MKURUGENZI WA MAGUFULI ALIYEMNYANYASA MWALIMU AIONYESHEA KIBURI CWT,SOMA HAPO KUJUA
ELIUD Mwaiteleke, Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Misungwi, aliyeamuru Hamis Sengo, mwalimu wa Shule ya Sekondari ya
Shilala kudeki darasa mbele ya wanafunzi ‘amekitolea nje’ Chama Cha Walimu
(CWT) mkoani Mwanza baada ya viongozi wake kutaka kumuona na kumtaka aombe
radhi, anaandika Moses Mseti.
Tukio la mkurugenzi huyo
kumdhalilisha mwalimu huyo mbele ya wanafunzi wake, lilitokea Oktoba 17, mwaka
huu shuleni hapo, baada ya ‘bosi’ huyo wa halmashauri kukuta baadhi ya madarasa
yakiwa machafu.
Mkurugenzi Mwaiteleke akiwa ameambatana na maofisa
wengine wa serikali ngazi ya wilaya hiyo, alifika shuleni hapo majira ya jioni
na kumuita mwalimu (Sengo) ili aeleze kwanini madarasa ni machafu na kumtaka
kudeki kitendo kilichotekelezwa na mwalimu huyo bila kupinga.
Sibora Kisheri, mwenyekiti wa CWT mkoani hapa
amesema kuwa wamelipokea tukio hilo kwa masikitiko na kwamba wamemtaka
mkurugenzi huyo kuomba radhi bila mafanikio.
“Tumefanya mazungumzo na tukaazimia kumtaka
mkurugenzi huyo kuomba radhi na kumhamisha mwalimu huyo shuleni hapo kwa
gharama zake na asifanye kitendo hicho kwa mwalimu mwingine.
Endapo mkurungezi huyo atashindwa kutekeleza maagizo
hayo, tutachukua hatua kali zaidi kwani tumechoka kuonewa na viongozi wa
serikali kila kukicha.
Kisheri amesema kuwa viongozi wa CWT walienda
kuonana na mkurugenzi huyo lakini hakutaka kuonesha ushirikiano kwao na alidai
kwamba leo anasafiri hawawezi kuonana na sisi.
“Mkurugenzi ni msimamizi wa watumishi lakini
tunashangaa kuona kiongozi kama huyo anageuka kuwa mnyanyasaji na viongozi
wasidhani kama sisi ni wanyonge, tunaweza kuchukua maamzi magumu zaidi ya
hayo,” amesema Kisheri.
Alipopigiwa simu yake zaidi ya mara tano, ilikuwa
ikiita na kukatwa lakini baadae ilipokelewa na mkurugenzi huyo kumtaka
mwandishi kuwa yupo barabarani na hawezi kuzungumzia suala hilo.
Mkurugenzi: Nipo
barabarani, sikusikii vizuri ni tukio gani?
Mwandishi: Ni
tukio la kumuamuru mwalimu kudeki darasa ulilolifanya Oktoba 17.
Mkurugenzi: Ngoja
nikutumie namba za afisa habari wa wilaya (Misungwi) atakueleza suala hilo.