RAIS MAGUFULI AMEKAMIA SERIKALI KUHAMIA DODOMA,AAGIZA SHEREHE ZA UHURU KUHAMIA DODOMA,SOMA HAPO KUJUA
Sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Tanzania
Bara zitakuwa zikifanyika mjini Dodoma kuanzia mwaka 2017 badala ya Jijini Dar
es Salaam kama ilivyozoeleka.
Uamuzi huo umetangazwa leo na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi ya Ulinzi na Usalama Dkt.
John Magufuli, wakati akitoa salamu zake za maadhimisho ya miaka 55 ya Uhuru wa
Tanzania Bara, kwenye sherehe zilizofanyika leo katika uwanja wa Uhuru dar es
Salaam.
Katika salamu hizo, Rais Magufuli ambaye ndiye
aliyekuwa mgeni rasmi, ameeleza sababu za kufuta sherehe hizo mwaka jana na
kuruhusu mwaka huu zifanyike ambapo amesema sababu moja wapo iliyomfanya afute
sherehe hizo mwaka jana ni kubana matumizi.
"Mwaka jana nilipouliza gharama za sherehe zile
nikaambiwa ni shilingi bilioni 4, nikashangaa, bilioni 4 zote ni za nini?"
Amesema Rais Magufuli.
Kuhusu sababu za kuruhusu mwaka huu sherehe hizo
zifanyike, Rais Magufuli ametaja sababu mbili ambazo ni pamoja na kutumia
gharama ndogo huku sababu ya pili akiitaja kuwa ni kutokana na kwamba
hizi ni sherehe za mwisho za Uhuru kufanyika Jijini Dar es Salaam huku akieleza
kuwa kuanzia mwaka 2017, sherehe hizo zitakuwa zikifanyika katika makao makuu
ya nchi Dodoma.
"Mwaka huu gharama ni ndogo, hata kula wala
kunywa hakuna, baada ya hapa hakuna kula wala kunywa"
Rais Magufuli pia ametumia nafasi hiyo kuelezea
mafanikio ya Tanzania katika miaka yake 55 ya Uhuru, huku akieleza mikakati ya
serikali yake ya awamu ya tano katika kuifikisha nchi kwenye kipato cha kati na
kuwashukuru viongozi wakuu wa awamu zilizopita.
Kaulimbiu ya sherehe hizo kwa mwaka huu ni: Tuunge
mkono jitihada za kupinga rushwa na ufisadi na tuimarishe uchumi wa viwanda kwa
maendeleo yetu.