ALIYEKUWA MBUNGE WA KASULU MJINI AKUBALI KUYALAMBA MATAPISHI YAKE,AKIKIMBIA CHAMA CHA ACT-WAZALENDO NA KUHAMIA CCM,SOMA HAPO KUJUA
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI NA WATANZANIA WOTE.
Kutoka
mezani kwangu Moses Joseph Machali, Tarehe: 21/11/2016
Napenda
kuutaarifu umma wa Watanzania kupitia kwenu waandishi wa habari kwamba ni jambo
la ajabu na aibu kwa watu makini na wenye kuhitaji mabadiliko ya kweli Kuacha
kuunga Mkono juhudi zinazofanywa na serikali ya awamu ya tano chini Uongozi wa
Rais Dr. John Pombe Joseph Magufuli bila kusahau utendaji makini wa Waziri Mkuu
wake Mhe. Majaliwa Kasim Majaliwa (Mb) pamoja na mawaziri mbalimbali wameonesha
kutaka kufuata mwenendo wa Rais Magufuli na Waziri Mkuu wake.
Mimi
Moses Joseph Machali niliyefanya sana siasa za Upinzani hapa nchini na
niliyepiga kelele na kupinga siasa za kifisadi zilizoitawala nchi hii;
niliyepinga pia ufisadi uliokuwa umeitawala serikali huko nyuma kwa nguvu na
uwezo wangu wote nikishirikiana na wapinzani wenzangu, ninaamua kujiunga na
watu wanaonesha dhamira safi ya kuiendeleza nchi yetu Tanzania. Watu wenye
mwelekeo na dhamira ya kuijenga nchi yetu kwa maendeleo enedelevu ni jamii ya
akina Magufuli, Kasim Majaliwa, nk.
Mwaka
mmoja wa Uongozi wa Rais Magufuli na baadhi ya wasaidizi wake kupitia hatua
mbalimbali zilizochukuliwa dhidi ya ufisadi uliokuwa umeigubika nchi yetu,
inatosha kabisa kwa mtu yeyote makini kufanya uamuzi wa kumuunga mkono au
kutokumuunga mkono Rais Magufuli.
Mimi
nimechagua kumuunga Mkono Rais kwa vitendo, kwa sababu ninaposoma Rekodi yangu
ya enzi nikiwa Mbunge (Hansard) na kabla ya kuwa mbunge ni kwamba nilipinga
mnoo wizi na ufisadi wa kila aina; Nilipinga Matumizi ya fedha serikalini
yasiyo ya lazima na yasiyo na tija kwa taifa (Rejeeni hotuba yangu ya Bajeti ya
Wizara ya Uchukuzi, nikiwa Waziri Kivuli wa wizara hiyo ya mwaka 2014/2015 na
2015/2016), vilevile bila kusahau hotuba zangu mbalimbali Bungeni na nje ya
Bunge.
Kwa
kushirikiana na wapinzania wenzangu enzi hizo tulishauri na kupinga ufisadi wa
kila aina, tuliitaka serikali kufanya mambo yenye tija kwa taifa na sasa kila
mwenye macho anaona hatua zinazochukuliwa na serikali ya awamu ya tano. Miradi
kama ya Ujenzi wa Reli, Ununuzi wa ndege mbili na mipango ya kununua ndege
zaidi kama namna ya kulifufua shirikia la ATCL ni mambo tuliyoyahitaji kuyaona
wapinzani; sasa yanafanyika. Wale wenye dhamira ya dhati ya kuona nchi yetu
ikipiga hatua, kamwe hatuwezi kubeza mambo hayo bali kuyaunga mkono.
Wale
tuliosema na kupiga kelele kwamba Serikali ni dhaifu ktk kuwachukulia hatua
watu mbalimbali wenye dhamana serikalini walioonekana kufanya vibaya serikalini
ktk nafasi zao, leo tunaona kumekuwepo na kasi nzuri ktk kuwachukulia hatua
watu hao. Hata hivyo leo hii upinzani umepiteza mwelekeo kwa sababu unapingana
na kile ulichokihubiri nchini.
Agenda
ya kupinga ufisadi siyo ya upinzani tena bali ya JPM na CCM yake au yao.
Wapinzani wamegeuka kuwa watu wanaokataa yale waliyoyasimamia na kuyahubiri
huko nyuma. Hakika huo siyo uungwana bali aina mpya ya ufisadi nchini na
usaliti kwa agenda zao.
