MBUNGE MNYIKA ALIPUKA NA MABOMU YA RICHMOND NA ESCROW BUNGENI,AWA MBOGO,SOMA HAPO KUJUA
MAAZIMIO ya Bunge kuhusu Richmond, Akaunti ya
‘Escrow’ pamoja na umiliki wa Kampuni ya IPTL yameibuka tena bungeni na kuipa
serikali wakati mgumu, anaandika Faki Sosi.
Akiwasilisha Hotuba ya Msemaji wa Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara ya Nishati na Madini kuhusu Mapato na
Matumizi katika Mwaka wa Fedha 2016/2017, msemaji wa wizara hiyo John Mnyika
ameibua upya hoja kuhusu utekelezwaji wa maazimio ya bunge. Ifuatayo ni sehemu
ya hotuba yake.
UTEKELEZAJI WA MAAZIMIO YA BUNGE KUHUSU RICHMOND NA
KUHUSU AKAUNTI YA ‘ESCROW’ YA TEGETA PAMOJA NA UMILIKI WA KAMPUNI YA IPTL
Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kurejea
maamuzi/maazimio ambayo Bunge hili Tukufu lilikwisha yafanya kuhusiana na
mikataba ambayo Serikali inaingia na makampuni mbalimbali hasa kwenye sekta ya
nishati na madini.
Mheshimiwa Spika, Taarifa mbili za serikali kuhusu
utekelezwaji wa maazimio haya ziliwasilishwa Bungeni tarehe 28 Agosti, 2008 na
tarehe 11 Februari, 2009. Taarifa moja ilikabidhiwa na kujadiliwa na Kamati,
ambazo zililitaarifu Bunge kuwa utekelezaji wa Maazimio 10 kati ya 23
yaliyotolewa na Bunge, yalifanyiwa kazi hadi mwezi Februari, 2009 na Maazimio
13 bado yalikuwa hayajakamilika.
Mheshimiwa Spika, Bunge liliazimia kwamba taarifa za
utekelezaji wa maazimio yaliyobaki ziwasilishwe kwa Kamati ya Mambo ya Nje,
Ulinzi na Usalama ambayo hata hivyo kuanzia mwaka 2011 mpaka mwaka huu wa 2016
kamati hiyo haikuwasilisha taarifa yoyote bungeni ya kueleza kukamilika kwa
utekelezaji wa maazimio husika hali ambayo inahitaji bunge kuingilia kati
kuweza kuisimamia Serikali kwa mujibu wa Katiba ya Nchi Ibara ya 63 (2) na (3).
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani iliitaka
Wizara ya Nishati na Madini na Serikali kwa ujumla kutoa majibu bungeni juu ya
hatma ya maazimio 10 yaliyobaki: Azimio Namba 3,5,7,8,9,10,11,13,14 na 18 ili
bunge liweze kuishauri na kuisimamia serikali kuhakikisha maazimio husika
yanatekelezwa kwa ukamilifu na kwa haraka. Lakini hadi sasa tunaposoma hotuba
hii maazimio hayo ya Bunge bado hayajatekelezwa na Bunge kupata mrejesho rasmi.
Mheshimiwa Spika, aidha Katika maazimio ya Bunge
kuhusiana na fedha ufisadi uliofanyika katika akaunti ya “Tegeta escrow” na
umiliki wa IPTL, maazimio yanayohusu sekta ya nishati na madini bado
hayajatekelezwa kwa ukamilifu wake, maazimio hayo yaliyotolewa na Bunge la
Kumi, Mkutano wa Kumi na Saba katika kikao cha Ishirini kilichofanyika tarehe
29 Novemba, 2014 katika azimio namba 2,7 na 8.
Mheshimiwa Spika, Bunge katika azimio namba 2
liliazimia kwamba naomba kunukuu;
KWA KUWA, Taarifa Maalum ya Kamati imeonesha jinsi
ambavyo TANESCO imekuwa ikitumia mabilioni ya fedha kulipa gharama za umeme
unaozalishwa na IPTL na hivyo kuathiri hali ya kifedha ya Shirika hilo;
NA KWA KUWA, Taarifa Maalum ya Kamati inaonesha
kwamba TANESCO itaendelea kulipa fedha nyingi kwa ajili ya gharama za umeme huo
wa IPTL;
HIVYO BASI, Bunge linaazimia kwamba Serikali
iangalie uwezekano wa kununua mitambo ya kufua umeme ya IPTL na kuimilikisha
kwa TANESCO kwa lengo la kuokoa fedha za Shirika hilo.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani
inasikitika kuona kwamba, mbali ya Serikali kushindwa kununua lakini bado
inaendelea kulipia gharama za “capacity charges” na hivyo kuendelea kukiukwa
kwa azimio ya Bunge. Hivyo basi tunamtaka Waziri alieleze Bunge ni kwa kiasi
gani azimio hilo limetekezwa?
