TAARIFA MUHIMU KUHUSU FARU JOHN WA KASSIM MAJALIWA,SOMA HAPO KUJUA
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amepokea taarifa
inayoelezea utaratibu uliotumika kumhamisha faru John kutoka Hifadhi ya
Ngorongoro kwenda Sasakwa Black Rhino Sanctuary iliyoko kwenye Hifadhi ya
Grumeti.
Akizungumza katika kikao kilichofanyika nyumbani
kwake Oysterbay leo mchana na kuhudhuriwa na Waziri wa Maliasili na Utalii,
Profesa Jumanne Maghembe na baadhi ya watendaji wa wizara yake, Waziri Mkuu
amesema taarifa hiyo itafanyiwa kazi na wataalamu wa ofisi yake.
Akisoma taarifa hiyo mbele ya Waziri Mkuu, Profesa
Maghembe amesema hadi kufikia Desemba 2015 wakati Faru John anahamishwa alikuwa
na watoto 26 (sawa na asilimia 70.2) ya faru wote waliokuwepo ndani ya kreta.
“Uamuzi wa kumuondoa John ulikuwa ni muhimu ili
kuwezesha kuongezeka kwa faru weusi na kupunguza tatizo la ‘inbreeding’ ndani
ya Hifadhi ya Ngorongoro,” alisema Waziri Maghembe
Baada ya kuhamishiwa Sasakwa, Waziri Maghembe
alisema Julai 10, 2016 afya ya faru John ilianza kudorora na alikufa tarehe 18
Agosti, mwaka huu. Taarifa hiyo iliandaliwa na Kamati ya Taifa ya kuwalinda
tembo na faru. Kamati hiyo inaundwa na Mkurugenzi Mkuu wa Tawiri, Mkurugenzi
Mkuu wa Tanapa, Mkurugenzi Mkuu wa NCAA na Mhifadhi Mkuu wa Ngorongoro.
Akikabidhi pembe za faru huyo mbele ya Waziri Mkuu,
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Kupambana na Ujangili wa Wanyamapori,
Robert Mande alimweleza kwamba pembe kubwa ya faru John ilikuwa na uzito wa
kilo 3.6 na pembe ndogo ilikuwa na uzito wa kilo 2.3.
Watendaji wa wizara waliohudhuria kikao hicho ni
Kaimu Katibu Mkuu, Iddi Mfunda; Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya
Ngorongoro (NCAA), Freddy Manongi; Mkurugenzi Mkuu wa Tawiri, Simon Mduma;
Kaimu Mkurugenzi Idara ya Wanyamapori, Alexander Songorwa na Mkuu wa Pori la
Akiba la Ikorongo/Grumeti, Nollasco Ngowe.
Desemba 6, mwaka huu, akiwa ziarani mkoani Arusha,
Waziri Mkuu aliuagiza uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA),
umletee nyaraka zote zilizotumika kumhamisha faru maarufu kwa jina la ‘John’
kutoka kwenye hifadhi hiyo ifikapo Alhamisi, Desemba 8.