Zinazobamba

KESI YA GAZETI LA MAWIO YAZIDI KUWA NGUMU MAHAKAMANI,SOMA HAPO



Tundu Lissu, Mbunge wa Singida Mashariki (Picha kubwa) na Simon Mkina, Mhariri wa Gazeti la Mawio

UTETEZI wa wakili wa Tundu Lissu na washtakiwa wenzake watatu katika kesi ya uchochezi kupitia Gazeti la Mawio iliyofunguliwa na Jamhuri, umekwama, anaandika Faki Sosi.

Peter Kibatala ambaye ni wakili wa Lissu, Simon Mkina, Jabir Idrissa na Ismail Merhboob, aliomba mahakama kutosomwa upya mashtaka kwa watuhumiwa baada ya mtuhumiwa wa kwanza, (Jabir) kufika mahakamani.

Lissu ambaye leo hakuwepo mahakamani, ni Mbunge wa Singida Mashariki; Mkina ni Mhariri wa Mawio; Jabiri, mwandishi mwandamizi wa Mawio na Merhboob ni Meneja wa Kampuni ya Flint.


Katika kesi hiyo ya uchochezi namba 208 ya mwaka 2016 iliyofunguliwa na Jamhuri dhidi ya gazeti hilo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, upande wa mashkata ulitaka kuanza kusomwa upya mashitaka hayo kwa kuwa, Jabir hakuwepo wakati mashitaka hayo yaliposomwa kwa mara ya kwanza.
Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba baada ya kusikiliza pande zote mbili le amesema kuwa, upande wa Jamhuri wanao uwezo wa kurudisha upya mashitaka mahakamani endapo wameyakosea hivyo.
Hatua ya upande wa washtakiwa kutaka mashtaka yasisomwe upya inatokana na kufanikiwa kupangua baadhi ya mashitaka hapo awali na kwamba, kutokana na uamuzi huo, mashitaka yote yatarejeshwa upya mahakamani.
Baada ya uamuzi huo, Wakili Kibatala ametoa taarifa ya kuukatia rufaa uamuzi huo katika Mahakama Kuu.
Hakimu Simba amesema kuwa, kesi hiyo itatajwa tena tarehe 21 Agosti huku rufaa ya kesi hiyo ikiendelea.
Agosti 29, upande wa utetezi walitoa hoja za kupinga kusomewa upya mashtaka kwa washtakiwa hao.
Kibatala alidai mahakamani hapo kuwa, mashitaka yaliyofutwa na mahakama, hayawezi kurudishwa kwa utaratibu wa kuyasoma upya, isipokuwa kilichotakiwa kutendeka, ni ama kukatia rufaa uamuzi wa awali au kuomba mapitio ya uamuzi huo.
Kibatala alidai kuwa, Jamhuri ingeweza kukata rufaa au kuomba kufanya mapitio.
Upande wa mashitaka ulitaka kusoma upya mashitaka yote manne kwa kutumia mwanya wa kuyasoma kwa ajili ya mshitakiwa wa kwanza (Jabir) ambaye hakuwepo mahakamani kesi hiyo ilipofikishwa kwa mara ya kwanza.
Jabir ambaye alikuwa mgonjwa, anahusishwa katika kesi hiyo kwa kuwa mwandishi wa habari iliyopewa kichwa cha habari “Machafuko yaja Z’bar” ambayo ililalamikiwa na serikali.
Habari hiyo iliisukuma serikali kufikia hatua ya kulifuta gazeti hilo kwa madaia ya kufanya uchochezi.
Kwenye kesi hiyo, Lissu ametajwa kutoa na mchango wa maoni yake kulingana na hali ya taharuki iliyokuwepo visiwani Zanzibar.
Mawakili Kishenyi Mutalemwa na Nassoro Katuga wanaoiwakilisha Jamhuri waliingia na hati mpya ya mashitaka wakitaka kuyasoma upya kwa kile walichoeleza “mshitakiwa wa kwanza, Jabir Idrissa amefika mahakamani kwa mara ya kwanza.”
Wakili wa utetezi Kibatala alipinga akieleza kuwa, hata kama mahakama itaridhia kupokea hati hiyo, ichukuliwe kama ni kuiona tu na sio kuitambua kama hati halali kwa kuwa “hati ina mashitaka yaliyofutwa tayari… na waendesha mashitaka wenyewe waliridhia kufutwa mashitaka.”
Alikazia hoja yake akieleza kuwa, mahakama iliyafuta mashitaka mawili – la kwanza na la tano – baada ya upande wa mashitaka wenyewe kuridhika kwamba, hayakuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).
Wakili Mutalemwa aliomba muda wa saa moja, kupitia maelezo ya kisheria ili aweze kujibu hoja za utetezi lakini hata alipokubaliwa, alishikilia maelezo ya kutaka mahakama iruhusu washitakiwa wasomewe mashitaka yote.
Hakimu Simba alikataa rai hiyo. Badaa yake akambana mwendesha mashitaka kusoma mashitaka yaliyokubaliwa – la pili, tatu na nne – vinginevyo angewaachia watuhumiwa kwa kukosekana mashitaka mbele ya mahakama hiyo.
Upande wa mashitaka ulisoma mashitaka hayo matatu yaliyobaki kwa washitakiwa; la pili likimkabili Jabir, Mkina na Lissu, wakidaiwa kuchapisha chapisho la uchochezi katika Gazeti la MAWIO, toleo Na. 182 la tarehe 14-20 Januari 2016.
Shitaka la tatu linamuhusu Ismail akidaiwa kuchapisha chapisho la uchochezi katika gazeti hilo lenye kichwa cha Habari ‘Machafuko yaja Z’bar’.
Shitaka la nne linamkabili Ismail akidaiwa kuchapisha gazeti bila kupeleka kiapo kwa Msajili wa Magazeti.