Mheshimiwa Spika, katika azimio namba 7 lililohusu
kuwajibishwa kwa Mawaziri na watendaji wakuu wa wizara na Bodi ya Tanesco
lilisema kwamba, nanukuu;
“KWA KUWA, vitendo vya kijinai wanavyohusishwa navyo
viongozi wa umma na maafisa wa ngazi za juu serikalini vinakiuka pia maadili ya
viongozi wa umma na kuwanyima viongozi na maafisa hao uhalali wa kuendelea
kushikilia nafasi za mamlaka katika uongozi wa umma;
HIVYO BASI, BUNGE LINAAZIMIA KWAMBA, Waziri wa
Nishati na Madini, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini na Wajumbe wa Bodi
ya Wakurugenzi wa TANESCO wawajibishwe, kwa kuishauri mamlaka yao ya uteuzi
kutengua uteuzi wao;”
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais bila ya kujali
nini Bunge lilikwisha azimia katika kikao ambacho na yeye alikuwa sehemu ya
azimio hilo, lakini bado akamteua Mhe Prof. Muhongo kuendelea kuiongoza wizara
hii. Kambi Rasmi ya Upinzani inaliona jambo hili kama ni dharau sana kwa Bunge
na ni fedheha binafsi kwake.
Mheshimiwa Spika, Bunge katika azimio namba 8 la
taarifa ya ukaguzi maalum kuhusiana na miamala iliyofanyika katika akaunti ya
‘escrow’ ya tegeta pamoja na umiliki wa kampuni ya Iptl iliazimiwa kwamba
“HIVYO BASI, Bunge linaazimia kwamba Serikali
itekeleze Azimio husika la Bunge mapema iwezekanavyo na kwa vyovyote vile kabla
ya kumalizika kwa Mkutano wa Bunge la Bajeti Serikali iwasilishe taarifa ya
utekelezaji wa mapitio ya mikataba ya umeme”
Mheshimiwa Spika, Azimio hili linashabihiana na
azimio namba 13 lililoazimiwa na Bunge wakati wa majadala wa taarifa ya kamati
teule ya Richmond lililosema kwamba;
“……….. Kamati Teule inatoa wito kwa Serikali
kuondokana na utaratibu huu usio na tija kwa kuzihusisha Kamati za Kudumu za
Bunge kwenye hatua za awali za maandalizi ya mikataba hiyo. Aidha, Kamati Teule
inatoa wito kwa Kamati zote za Bunge zihakikishe kuwa zinapitia mikataba
mikubwa na ya muda mrefu ya kibiashara chini ya sekta zao ili kuliondolea Taifa
mizigo isiyo ya lazima. Pale ambapo upatikanaji wa mikataba hiyo unakwamishwa
kwa urasimu usio wa lazima Kamati zitumie utaratibu uliotumiwa na Kamati ya
Bunge ya Uwekezaji na Biashara ya kuunda Kamati Teule yenye ufunguo wa mikataba
iliyofichika”.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani
imelazimika kunukuu maazimio hayo kutokana na ukweli kwamba Serikali imeshindwa
kabisa kutekeleza maazimio ya Bunge, na badala yake mikataba hiyo inaendelea
kutekelezwa kama ilivyoingiwa, mfano mzuri ni TANESCO kuendelea kuilipa IPTL
fedha za capacity charge mpaka sasa. Jambo hili linazidi kuliondolea shirika
hilo la umeme uwezo wa kuwahudumia wateja wake kwani haliwezi kuwekeza zaidi
katika miundombinu za kusambaza umeme kutokana na kutokuwa na fedha za kutosha.
Mheshimiwa Spika, mfano mwingine wa mikataba yenye
mashaka ni ule wa Mchuchuma na Liganga ambao NDC iliingia ubia na kampuni ya
kichina ya HONGDA SICHUAN LTD na kuunda kampuni ya Ubia ya Tanzania China Internatinal
Mineral Resource Ltd- TCIMRL katika kampuni hiyo ya ubia HONGDA SICHUAN LTD
inamiliki asilimia 80 na NDC inamiliki asilimia 20.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wabia wanakuja mikono
mitupu bila hela, sasa mbia mkubwa anatafuta mtaji kwa kutumia rasilimali za
Kampuni ya ubia kama dhamana. Hizi rasilimali za Kampuni ya ubia ni zile
zinazotakiwa kuchakatwa na kuuzwa, katika mazingira yoyote yale tukakubali vipi
kuwa ubia wa njia hii unainufaisha nchi?
Mheshimiwa Spika, kama tunaweza kutumia rasilimali
zetu kama dhamana ni kwanini tuingie ubia na tusitoe ajira kwa wataalamu
waliobobea katika fani hizo na sisi tukawa na umiliki wa asilimia 100?
Kambi Rasmi ya Upinzani inasema mikataba ya jinsi
hii ndiyo itakayoliangamiza taifa letu, ni kwa nini wataalam wanaoingia
mikataba ya namna hii wanatakiwa kuendelea kuwa maofisini?
Mheshimiwa Spika, licha ya ubabaishaji wa Kampuni
hiyo ya Kichina bado ina uhakika kwamba mkopo wa kutumia rasilimali zetu
ukipatikana ianze kuiuzia Tanesco umeme wa 600MW, hoja ya msingi je uhalali wa
TANESCO kununua umeme wa Mchuchuma na Liganga utakuwa wapi?
Hakuna maoni
Chapisha Maoni