Zinazobamba

ZITTO KABWE AMPOPOA RAIS MAGUFULI NA SERIKALI YAKE,SOMA HAPO KUJUA



Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe

ZITTO Kabwe, Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT- Wazalendo amesema, Rais John Magufuli anapapasa suala la ufisadi, anaandika Pendo Omary.

Amesema, serikali yake bado haijachukua hatua madhubuti katika vita dhidi ya rushwa nchini licha ya ‘shangwe’ nyingi.
Ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano wa Halmashauri Kuu ya ACT- Wazalendo.

“Bado Rais hafanyi inavyopaswa, bado rais anapapasa suala la ufisadi. Kuna mambo ya muda mrefu ambayo tunaendelea kama nchi kuyalipua lakini arais ameyakalia kimya. Mfano ni suala la Tegeta Escrow,” amesema Zitto na kuongeza;

“Bado mtambo wa IPTL upo chini ya matapeli na kila mwezi serikali inawalipa matapeli hawa zaidi ya Sh. 8 bilioni wazalishe au wasizalishe umeme.

“Hivi ndio vikundi maslahi  katika sekta ya nishati ambavyo bila kuvibomoa, rais ataonekana anachagua katika vita hii.”
Zitto amesema, serikali imeficha inaowaita madalali wa rushwa katika suala la hati fungani ya Dola za Marekani 6 milioni.
Na kwamba, tayari kuna watu wamefikishwa mahakamani lakini  walioitoa rushwa hiyo ambao ni Benki ya Standard ya Uingereza na waliopokea ambao ni maofisa wa serikali, hawakupelekwa mahakamani.
“Hati fungani hii ambayo serikali imeanza kulipa riba yake ni ghali mno na imeongeza deni la taifa kwa kiwango cha Sh. 1.2 trilioni bila ya riba. Itakapofika mwaka 2020 ambapo tutakuwa tumemaliza kulipa deni hili, tutakuwa tumelipa zaidi ya Sh. 1.8 trilioni, shilingi bilioni 600 zaidi,” amesema Zitto.
Zitto amesema, Watanzania zaidi ya 2000 duniani kote wameweka saini kutaka Taasisi ya Rushwa kubwa nchini Uingereza ( SFO ) kufungua upya shauri hili na kuitaka Benki ya Standard iwajibike kwa ufisadi huu dhidi ya nchi masikini ya Tanzania.
Amesema Rais Magufuli angeongoza Watanzania kukataa mikopo ya namna hiyo ambayo inafukarisha nchi ingekuwa ni hatua kubwa lakini Taasisi ya Kupambana na Rushwa (Takukuru) wanaona sifa kuweka ndani watu kwa Sh. bilioni 12 bila kuwataja watu watakaofaidika na Sh. bilioni 600 zaidi zitakazolipwa katika deni hilo.
“Ndio maama tunasema rais na serikali yake bado hawafanyi ya kutosha katika vita dhidi ya rushwa. Sio suala la kutumbua majipu tu, ni suala la kuweka mfumo madhubuti ambao utazuia rushwa kabisa.
“Chama chetu cha ACT -Wazalendo ni lazima kiendelee kuunga mkono juhudi zozote za kuondoa ufisadi nchini kwetu. Hata hivyo chama chetu ni lazima kiendelee kukosoa serikali pale ambapo tunapoona mambo hayaendi sawa.
“Tusiogope kuikosoa serikali kwa hoja kwani kukosoa serikali ni tukio muhimu sana la kizalendo,” amesema Zitto.

Hakuna maoni