WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA ATOA AGIZO HILI,SOMA HAPO KUJUA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameitaka
Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kuweka mikakati endelevu ya kuwawezesha
wananchi kuvua katika maji ya kina kirefu cha bahari kwa kutumia meli kubwa na
za kisasa ili Taifa liweze kunufaika na rasilimali hiyo ambayo imekuwa
ikichukuliwa na wavuvi wenye vyombo vya kisasa kutoka nje ya nchi.
Aidha, amezitaka halmashauri zote
nchini ziweke mikakati na mipango ya kuifanya mito na maziwa mbalimbali nchini
kuwa na uvuvi endelevu kwa kufuatilia kwa karibu shughuli za wavuvi na
kuwaadhibu wote watakaovua kinyume na sheria.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo
(Jumatatu, Agosti 01, 2016) wakati akifungua maadhimisho ya 23 ya sherehe za
maonesho ya wakulima Kanda ya Mashariki katika Uwanja wa Mwalimu J.K Nyerere
yanayofanyika katika mkoa wa Morogoro ambapo amesema bado nchi haijaweza
kutumia rasilimali hiyo kikamilifu.
Amesema halmashauri zinatakiwa
zihamasishe vijana kuunda vikundi vya kuanzisha miradi ya kufuga samaki katika
maeneo yao na wewezeshwe kupata teknolojia ya ufugaji huo.
Akizungumzia vikundi vya
wajasiariamali wanaovua katika maeneo ya bahari na maziwa alishauri waelimishwe
kuhusu namna ya kupata mikopo ya kununulia zana bora za kisasa za uvuvi ili
shughuli zao ziwe na tija.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amesema
wakulima wanatakiwa kuzingatia matumizi ya kanuni bora za kilimo ikiwemo
matumizi sahihi ya zana za kisasa, pembejeo na viuatilifu vilivyopendekezwa na
wataalam ili kufanikisha mapinduzi ya kilimo kuelekea kilimo cha biashara.
Akizungumzia kuhusu suala la
usindikaji alisema wakati anatembelea mabanda mbalimbali alipata fursa ya kuona
teknolojia zinazoweza kutumiwa na wakulima, wafugaji na wavuvi katika kuongeza
uzalishaji bora wenye tija.
Amesema amefurahi kuona wakulima,
wafugaji na wafanyabiashara wa mazao, pembejeo na zana za kilimo wana ari kubwa
ya kushiriki katika kuleta mapinduzi katika sekta ya kilimo ili kwenda sambamba
na kasi ya Serikali ya kuifanya nchi kujitosheleza kwa chakula na kuendeleza
uchumi wa viwanda.
“Naamini kuwa pamoja na lengo la
kujitosheleza kwa chakula, wakulima, wafugaji na wavuvi wataongeza ari ya
uzalishaji kwa kushirikiana na sekta za umma na binafsi katika kuvipatia
viwanda vyetu malighafi na kuongeza thamani ya mazao,” alisema.
Kufuatia hatua hiyo Waziri Mkuu aliziagiza
halmashauri zote kuhamasisha uanzishaji na uendelezaji wa viwanda vidogo vya
kusindika mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi kwa kushirikisha taasisi za umma na
binafsi, mashirika na vikundi vya ujasiriamali katika maeneo yao.
Akizungumzia namna Serikali
ilivyojipanga kutatua changamoto ya migogoro baina ya wafugaji na wakulima
Waziri Mkuu alisema wafugaji wenye mifugo mingi watahamishiwa katika vitalu
vinavyomilikiwa na ranchi za Taifa na wenye mifugo michache watatengewa maeneo
katika vijiji.
Awali Waziri Mkuu alitembelea baadhi
ya mabanda na maeneo ya vipando vya mazao mbali mbali yaliyoko katika viwanja
hivyo ambapo alisema ameridhishwa na juhudi zilizofanyika katika maandalizi ya
maonesho ya mwaka huu ikiwa ni pamoja na uendelezaji wa uwanja huo.
“Napenda kutoa pongezi za dhati kwa
kujenga miundombinu na nyumba za kudumu za kufanyia maonesho. Aidha, natoa
shukrani za pekee kwa Halmashauri zetu, Mashirika yetu ya Umma na binafsi; na
watu binafsi ambao wamejenga na wanaendelea kujenga majengo mazuri na ya
kudumu,” alisema.
Pia alizindua jengo la Halmashauri ya
Wilaya ya Temeke na kusema kuwa uboreshaji wa viwanja hivyo unaonesha jinsi
wadau wote katika sekta ya kilimo, mifugo, uvuvi na ushirika wanavyotambua
umuhimu wa maonesho hayo kama njia ya kuongeza maarifa na kumuenzi mkulima,
mfugaji na mvuvi kwa kutambua mchango wao katika uchumi wa Taifa.
Kauli mbiu ya maonyesho hayo kwa mwaka
huu ni kilimo, mifugo na uvuvi ni nguzo ya maendeleo: vijana shiriki
kikamilifu (“HAPA KAZI TU”)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, AGOSTI 01, 2016.