijiji, mitaa na kata, wakiwaadhibu bila kufuata utaratibu wa kiutumishi, huku
mamlaka zinazopaswa kutumika kwa kazi hiyo zikiporwa madaraka yake kwa nguvu ya
kisiasa.
“Jambo hili ni baya na la hatari kwa mujibu wa
mustakabali wa utawala wa sheria na linapaswa kukemewa mara moja na kwa nguvu
zote kwa sababu likiachwa lina madhara makubwa.
“Tumeshuhudia matukio ya udhalilishaji na ukiukwaji
wa taratibu za kazi wakifanyiwa kada hii, maofisa watendaji wamekuwa wakiwekwa
ndani ovyo kana kwamba wametenda makosa ya jinai, kutukanwa na kudharauliwa
hadharani na wanasiasa, kusimamishwa kazi ovyo bila kuzingatia mamlaka zao za
ajira.
“Kwa mfano Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi,
aliwaweka ndani watendaji wanne wa Kata ya Mikocheni kwa kushindwa kutekeleza
maagizo yake, vilevile Hapi alipotembelea Kata ya Kawe aliwaweka ndani
watendaji watatu wa mtaa kwa kosa la kuwapa mashine za kukusanyia fedha
wakandarasi na kutounda vikundi vya ulinzi shirikishi,” alisema Mtima.
Katibu mkuu huyo alisema kuwa sheria ya tawala za
mikoa ya mwaka 1997 inampa mamlaka mkuu wa mkoa katika kifungu cha 7 (1) hadi
(9) na mkuu wa wilaya katika kifungu cha 15 (1) hadi (9) ya kuamrisha mtu
yeyote kuwekwa ndani kwa kuona mbele yake au ufahamu wake mtu huyo kuwa
ametenda kosa.
Alisema kifungu kidogo cha (2) cha sheria hiyo
kinamtaka mkuu wa mkoa au wilaya kufanya hivyo pale ambapo atakuwa
amejihakikishia kuwa kosa lililotendwa na mhusika ni lazima litasababisha
uvunjivu wa amani kwa mtendaji na jamii kwa jumla na hakuna njia mbadala zaidi
ya kumuweka ndani.
“Pia kifungu (3) kinamtaka mtu aliyekamatwa kwa amri
au maelekezo ya mkuu wa mkoa au wilaya afikishwe mahakamani ndani ya saa 48 kwa
ajili ya kufunguliwa mashtaka ya jinai. Endapo hatofikishwa mahakamani kwa muda
unaopaswa na kuisha, anapaswa kauchiwa na hapaswi kukamatwa tena,” alisema.
Alisema kwa tafsiri hiyo ya kisheria, ni kwamba
viongozi wa kisiasa hawazingatii sheria hiyo kikamilifu na ni uonevu mkubwa kwa
watumishi waliowekwa ndani.
“Swali la kujiuliza je, uchunguzi ukishakamilika na
ikaonekana watendaji waliotangazwa hadharani na kudhalilishwa walionewa,
viongozi hao wa Serikali watatumia vyombo vya habari kusafisha majina ya
watendaji hao?” alisema na kuhoji.
Mtima alisema kuwa TALGWU haitetei wafanyakazi ambao
wanakwenda kinyume na sheria, kanuni na taratibu za kazi, lakini inataka
utaratibu ufuatwe na hatimaye watuhumiwa wachukuliwe hatua stahiki.
“Wito wetu viongozi wa kisiasa wenye tabia hiyo
watambue dhamana kubwa waliyopewa na Taifa, watumie mamlaka yao kwa mujibu wa
sheria, kanuni na taratibu za nchi vinginevyo kama chama hatutasita kuchukua
hatua za kisheria,” alisema Mtima