MTOTO WA KIKWETE NA MBUNGE PROFESA JAY WAINYOSHEA KIDOLE SERIKALI YA JPM,SOMA HAPO KUJUA
Wabunge wa Mikumi, Joseph Haule na Chalinze,
Ridhiwan Kikwete wamelaani kitendo kilichofanywa na jamii ya wafugaji kwa
kujichukulia sheria mkononi na kumjeruhi kwa mkuki mkulima Augustine Mtitu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, kuhusu tukio
hilo lilitokea katika kijiji cha Upangwani, Masanze, Mikumi, wabunge hao
waliezea kusikitishwa kwao na kutaka hatua zichukuliwe.
“Ni kitendo cha kusikitisha sana kwa
hawa ndugu zetu wafugaji walijiamulia kufanya kitendo cha kinyama kama hiki,
huu si ubinadamu kabisa,” alisema Haule.
Alisema mkulima huyo alichomwa mkuki na wafugaji wa
Kimasai alipokuwa akimsaidia jirani yake kufukuza ng’ombe wasiharibu mazao
shambani mwake.
Alisema Mwenyekiti wa Kijiji na Mwenyekiti wa
Kitongoji nao walijeruhiwa na wafugaji hao. “Sisi Ofisi ya Mbunge wa Mikumi
tunatoa mwito kwa Serikali kubaini waliofanya vitendo hivyo na kuwakamata ili
kuvikomesha,” alisema Haule.
Alisema atashirikiana na Serikali kukomesha migogoro
isiyokwisha kati ya wakulima na wafugaji Kilosa.
Ridhiwan naye alilaani vitendo hivyo na kuishauri
Serikali kutafuta suluhu ya kudumu ya tatizo hilo.
“Ni lazima Serikali ije na majibu
sahihi, ili kunusuru vita vya wenyewe kwa wenyewe visitokee kati ya jamii hizo.
Si ajabu kusikia mtu kavunjwa mgongo, mwingine mlemavu, leo kapigwa mkuki wa
midomo ukatokea shingoni, kilio hiki kipo katika masikio ya watu wengi kuhusu
mapigano ya wakulima na wafugaji,” alisema.
Aliongeza: “Serikali isikie hili na kuchukua
hatua stahiki ya kudhibiti kabla damu ya Watanzania wanyonge wanaotegemea
kilimo kama kiinua mgongo chao hawajapotea. Kuna sheria na mipango ya matumizi
bora ya ardhi, zitumike.”
Ridhiwan alisema jambo la msingi ambalo Serikali
inatakiwa kujua ni kwamba hali ilivyo sasa, si ya kufanyia mzaha na waziri
husika ayafanyie kazi.
Alisema binafsi analaani vitendo hivyo na kuiasa
Serikali kujipanga vizuri kabla mambo hayajaharibika. “Yalianza Kilosa,
Mvomero, Chalinze, Handeni, Kiteto na sasa Mikumi. Serikali jipangeni, kabla
hapajachafuka,” alihadharisha.