MCHUNGAJI ANTONY LUSEKELO AANZA KUJARIBIWA,SOMA HAPO KUJUA
Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Maombezi (GRC)
la Dar es Salaam, Anthony Lusekelo, maarufu Mzee wa Upako, amekamatwa na polisi
akituhumiwa kumfanyia fujo na kutishia kumuua jirani yake.
Tukio hilo lilitokea juzi maeneo ya Kawe wilayani Kinondoni,
Dar es Salaam, kuanzia saa 11 asubuhi hadi saa tatu alipochukuliwa na polisi wa
Kituo cha Kawe.
Wakati wa tukio hilo, Mchungaji Lusekelo alikuwa
ameegesha gari lake barabarani kiasi cha kusababisha usumbufu na foleni ya
magari mengine.
Chanzo cha tukio hilo kinadaiwa ni kulipiza kisasi
kwa jirani zake hao wanaoishi katika nyumba namba KAW/MZN/1348, ambao alidai
wamekuwa wakimkebehi kuwa hafai kuwa mchungaji kwa sababu ya ulevi.
Licha ya baadhi ya watu kumsihi aondoke eneo hilo
kutokana na hadhi yake, mchungaji huyo alikaidi, huku akiendelea kuongea kwa
sauti iliyofanana na mtu mwenye kilevi.
Baadhi ya maneno yaliyosikika kwenye video
iliyorekodiwa eneo la tukio hayaandikiki kwa kuwa si ya kawaida.
“Mjinga wewe, mimi ni zaidi ya askari na
wewe ni mgambo, na si mgambo wewe ni raia tu.
“Umenitukana sana wewe mpaka leo
nimeamua kuloana na mvua, usitoe gari hapo mshenzi sana wewe, na nikikuona
mahali popote…, mshenzi kabisa, muangalie sana huyo,”
alisikika Mchungaji Lusekelo akiongea kwa sauti.
Baada ya kuongea maneno hayo, ilisikika sauti ya
mwanamke kutoka ndani ya uzio wa nyumba hiyo ikimjibu mchungaji huyo:
“Huwezi, aniangalie kitu gani.”
Hata hivyo, hata watu mbalimbali walipomsihi aache
kutoa lugha hizo za kejeli na aondoe gari lake lililokuwa limesababisha foleni,
alikataa akisema hataliondoa hadi atakapokuja Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu
ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro.
Baada ya purukushani hizo, polisi kutoka katika
Kituo cha Kawe walifika eneo hilo saa tatu asubuhi, wakamchukua mchungaji huyo
na kumpeleka kituoni.
Inadaiwa baada ya kufikishwa kituoni hapo, mchungaji
huyo alipimwa kiwango cha ulevi na kukutwa 131, ambacho kinaelezwa kuwa ni
kikubwa – ulevi wa kupindukia.
Ilipofika saa tano asubuhi, mchungaji huyo alihamishiwa
Kituo Kikuu cha Polisi (Central), ambako huko nako inadaiwa alipimwa kilevi na
kuonekana kushuka hadi kufikia 121.
Alipotafutwa Kamishna Sirro ili kuzungumzia sakata
la mchungaji huyo, alisema atalizungumzia leo katika mkutano wake na waandishi
wa habari.