Zinazobamba

TANZANIA YAENDELEA KUPATA MAFANIKIO KATIKA KUKABILIANA NA UGONJWA WA VIKOPE (TRACHOMA)

Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk.Neema Rusibamayila akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa Mkutano uliowahusiaha  Wadau wa Wizara hiyo na washirika wa maendeleo Maendeleo kutoka Mfuko wa Malkia Elizabeth unaojihusisha na utokomezaji wa Ugonjwa wa Vikope na wale wa Idara ya Kimataifa ya Maendeleo (DFID).
Mkurugenzi Mkuu wa mfuko wa Malkia wa Uingereza unaojihusisha na utokomezaji wa ugonjwa wa Vikope katika nchi mbalimbali za Bara la Afrika ikiwemo Tanzania (The Queen Elizabeth Diamond Jubilee Trust Trachoma Initiative) Dk. Aristid Bonifield akieleza namna Mfuko huo utavyoendelea  kuisaidia Tanzania kwa kuwa inafanya vizuri katika kuhakikisha ugonjwa huo unatokomezwa nchini leo jijini Dar es salaam.
 Mkuu wa Idara ya Kimataifa ya Maendeleo nchini Tanzania (DFID) Vel Gnanendra akifafanua namna wadau wa maendeleo walivyojipanga kuiunga mkono Tanzania kwa kuhakikisha ugonjwa wa vikope (Trachoma) unatokomezwa nchini.
Mratibu wa Taifa wa Magonjwa yasiyopewa kipaumbele,   Upendo John Mwingira akizungumza wakati wa mkutano huo leo jijini Dar es salaam.
 Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Sightsavers kutoka Uingereza Dk. Caroline Harper akifafanua jambo wakati wa Mkutano wa wadau wa kutokomeza ugonjwa wa Vikope leo jijini Dar es salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Sightsavers kutoka Uingereza Dk. Caroline Harper akifafanua jambo wakati wa Mkutano wa wadau wa kutokomeza ugonjwa wa Vikope leo jijini Dar es salaam.
Washiriki wa Mkutano wa Kutokomeza Ugonjwa wa Vikope kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto  na Wale wa Mashirika ya Kimataifa wakiwa katika picha ya Pamoja leo jijini Dar es salaam.Picha/Aron Msigwa – MAELEZO.


Na. Aron Msigwa – Dar es salaam.

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeeleza kuwa licha ya Tanzania kuendelea kupata mafanikio katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Vikope (Trachoma) jamii bado inalojukumu la kuendelea kuzingatia na kufuata kanuni za afya kwa kufanya usafi wa mwili na mazingira ili kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa Mkutano wa Wadau wa magonjwa yasiyopewa kipaumbele wenye lengo la kuutokomeza ugonjwa wa Vikope,  Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk.Neema Rusibamayila amesema kuwa Tanzania imepiga hatua katika kupunguza ugonjwa huo ikishirikiana na wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi.

Amesema kupitia idadi ya wagonjwa wanaougua vikope imeendelea kupungua mwaka hadi mwaka kupitia afua mbalimbali chini mpango ujulikanao kama “SAFEambao unahusisha huduma za Upasuaji,utoaji wa dawa za Antibayotiki, kuosha uso  pamoja na usafi wa mazingira.

Ameeleza kuwa  wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeweza kufanikisha upunguzaji wa ugonjwa huo kwa kutoa dawa/tiba kinga kwa wananchi katika maeneo yaliyoathirika ambapo amesema kufuatia utafiti uliofanyika mpaka sasa wilaya 22 ugonjwa huo umepungua sana kiasi cha wananchi wa maeneo hayo kutohitaji dawa za tiba kinga.

Aidha, amesema kuwa juhudi za sasa ni kuendelea kuwaelimisha wananchi kuendelea kuchukua hatua kwa kufanya usafi ikiwemo unawaji wa uso pamoja pia kuwaangalia wale waliokwisha kuugua ugonjwa wa Vikope (Trachoma) ili waweze kufanyiwa upasuaji.

“Baada ya mtu kupata ugonjwa huu kope za mgonjwa huingia ndani , kope za mtu ambaye hana ugonjwa huu hutoka nje, zikiingia ndani zinakwaruza jicho na mtu asipofanyiwa upasuaji kope zake mapema na kuziacha zikaendelea kukwaruza jicho mwisho mgonjwa huyu hupata upofu” Amesisitiza Rusibamayila.

Amefafanua kuwa mashirika mbalimbali yamekuwa mstari wa mbele katika kufanikisha zoezi hilo ikiwemo Shirika na la Msaada la Kimataifa la Uingereza (DFID) pamoja na Mfuko wa Malkia ya Uingereza (The Queen Elizabeth Diamond Jubilee Trust) ambao umekua ukitoa fedha kutokomeza ugonjwa wa Trakoma , shirika la Sightsavers, Shirika la Helen Keller International (HIK) Tanzania pamoja na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali ambayo mengine yapo Kongwa mkoani Dodoma na Kilimanjaro ambao hushirikiana na wizara kuwatafuta wagonjwa kwa lengo la kutoa matibabu.

Amesema mpaka sasa kuna wilaya 18 ambazo zinakabiliwa na ugonjwa huo na kufafanua kuwa juhudi za kuwapata walioathirika zinaendelea ikiwa ni pamoja na kuwapata wale walioathirika kwa lengo la kuwafanyia upasuaji na kuwapatia dawa ya tiba kinga pia kuwaelimisha ili waweze kubadili tabia kwa kuwa wasafi.

“Tunaendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo uelimishaji wa wananchi wa maeneo husika wachukue hatua, tunajua ugonjwa huu unaletwa na nzi, tunawahimiza wananchi wanawe uso kuondoa uchafu na kuzuia nzi wanaosambaza ugonjwa huo kutua kwenye macho yao” Amesisitiza Dk. Dk.Neema Rusibamayila.

