Zinazobamba

LOWASSA NA MAALIM SEIF WAUNDA UTATU MTAKATIFU,WATEMA CHECHE NZITO ZANZIBAR,SOMA HAPO KUJUA

 
Katibu  Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad,  amesema kukaa kwake kimya kuna kishindo kikubwa kinakuja visiwani Zanzibar.

Maalim Seif ambaye aliwahi kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa visiwani humo, alisema kamwe hatorudi nyuma, kwani hajashindwa na wala haitotokea kushindwa katika maisha yake.

Kauli hiyo aliitoa jana mjini Unguja, alipokuwa akizungumza katika uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Dimani, ambapo pamoja na mambo mengine alisema umaskini sasa umekuwa ukiwatesa wananchi katika kila eneo.

Katika uchaguzi huo CUF inawakilishwa na mgombea wake Abdulrazak Khatib Ramadhan ambaye anapambana vikali na mgombea wa CCM, Juma Ali Juma.

Maalim Seif ni kama alikuwa akijibu mapigo ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdurhamn Kinana ambaye mwishoni mwa wiki alisema kuwa kiongozi huyo anazungumza hali ya kuwa hajui lolote kinachoendelea katika nchi wala katika chama chake.

“Sasa nawaambieni musinione kimya, kimya kikuu kina mshindo mkubwa wala usidhani kuwa tumeshaachia hapana bado kabisa tunaendelea kupigania haki yenu na haki Inshallah haipo mbali na mimi niwaambieni vijana sijashindwa na sitoshindwa.

“…na kama itatokea bahati mbaya nishindwe nitawataarifuni mchukue uamuzi wenu lakini sitegemei kufika huko kwani mambo haya yana miiko yake,’’ alisema Maalim Seif.

Akizungumzia hali ya umaskini nchini alisema tangu uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano, ulipoingia madarakani kwa kile alichodai kwa kutumia mabavu hali ya umaskini imeendelea kuwatesa wananchi.

Alisema hali hiyo inachangiwa na uongozi kufanya mambo yasiyokuwa na tija ambapo kwa kushirikiana na kiongozi mstaafu wa Serikali iliyopita walifanya mapinduzi na kubatilisha matokeo ya  uchaguzi yaliyofanywa na Wazanzibari waliyoyafanya Oktoba 25, mwaka 2015.

“Lakini  kilichotokea mwaka juzi sasa Serikali imekuwa ya dhulma wale wenye ajira wanapokonywaa ajira zao  ikiwemo kuwaondosha wafanyabiashara darajani, Kijangwani na sasa wanakwenda Michenzani jambo ambalo ni hatari kwa Taifa hili,’’ alisema Maalim Seif.

Katibu Mkuu huyo wa CUF ambaye alikuwa mgombea urais katika uchaguzi uliopita, alisema pamoja na hali hiyo lakini bado suala la mafuta na gesi limekuwa na upungufu hasa kupitia sheria yake ambapo sasa kunaifanya Zanzibar kuwa kama manispaa.

Naye aliyekuwa mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), aliyeungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) Edward Lowassa,  alimpongeza Maalim Seif kwa kumwalika na jinsi alivyokuwa mvumilivu katika mambo yote wanayomfanyia.

Alisema Maalim Seif alimshinda aliyekuwa mgombea urais wa CCM, Rais Dk. Ali Mohamed Shein  kwa wastani wa kura 16,000.

Kutokana na hilo aliwashukuru vijana waliosikia wito wake wa kutofanya vurugu baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo kwani kama wangefanya hivyo kulikuwa na hatari ya kupoteza maisha.

Akizungumzia suala la njaa  alisema ni ajabu kwa Rais aliyepo madarakani kubeza suala hilo.

Lowassa alisema kuwa wakati wa utawala wa Rais wa Awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere, hasa pale nchi ilipokubwa na baa la njaa, alisema yupo tayari kuzungumza na makaburu  ili kuweza kukabiliana na baa hilo lililoikumba nchi kwa wakati huo.

Alisema ni lazima kuhakikisha katika uchaguzi mbalimbali kunakuwa na ushindi na kila mmoja akatae azuie wizi wa kura kama uliotokea 2015.

“Lazima kukataa kuibiwa kura ni lazima kukataa kutiwa hofu na kutishwa hii ni nchi yetu sote tufuate sheria na uchaguzi ujao ni lazima kushinda na viongozi wanaopambana ni lazima kuungwa mkono kama ilivyokuwa kwa Maalim Seif ni mfano wa kuigwa,’’ alisema Lowassa.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar,  Nassor  Mazrui alisema wanaingia katika uchaguzi huo bila kuwa na ruzuku lakini hadi sasa tayari Sh milioni 20.4 zimepatikana kutoka kwa wanachama wenyewe.

Aliyashukuru majimbo yaliyochanga ikiwa ni pamoja na Nungwi, Makunduchi, Mtoni, Magomeni, Kikwajuni, Konde, Chambani, Chakechake, Chonga, Bububu na Ole.

Naye Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi Zanzibar,  alisema wataendesha kampeni kistaarabu tofauti na wa upande wa pili ambao ni CCM wanaorusha maneno badala kueleza sera.

Alitoa ratiba za kampeni hiyo ambapo Januari 11 atakuwepo Mbunge wa Singida Tundu Lisu na Januari 15 Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro atakuwa mgeni rasmi.