YUSUFU MANJI HATARINI KUKAMATWA,SOMA HAPO KUJUA
Siku moja baada ya mfanyabiashara Yusuf Manji kuhama
kwenye jengo la Quality Plaza, uongozi wa kampuni ya udalali ya Yono umesema
kinachosubiriwa ni mfanyabiashara huyo kulipa deni au kukamatwa kwa mali zake.
Akizungumza jana, Mwenyekiti wa Bodi ya kampuni
hiyo, Stanley Kevela alisema Manji alipewa siku 14 zilizoanza kuhesabiwa tangu
Jumamosi ili kulipa deni.
Alisema endapo siku hizo zitamalizika bila kulipwa,
mali za mfanyabiashara huyo zitakamatwa ili kufidia deni la Dola 6.1 milioni za
Marekani (zaidi ya Sh13 bilioni) anazodaiwa.
Kevela alisema fedha hizo ni gharama ya kupanga
kwenye jengo hilo ambalo ni mali ya Mfuko wa Pensheni wa Watumishi wa Umma
(PSPF).
Alisema baada ya kukamilika kwa mchakato huo,
kampuni italikabidhi jengo hilo kwa PSPF kwa ajili ya shughuli nyingine.
Mfanyabiashara huyo alipotafutwa jana ili
kuzungumzia suala hilo, simu yake ya mkononi haikupatikana.
Mkurugenzi wa kampuni ya Yono, Skolastika Kevela
alisema kazi ya kuondoa mali za mpangaji kwenye jengo hilo ilikamilika juzi.
“Kampuni zote zimeshaondoa vifaa na
milango ya jengo hilo imefungwa kwa kufuli za kampuni yetu. Tutalisimamia jengo
hadi tutakapowakabidhi PSPF,” alisema.
Uamuzi wa Manji kuhamishwa kwenye jengo hilo
ulitolewa na Mahakama kutokana na kushindwa kulipa kodi ya pango ambapo
alipewa masaa 24 ya kuondoa vitu vyake.