MSIBA MZITO LEO KUTOKA NDANI YA JESHI LA POLISI,SOMA HAPO KUJUA
Aliyekuwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Singida,
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) EX Peter Kakamba amefariki dunia
alfajiri ya tarehe 30/11/2016 katika hospital ya taifa Muhimbili alipokuwa
akipatiwa matibabu.
Kakamba alizaliwa mwaka 1963 katika kijiji cha
Kawajense Wilayani Mpanda, mkoa wa Katavi. Alisoma shule ya msingi Shanwe
Kawajense mwaka 1973 hadi 1980, Kidato cha kwanza hadi cha nne katika
shule ya Sekondari Kantalamba mwaka 1981 hadi 1984 ambapo kidato cha tano na
sita alisoma katika shule ya Sekondari Umbwe mkoani Kilimanjaro mwaka 1985 hadi
1987. Mwaka 1992 hadi 1994 alisoma Astashahada ya Sheria katika Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam.
Marehemu alijiunga na Jeshi la Polisi mwaka 1988
ambapo katika utumishi wake alipandishwa vyeo mbalimbali ikiwemo Konstable wa
Polisi (1989), Sagenti wa Polisi (1991), Mkaguzi Msaidizi wa Polisi (1997),
Mkaguzi wa Polisi (2003), Mrakibu Msaidizi wa Polisi (2006), Mrakibu wa Polisi
(2008), Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (2011), Kamishna Msaidizi wa Polisi (2015)
na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (2016).
Baadhi ya nafasi alizowahi kushika ni pamoja na
kuwa Mwendesha Mashtaka wa Polisi katika mkoa wa Iringa, Mkuu wa Polisi
wa Wilaya ya Mufindi, Afisa mnadhimu wa Polisi katika Mikoa ya Iringa na Geita,
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa na mpaka anafariki alikuwa Kamanda wa Polisi
katika mkoa wa Singida.
Kufuatia kifo hicho Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini
IGP Ernest Mangu anatoa pole kwa Maofisa, Wakaguzi,Askari, ndugu, jamaa na
marafiki kwa Msiba huo.
Bwana alitoa na Bwana ametwaa,
Jina la Bwana lihimidiwe - Amen.
Imetolewa na:
Advera John Bulimba - ACP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.
Makao Makuu ya Polisi.