Kama
kweli sisi tumeokuwa wapinzani na tulioonesha kupinga kwa nguvu zote ufisadi
ulioiumiza nchi hii tulimaanisha yale tuliyoyahubiri na kuwaaminisha watu basi
tunao wajibu wa kuacha tabia ya kuwa vigeugeu kwa mambo tuliyoyaamini na
kuyahubiri. Kutofanya hivyo basi ni mwendelezo wa ufisadi kwa maslahi binafsi.
Ni
nani asiyeona kwamba serikali ya awamu ya tano inafanyia kazi mambo mengi tuliyoyapigia
kelele? Au tunajifanya kutokukubali ukweli unaoishi kwa ule msingi wa upinzani
wa Tanzania kwamba Tukimuunga mkono Mtawala kamwe hatutapata kuaminiwa na
wapiga kura nchini na hivyo tupinge tu hata kama ni ukweli? Nadhani
kinachofanyika ni mwendelezo wa kupinga hata mazuri ili kutafuta fursa ya
wapinzani kukubalika kisiasa zaidi hata kwa njia na mbinu haramu kama kawaida
ya siasa zilizo zoeleka hapa nchini kwa miaka mingi.
Taifa
hili haliwezi kuendelea kwa kuwa na siasa za kutokukubaliana na ukweli
unaoishi. Kama dhamira ya kila mtanzania ikiwemo wapinzani ni kuona nchi ina
move basi hatuhitaji kuwa watu wa kupingapinga hata yaliyo mema bali kuyaunga
mkono yale yaliyo mema bila kujali yanafanywa na nani bali msingi mzuri
unapaswa kuwa ukweli kwa kila jambo.
Serikali
ya awamu ya tano imeonesha njia ktk mambo mengi na inastahili kuungwa mkono.
Safari ni hatua na ninaamini kwamba hata yale yanayoonekana kutokufanyiwa kazi
ndani ya mwaka mmoja uliopita na ambayo yalishindikana huko nyuma, bado yanaweza
kuja kufanyiwa kazi huko mbeleni. Serikali ya JPM imejitahidi sana
tukilinganisha na huko tuliko toka. Uongozi huu unafanana sana na ule wa akina
Hayati EDAWARD MORINGE SOKOINE chini ya hayati Baba wa Taifa Mwl Julius
Kambarage Nyerere.
Daima
ninaamini ktk yale ninayoyaamini pasipo kufungwa na ukada bali kuangalia ukweli
ni upi. Hata kelele wanazopiga baadhi ya watu kwamba maisha yamekuwa magumu kwa
sababu ya Magufuli ni propaganda tu kwa sababu hakuna uhusiano wa maisha magumu
na suala la KUDHIBITI wapiga dili wa fedha na mali za umma bali tukubali kwamba
wapiga dili waliozoea kupiga dili na kuziingiza fedha walizopiga ktk mzunguko
kwamba siyo jambo la msingi ktk kujenga uchumi imara.
Uchumi
imara hauwezi kujengwa kwa kuruhusu ubadhirifu wa fedha na mali za umma au hata
za mtu mmoja mmoja. Kinachoonekana hivi sasa ni kama nchi inasukwa upya na
hivyo tuwaunge mkono viongozi wa serikali ya awamu ya tano kwa mema
wanayoyafanya na kuwashauri kurekebisha ktk yale ambayo hayajakaa vizuri.
Tuachane na siasa nyepesi za kutaka kuona kwamba mazuri ni yale yanayofanywa na
wapinzani huku mambo hayohayo yakifanywa na CCM yaonekane hayafai na kutajwa
kuwa ni ya hovyo. CCM ya JPM siyo ile ya 2015 kurudi nyuma kidogo. Hii ni
tofauti na ninaiunga mkono.
Hivyo
basi leo Tarehe 21/11/2016 ninatangaza rasmi kwamba ninajiunga na timu JPM kwa
maslahi ya taifa kwa kuwa sioni sababu ya kupingana na yale niliyoyapigania na
itakuwa ni sawa na mtu kupigana na kivuli chake mwenyewe. Kwaherini Upinzani
nimeamua kuanza siasa mpya za masuala yale niliyoyaamini na ninayoyaamini.
Imani ni Matendo Na Matendo ni imani. Piga vita ufisadi kwa imani na Matendo.
Moses
Joseph Machali
X-mbunge,
Kasulu Mjini 2010-2015