KUMFANANISHA IMAAM HUSSEIN NA NABII ISA" YAANI YESU" NI UPOTOSHAJI ULIOVUKA MIPAKA...

Na Mwandishi wetu,
Katika kuendeleza upotovu wao, Mashia
wamemfananisha mjukuu wa Hussein na Nabii Isa, na kwamba eti Nabii Isa aliuawa
akipigania haki, mambo ambayo si ya kweli na yanapingana Qur’an na Sunna za
Mtume.
Kauli hizo za upotofu za Mashia
zilisikika Jumapili iliyopita katika kituo cha Mashia cha Ghadir kilichopo
Kigogo jijini Dares Salaam, ambako kulifanyika semina yenye anuani ‘Jitihada za Imam Hussein na Masihi Yesu
katika kusimamisha haki na amani ya dunia”. Katika hotuba yake, Sheikh wa dini
hiyo ya Mashia, Hemed Jalala alidai kuwa amani, mapenzi, huruma, utulivu na
maelewano baina ya wanajamii vitatokana na kuyasoma maisha ya Nabii Issa (amani
ya Allah iwe juu yake) sanjari na kufanyia kazi harakati za utumishi wa Walii
wa Mwenyezi Mungu (Imam Hussein) kama mrithi wa kiti cha Utume wa Muhammad
(rehema na amani ya Allah iwe juu yake).
Alisema malengo ya Nabii Issa yalikuwa ni
kuleta mabadiliko kwenye jamii yake kama ilivyokuwa kwa Imamu Hussein (Allah
amridhie) ambaye katika kipindi chote cha maisha yake alihakikisha haki na
amani vinatawala katika mji wa Karbala (Iraq).
Katika hali ya kushangaza kiongozi
huyo wa jamii ya Mashia alidai Waislamu, Mayahudi na Wakristo ni ndugu, na
ndiyo maana ndani ya Qur’an kuna sura mbalimbali zinazoonesha mahusiano ya
karibu kati ya watu wa dini hizo. Alizitaja sura hizo kuwa ni Maryam –yaani-
sura ya Mariam Mtakatifu ambayo Wakristo huitambua kama sura ya Bikira Maria,
pamoja na Surati Ruum yaani sura ya Roma. Kwa ajili hiyo, akawataka wasomi na
jamii ya Watanzania kuwa macho na maadui wasioutambua Uislamu ambao moja ya
harakati zao ni kutaka kuiaminisha jamii kuwa, Waislamu na Wakristo ni watu
waliotofautiana sana.
Sheikh Jalala aliwaambia wajumbe wa
semina hiyo kuwa, dini za Uislamu, Ukristo na Uyahudi kwa pamoja zimekuja na
misingi mitatu ambayo ni kumuabudu Mungu mmoja, kumuamini mjumbe aliyetumwa na
Mungu, na kuamini siku ya mwisho.
Kuhusiana na itikadi ya Wakristo katika
kuamini utatu, Mtakatifu Sheikh Jalala alisema, hilo ni suala la tofauti za
kifalsafa na mitazamo katika madhehebu, lakini ukweli ni kuwa kinachotoka
katika vinywa vyao ni neno la Mungu mmoja. “Waislamu na Wakristo ni ndugu, na
Nabii Issa (amani ya Allah ziwe juu
yake), Hussein bin Ali (amani ya Allah iwe juu yake), pamoja na Mtume (Rehema
na amani ya Allah zimfikie) wote ukijaribu kuwasoma utagundua kuwa
walichokilingania ni kitu kimoja, lakini pia hata lugha yao ni moja”
alibainisha.
Katika hali ya kushangaza, pamoja na maneno
yake hayo, bado alinukuu aya za Mwenyezi Mungu zinazosema: “Huyo ndiye Isa
mwana wa Maryamu, hiyo ndiyo kauli ya haki ambayo wanaifanyia shaka. Haiwi kwa Mwenyezi
Mungu kuwa na mwana, Subhanahu, Yeye ametakasika! Anapolihukumia jambo basi
huliambia tu: kuwa! Likawa” (Qur’an, 19:34-35). Ukitafakari juu ya maneno ya
Jalala, utaona ni juhudi za Mashia kutaka kujikurubisha kwa wasio Waislamu
kitaqiya hata kwa kuziuza aya za Allah Ta’ala kwa thamani ndogo ya kidunia.
