CCM YASHIKA UCHAWI HUKU ZANZIBAR YAONYANA UMBEA KWENYE MITANDAO YA JAMII,SOMA HAPO KUJUA
Baadhi ya Viongozi na wanachama wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) Zanzibar wametakiwa kuacha tabia ya kutumia mitandao ya kijamii
kujadili masuala yanayohusu Chama badala yake watumie vikao halali
vinavyotambuliwa na Katiba ya Chama hicho.
Rai hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM
Zanzibar Vuai Ali Vuai wakati akifunga Mkutano wa Viongozi wa Halmashauri Kuu
ya CCM Mkoa wa Kusini Unguja Kichama uliofanyika katika Shule ya Msingi
Makunduchi Mkoani humo.
Alifafanua kwamba tabia hiyo ya kujadili,
kukosoa na kuwatuhumu baadhi ya viongozi wa ngazi mbali mbali wa Chama na Jumuiya
zake kupitia Mitandao ya kijamii ni utaratibu unaokwenda kinyume na miongozo ya
chama hicho.
Alisema Katiba ya CCM inaelekeza Kwamba mambo
yote yanayogusa maslahi mapana ya Chama yajadiliwe Katika Vikao halali
vinavyotambuliwa na kanuni za Chama, kwani jukwaa hilo ndiyo sehemu rasmi ya
kukosoana na kupeana maelekezo.
Vuai alisikitishwa na tabia hiyo na kueleza
kuwa njia pekee ya kumaliza Changamoto hiyo ni Wanachama na Viongozi
kujenga utamaduni wa Kusoma na kuelewa Kanuni, Katiba na miongozo mbali mbali
ya CCM ili kufahamu wajibu, majukumu, haki na maadili yanayoongoza Chama.
Alisema tabia hiyo imekuwa ikifanyika katika Magroup
ya Mitandao ya kijamii zikiwemo Facebook, WhatsApp na mitandao mingine, jambo
ambalo ni kosa kwa mujibu wa kanuni za Chama.
“ Wanachama, Viongozi na Watendaji naomba muelewe
kwamba hiki Chama kinaendeshwa kwa utaratibu maalum ulioelezwa Kikatiba ,
Kikanuni na miongozo mbali mbali, kwa nia ya kulinda hadhi na heshima
ya Chama chetu, na hakuna jambo lolote linaloshindikana kupatiwa ufumbuzi
kupitia utaratibu huo.
"Sasa panapojitokeza baadhi ya Watu miongozi
mwetu wakaanza kujadili na kuwakosoa wenzao nje ya mfumo huo basi hao
tunawahesabu kuwa wana nia ya kuanzisha Majungu, Fitna na mpasuko katika
taasisi yetu.”, alieleza Vuai na Kuongeza kuwa CCM ni Chama imara
na kinachoheshimu Demokrasia katika kujadili mambo yake na kuyatolea maamuzi
stahiki katika Vikao rasmi na sio vichochoroni au vibarazani.
Aliongeza kuwa sio kwamba kuna viongozi na wanachama
wanaogopa ama hawataki kukosolewa lakini lazima heshima na nidhamu iwepo
katika kutekeleza matakwa ya Demokrasia ndani ya Chama hicho kwa kuheshimu
utaratibu uliowekwa Kikatiba.
Akizungumzia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi
ya Chama hicho ya mwaka 2015/ 2020 katika Mkoa huo aliwapongeza Viongozi wa
Majimbo wakiwemo wabunge, wawakilishi na Madiwani huku akiwasisitiza Viongozi
wa Chama kuhakikisha wanakagua kikamilifu miradi inayotekelezwa na viongozi hao
ili kujiridhisha kama inawanufaisha wananchi wote.
Aliwataka viongozi wa Chama na Jumuiya zake kuwa wa
kwanza kutambua kero na changamoto za wananchi wa maeneo mbali mbali na
waziwasilishe kwa Wakuu wa Wilaya (DC) ili ziweze kupatiwa ufumbuzi wa
kudumu na Serikali.
“ Huu sio wakati wa kusubiri taarifa zinazohusu
Changamoto za Chama, Jumuiya na Serikali ziletwe Ofisini, badala yake mtoke na
kuzitafuta wenyewe ili kuwasaidia wanachama na wananchi kutatuliwa kero zao kwa
haraka kupitia Mamlaka husika.”, alisisitiza Vuai.
Alisema Viongozi wanatakiwa kufahamu kwamba suala la
kuwatumikia wananchi sio jambo la hiari bali ni lazima watekeleze kwa vitendo
ahadi walizotoa wakati wa kampeni kwani wasipotekeleza Wajibu wao vizuri kwa
jamii mwisho wa siku kitakacho hukumiwa ni Chama na sio kiongozi husika.
Aidha aliwakumbusha viongozi hao kwamba Chama na
Jumuiya zake wanatarajia kufanya Uchaguzi mwaka 2017, hivyo waanze mapema
kuwaelimisha, kuhamasisha na kuwaandaa kisaikolojia wanachama wa Chama hicho
juu ya matumizi sahihi ya kanuni za UChaguzi ili kuepuka lawama zisizokuwa za
lazima.
Alisema Wanachama wanatakiwa kuwachagua viongozi
wenye sifa na wasiokuwa na Mukhari( kuoneana haya) katika kusimamia mambo ya
msingi ya CCM na waumini wa kweli wa Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964,
Muungano wa Serikali mbili wenye vigezo hivyo ndio wanaofaa kuwa viongozi.
Hata hivyo aliwapongeza Rais wa Zanzibar, Dkt. Shein
na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Magufuli kwa juhudi na
kasi zao za kufanikisha mipango ya maendeleo ya nchi kwa ufanisi mkubwa hali
inayoongeza hamasa kwa jamii kuendelea kuwaamini.