WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA AZIPIGA MIKWARA HALMASHAURI,SOMA HAPO KUJUA
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa
Wilaya ya Karatu, Bi. Theresia Mahongo kuhakikisha kampuni zinazomilikiwa na
madiwani na watumishi wa halmashauri hiyo hazipewi zabuni zinazotolewa
katika maeneo yao kwa ajiliya kuepusha migongano ya kimaslahi.
Ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Desemba 5, 2016)
wakati akizungumza na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Karatu mkoani
Arusha katika ukumbi bwalo la Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Karatu
akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani hapa.
"Hauzuiliwi kufanya biashara ili mradi kampuni
yako isifanye kazi katika halmashauri ambayo wewe unaitumikia na una nguvu nayo
ili kuepusha migongano ya kimaslahi kwani miradi yote utajilundikia,"
amesema.
Pia amewataka Wakuu wa Idara katika halmashauri hiyo
walisaidie Baraza la Madiwani katika kubaini vyanzo vipya vya mapato kwa lengo
la kuongeza mapato ya halmashauri yao.
Wakati huo huo Waziri Mkuu amewataka watumishi wa
halmashauri wa umma kujitathmini na kujiridhisha kama wanafuata misingi
ya utumishi katika utendaji kazi wao wa kila siku. Amewasisitiza
wawatumikie wananchi kwa uadilifu na uaminifu mkubwa.
"Hatuhitaji kuwa na mtumishi mvivu,
asiyewajibika, mwizi, mla rushwa na asiyekuwa muadilifu mahali pa kazi.Na
atakayeona ameshindwa kutunza na kusimamia fedha za miradi ya maendeleo ya
wananchi atoe taarifa hatutaki watu kufanya kazi kwa mazoea," amesema.
Waziri Mkuu ameongeza kuwa " watumishi wa umma
lazima mbadilike na muwe na nidhamu ya kazi. Muache malalamiko fanyeni kazi na
msitafute sympathy (huruma) kutoka kwa watu kwani Serikali haitamuonea
mtumishi yeyote ," amesema.
Amesema katika baadhi ya ofisi za Serikali kuna
ugonjwa wa watumishi wanapoona wageni wamelifika kwa ajili ya kupatiwa huduma
wanawapita bila ya kuwasikiliza. " sasa hatutaki watumishi wa namna hiyo,
Jukumu lako ni kumtumikia Mtanzania na tunataka kuona mabadiliko. Hatutaki
kuona watu wakizubaa maofisini,".
Waziri Mkuu amesema Serikali ikikuta wananchi
wanalalamika kutokana na kutoridhishwa na huduma zitolewazo na watumishi
wa umma itahakikisha watumishi hao wanachukuliwa hatua. Serikali ni ya
Watanzania wote hivyo lazima wahudumiwe vizuri bila ya kujali uwezo wao kifedha
wala itikadi zao za kidini na kisiasa.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMATATU, DESEMBA 5, 2016.