MCT,LHRC.TDRC WAIBURUZA SERIKALI YA JPM MAHAKAMANI,NI KUPINGA SHERIA YA MPYA YA VYOMBO VYA HABARI,SOMA HAPO KUJUA
Baraza
la Habari Tanzania (MCT), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na
Mtandao wa Haki za Binadamu Tanzania ( THRDC) leo Jumatano ya Januari 11, 2017
wamefungua kesi ya kuipinga Sheria Mpya ya Huduma za Vyombo vya Habari namba 12
ya mwaka 2016 katika Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ).
Akizungumza
na waandishi wa habari baada ya kufunguliwa kesi hiyo, Katibu Mtendaji MCT,
Kajubi Mukajanga amesema washirika waliofungua kesi hiyo wanataka baadhi ya
vifungu vya sheria vinavyokandamiza uhuru wa habari na kujieleza vifutwe
kwakuwa vinakiuka matakwa ya mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Na
kwamba mahakama ya EACJ imepewa mamlaka ya kutafsiri mkataba huo na kuhakikisha
nchi wanachama wanaufuata na kuusimamia.
“Vifungu
hivyo vya sheria vinakandamiza uhuru wa habari na wa kujieleza, vifutwe kwani
vinakiuka matakwa ya mkataba wa EAC ambao unataka nchi mwanachama kuzingatia na
kulinda haki ambazo zimeelezwa katika mkataba huo kwenye ibara ya 6(d) na
7(2),”
amesema.
Amesema
kuwa, Ibara ya 6(d) ya mkataba wa EAC inahimiza umuhimu wa kufuata kanuni za
utawala bora, wa kidemokrasia, sheria, uwajibikaji, uwazi na haki kwa wote
ikiwa pamoja na usawa wa kijinsia, kulinda na kuheshimu haki za binadamu.
“Kama
ilivyo kwenye kifungu cha 8(1) (c), Tanzania inatakiwa kuchukua hatua za
kuhakikisha haki zote zinazotajwa katika mkataba huo zinafuatwa na
kutekelezwa,”
amesema.
Mkurugenzi
Mtendaji wa LHRC, Helen Kijo-Bisimba amesema baadhi ya vifungu vya sheria hiyo
vinakiuka haki za binadamu na kwamba wameshiriki kufungua kesi hiyo ili
kuipinga sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari.
“Sheria
imekaa sivyo, tumeona tuungane na wenzetu ili kuipinga sheria hii,” amesema.
Mkurugenzi
wa THRDC, Onesmo Olengurumwa amesema sheria inabidi ibadilishwe hasa katika
vifungu kandamizi kabla ya kuanza kutumika.
“Kuna
mazingira yatakayowaweka katika mazingira magumu waandishi wa habari, ni vyema
kuipinga sheria hii isitumike hadi ibadilishwe.”