Zinazobamba

PROFESA LIPUMBA KUIUA CUF,SOMA HAPO KUJUA



Lipumba-Lowassa

HATIMAYE Prof. Ibrahim Lipumba, aliyekuwa Mwenyekti wa Chama cha Wananchi (CUF) ametangaza kurejea kwenye nafasi yake ya uenyekiti-taifa wa chama hicho, anaandika Faki Sosi.

Amesema, anarejea kwenye nafasi hiyo baada ya muda wa kutosha alioutumia kutafakari siasa za nchini na namna demokrasia inavyokanyagwa na watawala wa nchi hii.

“Nimemwandikia Katibu Mkuu (Maalim Seif Sharif Hamad) kutengua barua yangu niliyoandika 5 Agosti mwaka jana,” amesema Prof. Lipumba.

Prof. Lipumba alijiuzulu nafasi yake mwaka jana kwa madai ya kutoridhishwa na uamuzi wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kumridhia Edward Lowassa kupeperusha bendera ya umoja huo kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015 kupitia Chadema.

Hatua hiyo imeibua maswali kwamba, je sababu za kujiuzulu kwake zimepatiwa ufumbuzi? Lowassa bado yupo, je ni ipi hatma ya Ukawa?

Ndani ya CUF kuliibuka makundi mawili, moja likimtaka na lingine likitaka atose, je nini hatma ya makundi hayo?
Hata hivyo amesema, analazimika kurejea kwenye nafasi ya uenyekiti wa chama hicho taifa kutokana na kuguswa na matatizo ya demokrasia nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam amesema kuwa, amemuandikia barua Maalim Seif ili atengue uamuzi wake wa awali wa kuachia nafasi hiyo.

Kabla ya hatua yake ya leo, ndani (CUF) kuliibuka makundi mawili makuu, moja likimtaka Prof. Ibrahim Lipumba aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho na lingine likitaka atoswe.

Kwa muda wote huo Prof. Lipumba alikaa kimywa. Hata alipoulizwa na wanahabari msimamo wake, hakutaka kueleza chochote.
 
Katiba ya mwaka 1992 Toleo 2013 Ibara ya 117 inayoeleza kwamba, barua ya kujiuzulu inapaswa kujadiliwa na Mkutano Mkuu kujadili jambo ambalo mpaka sasa halijafanyika.

Prof. Lipumba aliteuliwa kutwaa nafasi hiyo na Mkutano Mkuu mwaka 1999. Ibara hiyo inaipa mamlaka mkutano huo kukubali ama kukataa kujiuzulu kwake na kwamba, kauli yake ya leo kuwa Maalim Seif atengue barua yake inatokana na kutokwenda kwenye ngazi hiyo (Mkutano Mkuu) nyingine ya uamuzi.

Prof. Lipumba amesema kuwa, dhuluma iliyofanyika katika visiwa vya Zanzibar ya kuporwa kwa haki ya wananchi, imemsukuma kurejea kwenye mapambano ya haki nchini.
Amesema, demokrasia ya Tanzania ina matatizo akitaja miongoni mwayo ni Bunge kuendesha kwa itikadi ya chama.
Pia amesema  kuwa, uongozi wa Rais John Magufuli unaonekana kuwa wa kasi isiyojali Demokrasia.
Akizungumzia Zanzibar amesema, chama chao na watanzania wapenda haki hawatambui utawala wa Dk. Ali Mohammed Shein visiwani humo kwa kuwa hakupatikana kwa njia halali ya kidemokrasia.
Amesema kuwa, Rais Magufuli asipozingatia  misingi ya demokrasia nchi haitakuwa na uwajibikaji.
Awali ndani ya chama hicho yaliibuka makundi amwili, moja likimtaka na lingine likipinga kurejea kwake.
Mvutano huo ulidhihiri kwenye kongamano lililoandaliwa na Kata ya Makurumla Manispaa ya Kinondoni ambapo wajumbe waliibua hoja ya ukimya wa taarifa kuhusu maombi ya kujiuzulu ya Prof. Lipumba ambayo hayakuwa yamejibiwa.
Katika kongamano hilo, Mohamed Mgomvi, mmoja wa wanachama wa CUF alisema, upande wa bara chama hicho kimebaki kwenye uyatima na kwamba hakuna mtu madhubuti anayeweza kukiendesha kama Prof. Lipumba.
“Nashangaa viongozi wetu mnasema habari zisizoeleweka juu ya kujiuzulu kwa Lipumba badala ya kusema ukweli nini kinaendelea huko ndani, tangu alipoondoka Lipumba hakuna maendeleo alafu mnasema tupo pamoja naye, haiingii akilini hata kidogo,” alisema.
Maganga Dachi, mwanachama wa CUF katika mkutano huo pia alisema, kwa mujibu wa Katiba ya CUF, barua ya kujiuzulu inatakiwa ifike katika Mkutano Mkuu uliomchagua jambo ambalo halijafanyika.
“Kwa hatua hiyo chama kinavunja Katiba maana hadi leo hakuna kinachoendelea kama hivyo suala la Lipumba, linatakiwa kuwasilishwa kwenye Mkutano Mkuu nasi tunamtaka Lipumba arudi katika nafasi yake ili chama kiendelee na shughuli za kimaendeleo,” alisema Dachi.
Ushawishi ndani ya chama hicho uliendelea kufanywa na baadhi ya wanachama pia viongozi wa chama hicho kumrejesha Prof. Lipumba kwenye nafasi hiyo.

Hakuna maoni