Zinazobamba

MICHEZO MICHAFU YA LIPUMBA NA MSAJILI WAKE WA VYAMA ,YAZIDI FICHUKA,MTATIRO ABAINI UOVU HUU,SOMA HAPO KUJUA



bendera ya CUF

Kamati ya Uongozi ya Chama cha Wananchi (CUF) imedai kubaini njama za Prof. Ibrahim Lipumba waliyemfuta uanachama na kwamba anashikilia kinyume cha sheria wadhifa wa uenyekiti wa chama hicho, kuwa ana mkakati wa kuchukua ruzuku ya chama hicho kinyume cha sheria na kuitisha baraza feki ili kufanya maamuzi ya uvunjaji wa Bodi ya Wadhamini iliyoundwa kihalali na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa CUF.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi CUF, Julias Mtatiro amedai kuwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imemhakikishia Lipumba kwamba, akishafanikiwa kuivunja bodi ya wadhamini ya chama hicho, Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Francis Mutungi atabariki maamuzi ya baraza hilo aliloliita feki.
Mtatiro amesema baraza lolote litakaloketi kutokana na wito wa Lipumba waliye mvua uenyekiti, litakuwa si halali na kufafanua kuwa halitakuwa na akidi halali ya wajumbe kwa kuwa walio wengi hawamuungi mkono Lipumba hivyo hawatahudhuria.

Ameeleza kuwa, Baraza halali linalotambulika kisheria na kwa mujibu wa katiba ya chama hicho, ni lile lililochaguliwa mwaka 2014 ambalo litamaliza muda wake 2019 ambapo amesema kuwa halimtambui Lipumba kama mwenyekiti wake.
Amesisitiza kuwa, baraza halali linatakiwa liwe na wajumbe halali 53 na hii ni kutokana na baadhi ya wajumbe wake 6 kuvuliwa uanachama huku nafasi nyengine 4 zikiachwa wazi na kwamba idadi kamili ya wajumbe wa baraza hilo inatakiwa kuwa 63.
Kutokana na hoja hiyo, Lipumba hatokuwa na mamlaka ya kuitisha baraza halali kwa kuwa wajumbe 43 kati ya 53 waliohudhuria katika kikao waliliridhia Lipumba kuondolewa katika chama hicho.
“Chama chetu kinapata taarifa ya kila kitu kinachoendelea, tuna taarifa mpya kuwa Lipumba amekaa kikao na Jaji Mutungi katika kuendeleza mikakati ya kuivunja CUF, awali alikwenda Sakaya katika Ofisi ya Msajili kutafuta namna ya kupata ruzuku ya chama na kwamba wana wasiwasi kuwa ruzuku ikiingia itachukuliwa na wengine, ” amesema.
Mtatiro amedai kuwa Lipumba amepewa maelekezo kutoka kwa ofisi ya msajili wa vyama vya siasa ya kutengeneza utaratibu wa kuvunja kurugenzi za CUF na kwamba baada ya kufanikisha hilo, atafute wakurugenzi wapya aliowadai kuwa ni feki.
“Lipumba hawezi itisha Bodi halali ya Wadhamini ikasikia wito wake na kutekeleza maagizo yake sababu hana mamlaka, jana aliita watendaji wa Baraza Kuu la Uongozi Taifa lakini kwa sababu hana wajumbe halali walioitikia wito ni hawazidi 6, ila leo hii kamati yangu ikiita watendaji wanakuja wote hata iwe saa nane usiku, ” amesema.
Aidha, Mtatiro ametoa onyo kwa Jaji Mutungi kutoendelea kujihusisha na mgogoro wa chama hicho na kumtaka kutomdanganya Lipumba kuwa ana uhali wa kuendelea kuwa mwenyekiti kwa kuwa hatambuliki kisheria.
“Msajili hawezi akaamua mambo ya CUF, hiki ni chama kinaendeshwa kisheria, na wala uamuzi wake siyo wa mwisho unaweza pingwa mahakamani,” amesema.
Licha ya tuhuma hizo kwa jaji Mutungi, wabunge wa CUF wameomba kuonana nae na kwamba wanataraji kupeleka barua rasmi katika ofisi yake ili kufanya nae mazungumzo kwa ajili ya kutaka kumshauri kutoruhusu ofisi yake kukihujumu chama hicho.
Akizungumza kwa niaba ya wabunge wa CUF, Riziki Ngwale amesema wabunge wa cuf wataendelea kumsihi jaji Mutungi kutoingilia mgogoro wa chama hicho unaoendelea sasa.
“Tuanendelea kumsihi jaji Mutungi kuacha kuhujumu demokrasia kwa kumtambua mtu ambaye chama chetu hakimtambui. Na sisi wabunge tunaomba kuonana nae kwa ajili ya mazungumzo naamini atatuelewa,” amesema.