SERIKALI YA MAGUFULI YAANZA "KUANGUKA"SASA YAJAA MIGOGORO KILA KONA,SOMA HAPO KUJUA
SERIKALI ya Rais John Magufuli inayumba kutokana na
watendaji wake kujigawa makundi makundi,anaandika Moses Mseti.
Wakati Jijini Dar es Salaam
kukiwa na sintofahamu kutokana na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia
uchaguzi wa Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Jijini Mwanza hamasa ya wenyeviti wa
serikali za mitaa kuyumbisha shughuli za maendeleo zinazidi kuongezeka.
Tayari Mbunge wa Nyamagana jijini humo ameungana na
dhamira ya wenyeviti hao kutangaza kutoshirikiana na Kiomoni Kibamba,
Mkurugenzi wa Jiji hilo katika shughuli za maendeleo.
Tarehe 22 Oktoba mwaka huu, wenyeviti 172 wa wilaya
hiyo walisusia kikao cha ulinzi na usalama kilichoitishwa na Marry Tesha, Mkuu
wa Wilaya hiyo baada Kibamba kuwataka wenyeviti kukabidhi mihuri kwake.
Wenyeviti hao wakiongozwa na Keffa Otieno, Makamu
Mwenyekiti, walitangaza kwamba kuanzia tarehe 22 Oktoba mwaka huu, wenyeviti
wote hawatashiriki katika shughuli zozote za maendeleo hadi mkurugenzi huyo
atengue kauli yake.
Akizungumza na wenyeviti hao jana Mabula amesema
kuwa, hayupo tayari kuona mamlaka ya wenyeviti hao yakiporwa na kwamba,
atashirikiana kila hatua.
Mabula amesema kuwa, endapo wenyeviti hao
watanyang’anywa mihuri inayowatambulisha kama wasaidizi wa Serikali Kuu ngazi
za mitaa, wenyeviti hao hawatakuwa na kazi ya kuwatumikia wananchi.
“Hakuna mtu ambaye yupo juu ya sheria na kama kuna
mwenyekiti wa mtaa fulani alienda kinyume na taratibu na kuanza kuuza ardhi,
huyo ndio anatakiwa achukuliwe hatua na sio kurudisha mihuri,” amesema Mabula.
Hata hivyo, Mabula amesema kuwa, muhuri ni mali ya
mwenyekiti wa mtaa, mkurugenzi huyo anapaswa kuacha kuchukua maamuzi ya haraka
kwa kuwanyang’anya mihuri hiyo bila sababu za msingi.
Otieno, Makamo Mwenyekiti wa Wenyekiti 172 amesema
kuwa, msimamo wao wa kutoshirikiana na mkurugenzi huyo katika shughuli za
maendeleo upo pale pale na kwamba, mchezo wa kuwanyang’anya mihuri wanafahamu
kazi yake.
Otieno amesema kuwa, mkurugenzi huyo anataka kupora
mihuri hiyo kwa manufaa yake binafsi, kwa kisingizio kwamba wenyeviti hao
wamekuwa wakiuza ardhi bila kufuata sheria kitendo ambacho alidai sio cha
kweli.
“Yeye (Mkurugenzi Kiomoni) anasema hii mihuri ni
dili ni dili gani hilo na wakati wanaouza ardhi na kuwadhulumu wananchi maeneo
yao ni watumishi wake mwenyewe, hatupo tayari kuirudisha,” amesema Otieno.
Amesema kuwa, endapo mkurugenzi huyo ataendelea
kung’ang’ania kuichukua mihuri hiyo, tayari wenyeviti hao wamekubaliana
kung’atuka na kuachia nafasi zao ili afanye kazi yeye mwenye za kuwatumikia
wananchi.
Hamza Shido, Katibu wa Wenyeviti hao Wilaya ya
Nyamagana amesema kuwa, mkurugenzi huyo amechukua uamzi wa kukurupuka bila
kushirikisha baraza la madiwani ili kulitolea ufafanuzi na kuchukua hatua.
“Tumeongea na Meya (James Bwire) tumemuuliza kuhusu
suala hili kama madiwani wana taarifa amesema hawalifahamu, no tunajiuliza yeye
anachukua hatua bila kuwashirikisha madiwani,” amesema Shido.
Kibamba, alipotafutwa kuzungumzia suala hilo,
amesema kuwa, wenyeviti wa mitaa hawana mamlaka ya kumiliki mihuri hiyo na
kwamba wenye mamlaka hiyo ni mtendaji wa mtaa huku akidai ni lazima mihuri hiyo
ataichukua.
Amesema kuwa wenyeviti hao wanagoma kurudisha mihuri
hiyo kwa kile anachodai ni upigaji wa dili wa kuuza ardhi kinyume na utaratibu
huku pia akidai kama wenyeviti hao wataachia ngazi yupo tayari kuitisha
uchaguzi mwingine.