WANAOJIFANYA KUMSHANGILIA PROFESA LIPUMBA,WAJIBU HOJA HIZI,SOMA HAPO KUJUA
WAPO wanaomshauri Profesa Ibrahim Lipumba ajiunge na
CCM (Chama Cha Mapinduzi), na sababu anayotajiwa kwa ushauri huo, inatajwa kuwa
ndiko atatumika ipasavyo. Sawa, inaweza kuwa ndiko atatumika au kutumiwa, anaandika Jabir Idrissa.
Mchambuzi mmoja anasema Prof.
Lipumba atatumika vizuri huko CCM kwa sababu tayari amewasaidia kwa “kuwafanyia
kazi nzuri ya kuhakikisha Edward Lowassa haupati urais ng’o.”
Ushauri huu siuamini na simtakii profesa huyu mahiri
wa uchumi ari na utashi wa kuamua kuingia chama hicho ambacho kadiri siku
ziendavyo, naona kinazidi kuthibitisha kinaishi kwa kuhitaji sana msaada wa
vyombo vya dola.
Kwanza sidhani kama ni kweli Prof. Lipumba alitumika
kumzuia Lowassa kupata urais wakati wa uchaguzi mkuu uliopita. Lowassa alifanya
kampeni nzuri kuliko mgombea mwingine yeyote wa wadhifa huo katika wale
walioingia kugombea.
Lowassa, waziri mkuu aliyeshika nafasi hiyo kipindi
kifupi zaidi katika jamhuri hii – Novemba 2005 hadi Februari 2007 –
alizichangamsha siasa za Tanzania zaidi kuliko mwanasiasa mwingine yeyote tangu
kipindi kile.
Na kwa ufundi wa timu ya kampeni iliyomsimamia,
ikiongozwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) chini ya mwamvuli wa
Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), alirudisha heshima yake kisiasa na
kimtizamo.
Heshima ya Lowassa anayeichagiza CCM hata viongozi
wake kukosa usingizi kikawaida, ilikuwa imefifia kutokana na tuhuma nzito za
kuwa fisadi miongoni mwa makada wa CCM waliotajwa na chama hicho kama magamba.
Ukweli huo ulimpaisha akaeleweka zaidi alivyo
kiuongozi, bali pia alivyo na mahaba makubwa kwa nchi na watu wake. Hizo zikawa
hazina zilizomhakikishia uungwaji mkono na hatimaye milioni nyingi za kura.
Walipoona wingi wa kura zake, wasimamizi wa ulinzi
na usalama waliokuwa katika hekaheka zisizo mfano, wakapata kiwewe. Kwa
shinikizo nzito, wakalazimika kutumia ufundi waliofunzwa kubadilisha mazingira
walimokuwa. Hawakujali kuumiza vijana na kutunga uongo katika kudhibiti hali,
ilimradi waridhishe wakubwa zao.
Vitendo vilivyofanyika hadharani, ikiwemo kuvamia
ofisi ya kupokelea matokeo ya kura za urais za mgombea wa UKAWA, vilisaidia
kufungua zaidi macho ya wafuatiliaji siasa na wakajua ni upi utakuwa mwisho wa
Lowassa katika matumaini yake ya kuunyaka uongozi wa taifa, chini ya kaulimbiu aliyoichagua
ya “Lowassa mabadiliko, mabadiliko Lowassa.”
Mimi naona Prof. Lipumba analazimika kwanza kukubali
ukweli kuwa kwa alipofikia sasa, maji ya shingoni kwake kubakia CUF. Namuonea
huruma maana amejenga hofu moyoni mwake pamoja na kujitia ujasiri wa
kung’ang’ania jengo la Ofisi Kuu ya CUF Buguruni.
Msukosuko aliojipa kwa sababu anazozijua, umemgeuka
kuwa msomi aliyejichafua kwa kiwango cha kutisha mbele ya umma wa CUF na
Watanzania.
Anavyoshikilia kuwa angali mwenyekiti, tena halali,
ndivyo anavyoongeza kasi ya kujipotezea heshima kidogo aliyobaki nayo.
Kwa hakika profesa wa uchumi amegeuka mbumbumbu.
Angeangalia sababu zinazosukuma wachora katuni kumfikiria kila wakati. Ona
anavyochorwa karikacha hii na ile zikimuelezea kwa namna za ovyo.
