MBUNGE SELUKAMBA AANZA KUCHUKIZA WAHARIRI,SASA WAMSIHII RAIS MAGUFULI,SOMA HAPO KUJUA
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limemwomba Rais
John Magufuli kumshughulikia Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Huduma na
Maendeleo ya Jamii, Peter Serukamba kwa maelezo kuwa ni ‘jipu’ ambalo
limevuruga mjadala wa Muswada wa Huduma za Habari.
Hayo yalibainishwa jana Dar es Salaam wakati
wahariri wa vyombo vya habari walipokuwa wakijadili vipengele vya Muswada huo
ambavyo vinatakiwa kufanyiwa mabadiliko kabla ya kupitishwa kuwa sheria kwa
kuwa si rafiki kwa tasnia ya habari nchini.
Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari
Limited, Absalom Kibanda alisema Serukamba ni ‘jipu’ na kumwomba Rais aamini
hivyo, akibainisha kwamba kipindi cha aliyekuwa Waziri wa Habari, Fenella
Mukangara walipeleka hati ya dharura kutaka Muswada huo ujadiliwe vizuri,
lakini alikataa huku akiunga mkono kama ulivyo.
“Kuna sauti ilisikika ikitembea katika
mitandao, nikajiuliza ameongea kama Waziri, Ofisa Habari wa Serikali au mtu
binafsi?” Alihoji Kibanda.
Kibanda alimwomba Rais aangalie ni nani wasemao
ukweli kati ya wadau wa habari (wahariri na waandishiwa habari) na mamlaka
nyingine za Serikali kuhusu namna nzuri ambayo Muswada huo unaweza kujadiliwa
na kuwa sheria kwa maslahi ya Taifa bila kukwaza upande.
Aidha, alibainisha kuwa kuna watendaji wa Serikali
ambao wamekuwa wakimsukuma Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, ili
aridhie mahitaji yao kwa maslahi binafsi.
Alisema kwa sasa waandishi wa habari wanafananishwa
na wahalifu na kusema hivi karibuni walichapisha habari kwenye gazeti lao na
walikuja kuomba radhi baada ya kupokea vitisho.
Aliongeza kuwa Muswada huo ulitakiwa uwekwe
vipengele vinavyowachukulia hatua watu wanaoingilia kazi za vyombo vya habari,
kwa kuwa makosa mengi vinayotupiwa vyombo vya habari vyanzo huwa ni wanasiasa.
Mjumbe wa TEF, Jesse Kwayu alisema wana wasiwasi na
msimamo wa Serukamba, kwa kuwa anashindwa kutimiza majukumu yake ya kuisimamia
Serikali na badala yake anakuwa kama ni ofisa wa Serikali.
“Wakati akiusoma Muswada huu kwenye
Kamati, akihitimisha alisema hakuna uhuru usio na mipaka,”
alisema Kwayu.
Alibainisha kuwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo
aliyepita, alisikiliza vizuri mapendekezo ya wadau wa habari na kuyafikisha
bungeni yajadiliwe tofauti na wa sasa ambaye si msikivu.
Alisema wakati wakiujadili hivi karibuni Dodoma
ilifika mahali kukawa na mvutano mkali kati ya Serukamba na Zitto Kabwe kwa
kuwa alikuwa hajaridhishwa na namna Muswada huo ulivyojadiliwa, kwa sababu
wadau wa habari wahusika hawajahusishwa kikamilifu.
Alisema asilimia 80 ya waandishi wa habari wako
mikoani ambako waandishi hao pia hawajajadili na kupata mwafaka wa Muswada huo.
Naibu Mhariri Mtendaji wa Jamhuri, Manyerere Jackton
aliwataka Serukamba na Mkurugenzi wa Idara ya Habari, MAELEZO, Hassan Abbas
wasijisahau na kupitisha Muswada huo eti kwa kuwa wako serikalini, bali wajue
kuwa kuna wakati watarudi na kukabiliwa na sheria hiyo.
Mwenyekiti wa TEF, Theophil Makunga alisema Muswada
huo usipobadilishwa vipengele hivyo na ukapitishwa kuwa sheria, waandishi wa
habari watakuwa kwenye shida kubwa kwa kuwa watakuwa wakipambana na kitu kibaya
sana