SHERIA MPYA YA MADAWA YA KULEVYA NI KIBOKO,KIJANA AFTUPWA JERA MIAKA 30 KISA AKUTWA NA BANGI TU,SOMA HAPO KUJUA
Fundi wa kuziba pancha, Harson Solomon (38), mkazi
wa wilayani hapa amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kutiwa hatiani
kwa kupatikana na misokoto 601 ya bangi.
Kifungo hicho kimeangukia sheria mpya ya udhibiti wa
dawa za kulevya iliyosainiwa Mei 11, 2015 na aliyekuwa Rais wakati huo, Jakaya
Kikwete. Imeelezwa Solomon ni miongoni mwa washtakiwa wa mwanzo kufungwa kwa
sheria hiyo.
Awali, sheria ilikuwa inatoa mwanya wa faini na mtu
anaposhindwa kulipa ndipo hutumikia kifungo jela lakini hivi sasa anayepatikana
na hatia ya kukutwa na kiwango kikubwa hutupwa jela.
Kifungu cha 11(1) D cha sheria hiyo mpya, kinaeleza
wazi mtu anayezalisha, kumiliki, kuuza, kununua au kusafirisha dawa za kulevya
ikiwamo bangi, adhabu ya chini ni kifungo cha miaka 30 jela.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi,
Joachim Tiganga baada ya kuridhishwa bila kuacha shaka na ushahidi wa upande wa
mashtaka.
Wakili wa Serikali, Ignas Mwinuka alidai kortini
kuwa Desemba 1, 2015 katika maeneo ya Mwika Kimangara, Moshi Vijijini
mshitakiwa alipatikana na kiasi hicho cha bangi.
Pia, anadaiwa kuruhusu eneo lake kutumika
kuuza bangi na gongo.
Akisoma hukumu, Hakimu Tiganga alisema matumizi ya
dawa za kulevya yanazidi kuongezeka nchini na kuathiri jamii, hivyo Mahakama
inatoa adhabu hiyo iwe fundisho kwa wengine.
Katika kipindi chote tangu afikishwe kortini kwa
mara ya kwanza Desemba 11 mwaka jana, mshtakiwa alikana mashtaka hadi alipotiwa
hatiani na kuhukumiwa jana.