Mchoraji mmoja katika gazeti la Kingereza Ijumaa
iliyopita, alimchora aliyeonekana ni profesa akiwa amevaa shuka au seruni au
taulo au kaptura; tumbo wazi, kinywani ameshika msuaki na mikononi (wa kushoto)
ameshika kopo na (kulia) ndoo.
Karikacha inamuonesha mtu amevaa ndara miguuni na
miwani ipo vizuri inapovaliwa. Mkato wa nywele ni wa ujana; sijui ni panki au
wanaitaje wenyewe. Mtu yupo chumbani, hapana, ni ofisini ambako amekugeuza
chumba cha kulala. Vipi, amefukuzwa na mama?
Alama za chumba zinazoonekana ni godoro ambalo ni
kama limewekwa sakafuni huku likiwa limebeba mto. Juu ya meza inaonekana
kompyuta, simu ya mezani, karatasi chache, kikombe na bendera yenye nembo ya
CUF.
Mtu anaonekana kama vile anachapa kazi kwelikweli
kwa kuwa kikapu cha kutupia taka ofisini, kimejaa uchafu hadi karatasi nyingine
kukutwa chini zimeanguka.
Yu kwenye chumba ambacho mlango wake umefungwa kwa
ndani; lakini umesheheni vitasa na kuwekewa chuma maalum cha kuuzuia kufunguliwa
kwa ndani. Profesa amejifungia!
Kwa hivyo, leo anashuhudiwa profesa aliyekuwa tishio
kwa utawala, amejifungia katika chumba kilicho varuvaru. Katika uhalisia,
inaonekana tangu aliposimamishwa uanachama na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa
(BKUT) la chama hicho Agosti 28 mjini Zanzibar, ameamua kuhama kwa muda
nyumbani kwake, na kuhamia Buguruni.
Sasa huyu ndo Profesa Lipumba wa leo. Akiwa hapo, na
kikundi kinachozidi kupungua, anatamba akisimamia msimamo wa kisanii wa Msajili
wa Vyama vya Siasa Tanzania, Jaji Francis Mutungi, kumthibitisha ndiye
kiongozi.
Jaji Mutungi ambaye analalamikiwa na wajuzi wa
sheria na wakuu wa upinzani, alifanya hivyo baada ya kufanya uchambuzi wa
malalamiko yake na taarifa zilizo zilizowasilishwa na uongozi wa CUF, usiomtambua
baada ya kumsimamisha.
Lakini pia jaji amesahau kuwa bado tovutini mwa
msajili hadi juzi tu akitambulika Wakili Twaha Taslima kuwa kiongozi halali
baada ya Prof. Lipumba kujiuzulu mwenyewe kwa barua ya 5 Agosti 2015. Wakili
Taslima aliteuliwa baadaye kuongoza kamati ya muda ya kufanya kazi ya
mwenyekiti na makamu wake.
Hatua inayosomeka kwamba profesa amevuliwa uanachama
ilikuja kwa kikao cha dharura cha Baraza Kuu la Uongozi cha 27 Septemba 2016,
baada ya kutofika kujitetea dhidi ya tuhuma kuwa amedharau wito wa kufika mbele
kujieleza ni kwa nini asichukuliwe hatua za kinidhamu kufuatia shitaka la
kuongoza na kusimamia kikundi cha wahuni kuvamia Ofisi Kuu ya chama iliopo
Buguruni, jijini Dar es Salaam tarehe 24 Septemba, 2016.
Ushauri mzuri kwa Profesa angechagua njia ya
mahakama kuitafuta haki. Kule angesikilizwa anachokiamini, kikapimwa na
ukasikilizwa utetezi wa CUF, na akasubiri hatima yake. Ameamua kuamini serikali
ileile iliyofurahia kuvunjwa kwake mkono 2005 na kubebwa juujuu na vijana
Januari 2015 Mtoni kwa Azizi Ali.
Namsema Prof. Lipumba kwa sababu fujo zake naziona
kama zinavyoonekana na wengi zimelenga kudhoofisha nguvu za CUF kupigania haki
ya Wazanzibari walioichagua 25 Oktoba 2015 Zanzibar.
Isitoshe, kujenga kwake uswahiba na walewale waliomdhalilisha
huko nyuma alipokuwa imara kitini, kunaazimia kuangamiza harakati za mabadiliko
nchi nzima. Natabiri atashindwa baada ya muda si mrefu, lakini kuua nguvu ya
upinzani ndio mwelekeo wa kampeni yake iliyojaa dalili za kufadhiliwa na
watawala.