SIKIKI YAJIBU SERIKALI YA MAGUFULI,YASEMA IMEJAA SIASA ,SOMA HAPO KUJUA

Wiki iliyopita Sikika ilikutana na vyombo vya habari
kujadili uhaba wa dawa unaoikabili Bohari Kuu ya Dawa (MSD). Vyombo vya habari
kwa nyakati tofauti vilitoa taarifa sahihi kuhusu tatizo hili.
Hata hivyo, majibu kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Bohari Kuu ya Dawa hayakuonesha kutoa kipaumbele kwa tatizo hili. Kwa kuwa taarifa za uhaba wa dawa zilipatikana kutoka kwenye tovuti ya Bohari Kuu ya Dawa, tulitegemea majibu yenye ukweli,weledi na kuonesha ukubwa wa tatizo kutoka kwa wahusika. Taarifa hizo zingesaidia Ofisi ya Rais kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kuona uharaka na umuhimu wa kutatua tatizo hili ili kuwasaidia wananchi kwa wakati. Badala yake majibu ya Wizara na Bohari Kuu yalipoteza msingi wa tatizo kama ifuatavyo;
(i) Vyombo vya habari vilitumia takwimu
kutoka katika tovuti rasmi ya Bohari Kuu ya Dawa kwamba kuna upungufu wa
asilimia 47 ya aina mbalimbali za dawa zilizotakiwa kuwepo kwenye orodha ya
dawa MSD. Tarehe 27 Septemba 2016, Wizara ya Afya ilikanusha kwa kudai kwamba
aina ya dawa zilizokuwepo ni asilimia 53. Hata hivyo, mtu akisema uhaba ni
asilimia 47 ya aina ya dawa na mwingine akasema uwepo ni asilimia 53 wote
wanamaanisha kitu kile kile.
(ii) Taarifa za vyombo vya habari zilionesha
uhaba wa baadhi ya dawa muhimu ambazo zilitarajiwa kupatikana MSD muda wote
Taarifa hizi zilikusudia kuonesha mifano ya kiwango cha ukubwa wa upungufu wa
dawa. Badala ya kujibu hoja ya msingi, yaani upungufu wa dawa nchini kwa
ujumla; Wizara iliamua kujikita kwenye kutaja uwepo wa baadhi ya dawa kama
vidonge vyaparacetamol na zingine chache.
(iii) Bohari Kuu ya Dawa ilinukuliwa na vyombo
vya habari ikikanusha uwepo wa upungufu wa dawa na kusema kwamba serikali
imefanya maajabu kwa kuipatia MSD jumla ya Shilingi bilioni 20 kwa robo ya
2016/2017. Hata hivyo, bilioni 20 ni pungufu ya kiwango halisi ambacho
kingehitajika (Shilingi bilioni 62.5), kwa robo ya kwanza ya mwaka iwapo bajeti
iliyotengwa ya shilingi bilioni 251 ingegawanya sawa na kutolewa katika awamu
nne. Je, Bohari Kuu ya Dawa inaposema serikali imefanya maajabu ina maana
haihitaji fedha zaidi kwa ajili ya kutatua tatizo la dawa nchini?
(iv) Wizara ya Afya imeahidi
kuongeza akiba ya baadhi ya dawa kuanzia mwezi Oktoba, 2016. Hii ni sawa na
kukiri kwamba kulikuwa na upungufu wa dawa. Ingawa tunaipongeza wizara kwa
hili, Wizara haikueleza ni lini itapata fedha zilizobaki na iwapo ongezeko hilo
la dawa litakidhi mahitaji halisi.
Katika kufafanua suala hili, Sikika ingependa
kuelezea umma na wadau wa sekta ya afya ukweli kuhusu upungufu huu sugu wa dawa
na vifaatiba kwenye Bohari Kuu ya Dawa na katika vituo vya kutolea huduma za
afya:
(i) Uhaba
wa dawa na vifaa tiba katika Bohari Kuu ya Dawa siyo tatizo jipya, bali ni la
muda mrefu, ambalo serikali yenyewe imekuwa ikikiri kupitia taarifa zake mbali
mbali. Isipokuwa sasa limefikia kiwango kikubwa, hata kupelekea uhaba wa dawa
kama za chanjo kwa kipindi cha zaidi ya miezi mitatu.
