CHADEMA SASA KUKINUKISHA NCHI NZIMA,YATANGAZA MAPAMBANO RASMI,MBOWE ASEMA UVUMILIVU SASA BASI,SOMA HAPO KUJUA
Kamati Kuu ya Chadema wakishikana mikono kuonyesha mshikamano |
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
kimeanzisha opereshani “Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania” (Ukuta) ikiwa
ni sehemu ya maazimio ya Kamati Kuu ya chama hicho iliyoketi tarehe 23 – 26
mwezi huu, anaandika Pendo Omary.
Utekelezaji wa operesheni hiyo utaenda sambamba na chama
hicho kufanya mikutano ya hadhara kuanzia tarehe 1 Septemba mwaka huu, huku
viongozi wa chama hicho ngazi ya msingi hadi taifa wakitakiwa kukaa vikao vya
kikatiba na kuelekezwa ajenda ya vikao hivyo kuwa ni kujadili hali ya siasa na
uchumi.
Akizungumza
katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Freeman Mbowe,
Mwenyekiti wa Chadema Taifa amesema, hatua hiyo imechukuliwa ili kujenga jamii
inayozingatia misingi ya uhuru, haki, udugu na amani.
“Ni
wazi sasa kuwa, kuna tishio kubwa dhidi ya ukuaji wa demokrasia hapa nchini
mwetu kutoka kwa viongozi wa serikali hii ya awamu ya tano ambao wanakandamiza
demokrasia na madhara yameshaanza kulitafuna taifa letu,” amesema Mbowe.
Ametaja
baadhi ya matukio ya ukandamizaji wa haki na demokrasia nchini kuwa ni; kupiga
marufuko mikutano ya vyama vya siasa wakati Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kinaendelea kufanya, kupiga marufuku urushwaji wa moja kwa moja wa mijadala ya
Bunge na kudhibiti wabunge wa upinzani bungeni kupitia kwa Dk. Tulia Ackson,
Naibu Spika
.
Matokeo
mengine ni kuingilia mhimili wa mahakama, kupuuza utawala wa sheria, serikali
kupeleka mswada kandamizi wa Sheria ya Haki ya Kupata Habari, serikali za mitaa
kunyang’anywa mapato na serikali kuu na uteuzi wa wakurungezi, makatibu tawala
wa wilaya bila kuzingatia sheria ya utumishi wa umma.
“Mbali
na hayo, serikali pia imetoa maelekezo kupitia mawasiliano yake na mabalozi
kuelekeza kuwa, kabala ya mabalozi au maofisa wa ubalozi kukutana na asasi
zisizo za kiserikali au vyama vya siasa ni lazima kwanza waombe kibali cha
serikali kupitia wizara ya mambo ya nje.
“Pia
kwa sababu ya hasira ya kukataliwa na CCM, vikosi vya ulinzi na hasa Jeshi la
Polisi vimekuwa vikishiriki katika vitendo kadhaa vya ukiukwaji wa haki za raia
huko Zanzibar ambapo kwa zaidi ya miezi sasa, wamekuwa wakipita katika vijiji
na kuwapiga, kuwatesa, kuwakamata, kuwatishia na hata kuharibu mali za wananchi
na mifugo yao,” amesema Mbowe