MAALIM SEIF ACHARUKA SASA,KUANZA ZIARA YA KUFAGIA ALIPOPITA LIPUMBA ,SOMA HAPO KUJUA
Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif
Sharif Hamad anatarajiwa kuzuru mikoa ya Kusini mwa Tanzania katika kipindi
ambacho bado kuna sintofahamu kuhusu nafasi ya Uenyekiti wa chama hicho.
Mwanasiasa huyo ambaye ataongozana na Mwenyekiti wa
Kamati ya Uongozi ya chama hicho, Julius Mtatiro pamoja na Wajumbe wa Baraza
Kuu watazuru Mtwara na Lindi ikiwa ni miezi michache baada ya Mwenyekiti wa
chama hicho anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama Vya Siasa, Profesa
Ibrahim Lipumba kuzuru eneo hilo la kusini.
Akizungumzia ziara hiyo, Naibu Mkurugenzi wa Habari,
Uenezi na Uhusiano wa Umma wa chama hicho, Mbarala Maharagande alisema kuwa
lengo la ziara hiyo ni kukagua shughuli za chama na kupokea maoni ya pamoja ya
namna ya kuboresha utendaji wa chama hicho kwa ngazi za chini.
Maalim Seif anatua katika eneo hilo wakati ambapo
kukiwa na mvutano baada ya baraza la madiwani kufanya jaribio lililoshindikana
la kumng’oa Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani, Geofrey
Mwanchisye.
Jaribio hilo liligonga mwamba baada ya Mwanasheria
wa Halmashauri hiyo, Sifaeli Kulanga kueleza kuwa hoja zao hazina msingi kwani
tuhuma zao kuhusika na matumizi mabaya ya fedha za umma yanakinzana na ripoti
ya kamati maalum iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara.
Kesi kuhusu Uenyekiti wa chama hicho inaendelea
Mahakamani ambapo Baraza Kuu la chama hicho linapinga barua ya Msajili
inayomtambua Lipumba kama Mwenyekiti wa chama hicho wakati ambapo Baraza hilo
lilikuwa limetangaza kumfuta uanachama.