Aidha, amewashukuru wadau hao wa maendeleo kwa kuendelea kutambua mchango wa Tanzania katika mapambano dhidi ya magonjwa hayo na pia kuendelea kutimiza malengo ya kidunia ambayo yanaeleza kwamba ifikapo mwaka 2020 Tanzania iwe imeondoa ugonjwa wa vikope nchini.

Akizitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili kampeni ya kuwafikia wale walioathirika katika maeneo yaliyo na ugonjwa huo hasa kwenye jamii za wafugaji amesema  ni pamoja na hali ya wananchi hao huishi kwa kuhamahama pia sababu za mazingira hasa miundombinu ya barabara ambayo imekua kikwazo cha kuzifikia jamii hizo hasa wakati wa kipindi cha mvua.

Kwa upande wake Mratibu wa Taifa wa Magonjwa yasiyopewa kipaumbele kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto   Upendo John Mwingira akizungumza wakati wa mkutano huo amesema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi za Bara la Afrika ambazo zimekuwa zikinufaika na fedha kutoka Shirika la Kimataifa la Uingereza na DFID na mfuko wa ulioanzishwa wa kumuenzi Malkia wa Uingereza kwa miaka 60 ya Utawala wake unaojihusisha na utokomezaji wa ugonjwa wa Trakoma katika nchi mbalimbali za Bara la Afrika Tanzania ikiwemo.

Amesema ugonjwa wa Vikope nchini Tanzania kwa mujibu wa Takwimu uko katika wilaya 56 na kueleza kuwa kutokana na juhudi ambazo zimekuwa zikichukuliwa na Serikali kuanzia mwaka 1990 hali inaonesha kuwa maabukizi yameshuka hasa katika wilaya 22 ambako wananchi hawahitaji tena ugawaji wa dawa.

Amesema kuwa hali ya maambukizi katika maeneo hayo imekuwa zaidi kwa watoto na wanawake kwenye maeneo yenye ukame na shida ya maji ikiwemo mkoa wa Manyara na Dodoma na kubainisha kuwa mpaka sasa ni wilaya 18 ambazo zinahitaji huduma ya dawa katika mkoa wa Arusha , Manyara, Dodoma katika wilaya ya Kongwa, Chemba na Chamwino.

“Naweza kusema jitihada tunazofanya ni kubwa na kazi bado ipo hasa maeneo ya wafugaji ambao baadhi yao wamekuwa wakitumia kifaa Fulani ambacho kinaweza kunyofoa zile kope zinazowasumbua ili kuondoa usumbufu bila kujua hali hiyo inatengeneza tatizo zaidi, ni changamoto kwetu, tunahitaji kuendelea kuwaelimisha” Amesisitiza.

Ameeleza kuwa kupitia juhudi mbalimbali zilizofanyika wanajiandaa kufanya tathmini katika wilaya zipatazo 10 katika kipindi cha mwaka huu kuangalia maambukizi yamefikia wapi kwa lengo la kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa Trakoma na kupunguza hali ya maabukizi katika wilaya hizo.

Akizungumzia idadi ya wagonjwa katika wilaya 56 ambazo maambukizi ya ugonjwa huo yapo ilikadiliwa kwamba kuna maambukizi ya watu takribani 160,000 ambao wameambukizwa tayari Vikope na kubainisha kwamba kuna mikakati mbalimbali ilifanywa na Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuendesha  upasuaji kwa wagonjwa wenye tatizo hilo hali iliyoshusha kiwango hicho hadi kufikia wagonjwa 80,000 mwaka huu.

Amesema chini ya ufadhili wa wadau hao wa miaka 5 wagonjwa takribani 50,000 wenye tatizo la vikope watafanyiwa upasuaji, huku Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine ikiendelea kutafuta fedha za kuwafikia wagonjwa 30,000 watakaobaki.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Kimataifa ya Maendeleo nchini Tanzania (DFID) Vel Gnanendra amesema kuwa wao kama wadau wa maendeleo wataendelea kuiunga mkono Tanzania kwa kuhakikisha ugonjwa wa vikope (Trachoma) unatokomezwa nchini.

“Tunafurahia ushirikiano huu kutoa mchango wetu kuisaidia Tanzania kutokomeza ugonjwa wa Vikope (Trachoma), kuzuia maumivu na mateso yanayosababishwa na ugonjwa huu yanayowafanya watu kuangukia katika lindi la umasikini, Tunaiahidi Serikali ya Tanzania kuwa kupitia ushirikiano huu tutautokomeza ugonjwa huu na kubadili maisha ya wengi miaka ijayo” Amesisitiza Gnanendra.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa mfuko wa Malkia wa Uingereza unaojihusisha na utokomezaji wa ugonjwa wa Vikope katika nchi mbalimbali za Bara la Afrika ikiwemo Tanzania Dk. Astrid Bonfield CBE amesema kuwa Mfuko huo utaendelea kuisaidia Tanzania kwa kuwa inafanya vizuri katika kuhakikisha ugonjwa huo unatokomezwa nchini.

Amesema Mfuko wa Malkia Elizabeth utafanya kazi bega kwa bega na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya, maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuhakikisha kuwa hakuna mtanzania anayepoteza haki ya kuonakutokana na ugonjwa wa vikope.

" Kwa pamoja tutahakikisha hakuna mtanzania anayepata shida na madhara yanayotokana na ugonjwa wa Vikope, tutafanya kazi na Serikali ya Tanzania tukishirikiana na wadau wengine wa Maendeleo na mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali kutokomeza ugonjwa huu" Amesisiza Dk. Astrid.