Allah Ta’ala anasema kuwaambia wana
wa Israeli: “Na wala msiivike haki batili na mkaificha haki na huku mnajua”
(Qur’an 2: 42 ). Jalala amefanya talbisi nyingi katika hotuba yake hiyo. Kwanza
amemlinganisha Hussein bin Ali (Allah amridhie) na Manabii wawili wa Allah
katika wale Mitume wakuu watano waitwao ‘Ulu al‘azmi” yaani Nabii Nuhu, Nabii
Ibrahim, Nabii Musa, Nabii Isa na Nabii
Muhammad (amani za Allah ziwe juu yao). Hilo ni kosa kiitikadi kwa sababu
mjukuu wa Mtume Hussein bin Ali (Allah amridhie) alikuwa mwanadamu wa kawaida
tu na wala si Mtume wala Nabii.
Pamoja na juhudi yake kupinga na kuondoa
dhulma iliyozuka zama za fitna, Hussein bin Ali katu hawezi kulinganishwa na
Manabii hao wawili wa Allah. Halafu Jalala akasema: “…Nabii Isa na Hussein wote
wawili waliuawa wakipigania haki na kupinga dhulma”. Kudai kwamba Nabii Isa
aliuawa hiyo ni imani ya Wakristo na Wayahudi.
Ama Waislamu wa Ahlus Sunnah imani
yetu kuhusu Isa ni hii. “Na walisema hakika sisi tumemuuwa Isa mwana wa Maryam
mtume wa Allah, na wala hawakumuua na wala hawakumsulubu lakini
walishabihishiwa (hivyo), na hakika wale waliotofautiana kuhusu yeye (Isa) wako
katika shaka juu yake, hawana elimu juu ya hilo isipokuwa kufuata dhana, na
wala hawakumuuwa kwa yakini” (Qur’an, 4:137).
Sasa Jalala anaposema Nabii Isa
(amani ya Allah iwe juu yake) na Imam Hussein waliuawa wakipigania haki, kama
lipo katika itikadi za Shia au alikuwa anafanya taqiya ni vema akabainisha na
kama alikuwa anawafurahisha Wakristo basi ajuwe amemuudhi Allah Taa’la. Lakini
hatushangai sana kwani hiyo ndiyo itikadi ya Mashia juu ya maimamu wao kwamba
nao wanapokea wahyi kama manabii na hata kudai maimamu wao ni bora kuliko hata
manabii! Astaghfirullah.
Wakati Jalala akitangaza kwamba
Mashia ni kitu na ndugu moja na Mayahudi na Wakristo, Mashia hao hao wanajiona
ni tofauti na Masunni lakini kwa Mayahudi na Wakristo wao ni kitu kimoja. Sisi
tumeambiwa: “Hakika Waumini ni ndugu, basi patanisheni baina ya ndugu zenu, na
mcheni Mwenyezi Mungu ili mrehemewe”(Qur’an, 49:10) Aliyesema Wakristo ni
tofauti na Waislamu ni Allah Jalala anadai kwamba wanaoamini kuwa Wakristo na
Waislamu ni watu wanaotofautiana sana ni maadui na wasioutambua Uislamu.
Huku ni kupotosha ukweli kutoka kwa
Allah. Kuhusiana na itikadi ya Wakristo katika kuamini utatu Mtakatifu Sheikh
Jalala alisema, hilo ni suala la tofauti za kifalsafa na mitazamo katika
madhehebu, lakini ukweli ni kuwa kinachotoka katika vinywa vyao ni neno la
Mungu mmoja Allah anasema: “Hakika wamekufuru wale wasemao hakika Mungu ni Isa
mwana wa Maryamu …” (Qur’an, 5:72). Kisha Allah akasema: “Hakika wamekufuru
wale wasemao hakika Allah ni wa tatu katika utatu…” (5:73) Sasa vipi huyu Shia
kudai kwamba tofauti kati ya Uislamu na Ukrsito ni tofauti za kifalsafa na
mitazamo ya kimadhehebu tu? Aya hizi na nyingine nyingi hazioni?
Ina maana Ukristo, Uyahudi na Uislamu
ni madhehebu tu za dini moja? Kauli kama hizi ni kupingana wazi wazi na Allah
Ta’ala kwa malengo ya kuwafurahisha Wakristo waliohudhuria semina hiyo ambapo
kwa mujibu wa mmoja wa Maprofesa aliyekuweko siku hiyo, alidai sasa ameuelewa
Uislamu. Waislamu tujihadhari na upotoshaji wa aina hii kwani hawa hawana
tofauti na yule ‘Bwana’ aliyedai siku za hivi karibuni akiwa kanisani kwamba
huu ni wakati wa Injili na mkombozi wa ulimwengu ni Yesu.