MAASKOFU WATUMIA SIKUKU KUISHAURI SERIKALI YA JPM,SOMA HAPO KUJUA
MAADILI kwa watumishi wa umma yameporomoka kutokana
na viongozi hao kutomjua Mungu, anaandika Dany Tibason.
Ni
kauli ya Christopher Madole, Askofu wa Kanisa la Gospel Ministry Jimbo la
Dodoma aliyoitoa Jana alipokuwa akihubiri katika kanisa hilo lililopo viwanja
vya Reli mjini Dodoma.
Alikuwa akiendesha ibada ya Siku ya Kumbukumbu ya
Kuzaliwa kwa Yesu Kristo ambapo amesema, umefika wakati sasa wa wanasiasa na
viongozi mbalimbali serikalini kuwa na hofu ya Mungu na sio kuigiza.
“… namshauri Rais Magufuli (Rais John Magufuli)
aongeze wizara moja tu ya maadili ambayo waziri wake asitokane na chama
chochote cha siasa.
“Maana tunaona kuna wakati mawaziri wanaonekana
kutetea vyama vyao sasa hii wizara ya maadili itakuwa inasimamiwa na kiongozi
wa kiroho,”amesema Askofu Madole.
Amesema kwamba, kutokana na kuporomoka kwa maadili,
mawaziri na wabunge wamekosa aibu na hata kuwa na maneno ya kashfa ndani ya
Bunge.
“Kumekuwepo na maneno ya kashfa hata ndani ya bunge,
mfano; mbunge anasema sizungumzi na mbwa bali nazungumza na mwenye mbwa au
kusikia mbunge anasema funga milango tupigane,” amesema.
Askofu Madole amesema kuwa, yote hayo ni dalili ya
watu kukosa hekima na busara na zaidi ni kukosa hofu ya Mungu jambo ambalo ni
hatari kwa viongozi na jamii kwa ujumla.
Kiongozi huyo wa imani amesema kwamba, wanasiasa
sasa wamekuwa chanzo cha machafuko katika nchi zao kutokana na kuwa na tabia ya
kutopenda kuachia madaraka sambamba na kukandaniza demokrasia.
Pia imeelezwa kwamba, wanasiasa wanakumbwa na tabia
hiyo kutokana na kuwa na uchu wa madaraka jambo ambalo linatokana na kutokuwa
na hofu ya Mungu.
Askofu Madele amesema yapo mataifa ambayo yanaingia
katika machafuko kutokana na watawala wa nchi husika kukataa kutoka madarakani
licha ya kumaliza muda wao.
Kiongozi huyo ametolea mfano wa rais wa Ghambia
ambaye alishindwa katika uchaguzi mkuu wa urais na kukubali matokeo lakini muda
mfupi alijitokeza na kupinga.