(ii) Kila
mwaka, Wizara ya Afya wamekuwa wakiahidi Bungeni kutatua upungufu na uhaba wa
dawa muhimu na vifaatiba. Pia Wizara ya Afya imekuwa ikiahidi bungeni kila
mwaka kulipa deni inalodaiwa na MSD ili kuboresha ufanisi wa bohari. Hata hivyo
uhaba wa dawa umeendelea kuwepo na deni la MSD limekuwa likikua kila mwaka.
(iii) Uhaba ukitokea MSD moja kwa moja
unaathiri upatikanaji wa dawa muhimu na vifaa tiba katika vituo vya kutolea
huduma za afya vya umma, kwa sababu mfumo wa sasa unalazimisha vituo kuagiza
dawa kutoka MSD kwanza kabla ya kuruhusiwa kununua mahali pengine. Pamoja na
hilo, mgao wa fedha za dawa kwa vituo hivyo hupelekwa moja kwa moja MSD ambapo
vituo haviwezi kuzichukua kuagiza dawa pengine pale wanapokosa dawa MSD.
(iv) Mnamo Septemba 16, 2016, tovuti ya MSD
ilionesha ukosefu wa asilimia 47 wa aina mbali mbali za dawa. Miongoni mwa dawa
na vifaatiba vilivyokosekana ni vile vinavyotumika katika matibabu muhimu ya
kupunguza vifo, mfano dawa za kuharisha kwa watoto (ORS+Zinc), vifaa vya
kujifungulia (Delivery kits), dawa za maumivu, dawa za magonjwa ya moyo na chanjo
kama vile za surua, homa ya manjano na kichaa cha mbwa.
(v) Mojawapo ya sababu za uhaba huu ni
serikali kushindwa kutenga na kutoa fedha za kutosha kukidhi mahitaji ya nchi
ya dawa muhimu na vifaatiba. Kwa mfano, mahitaji ya sasa ya dawa na vifaatiba
ni zaidi ya shilingi bilioni 577 lakini bajeti iliyotengwa kwa mwaka huu
ni shilingi bilioni 251, ambapo kati ya hizo, shilingi bilioni 108 ni zakulipa
deni la MSD.
(vi) Vituo vya afya vya umma vinapata
usumbufu mkubwa kutokana na utaratibu unaovilazimisha kutuma maombi ya dawa MSD
licha ya kufahamu ukweli kwamba hazipo. Baada ya vituo kupata uthibitisho wa
maandishi wa kutokuwepo dawa MSD, ndipo vinaruhusiwa kufanya taratibu zingine.
Pamoja na usumbufu huu, baadhi ya vituo vimemudu kukabiliana na uhaba wa dawa
kwa kutumia vyanzo mbadala vya fedha kununua dawa kutoka kwa wauzaji binafsi.
Mfano halisi ni katika vituo vya afya vya wilaya za Kondoa na Kilolo
ambapo Sikika ilifuatilia kwa kina.
Kutokana na uzoefu wa Sikika wa kufanya
kazi katika sekta ya afya kwa takribani miaka kumi, tunashauri mapendekezo
yafuatayo yafanyiwe kazi:
(i) Bohari Kuu ya Dawa iachwe iwe taasisi
au kampuni huru itakayofanya maamuzi yake yenyewe na kukusanya mtaji kushindana
na wauzaji wengine binafsi wa dawa nchini.
(ii) Serikali ifute ulazima wa vituo vya
kutolea huduma za afya vya umma kuagiza dawa MSD kwanza, badala yake viachwe
huru kuamua kununua kutoka kwa muuzaji yeyote mwenye dawa ambaye anadhibitiwa
na kuhakikiwa na serikali.
(iii) Serikali ihakikishe kuwa fedha
zinazotengwa kwa ajili ya dawa muhimu na vifaatiba zinapelekwa moja kwa moja
kwenye akaunti za vituo au Halmashauri badala ya utaratibu wa sasa ambapo
zinapelekwa kwenye akaunti za vituo zilizopo MSD.
(iv) TAMISEMI iimarishe na kusimamia uwezo wa
vituo vya kutolea huduma za afya katika halmashauri ili kujiendesha vyenyewe,
na Wizara ya Afya ijikite katika kusimamia ubora na udhibiti wa bei za dawa.
(v) Tunaomba watendaji na viongozi katika
sekta ya Afya wafanye kazi kitaalam zaidi badala ya kisiasa.
(vi) Mwisho, wakati Wizara ya Afya ikifanyia
kazi mapendekezo haya. tunaiomba Ofisi ya Rais kuagiza fedha zitolewe kama
mpango wa dharura kutatua tatizo lililopo la dawa, ikiwa ni pamoja na kulipa
deni lote la MSD.