NI KITUKO KITUPU ZANZIBAR,JECHA AENDESHA UCHAGUZI WAKE AKIWA MAFICHONI,SOMA HAPO KUJUA
Hatimaye uchaguzi mkuu wa marudio Zanzibar unafanyika leo
huku Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salim Jecha
akishindwa kuonekana hadharani kuzungumzia uchaguzi huo.
Kwa kawaida, kama
ilivyokuwa katika uchaguzi wa awali uliofanyika Oktoba 25 kabla ya kufutwa siku
tatu baadaye, Jecha alitarajiwa kuwa mstari wa mbele na kuzungumza na waandishi
wa habari kwa nia ya kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali kuhusiana na uchaguzi
huo.
Hata hivyo, katika
tukio nadra kuwahi kutokea hapo kabla, Jecha aliendelea kuadimika na hadi
kufikia jana jioni, taarifa zake kwa umma zilitolewa kupitia taarifa
iliyosambazwa kwa vyombo vya habari na wasaidizi wake tu huku yeye mwenyewe
akiendelea kutoonekana hadharani.
Uchaguzi huo wa
marudio unafanyika leo baada ya ule wa awali uliofanyika Oktoba 25, 2015
kufutwa na Jecha kutokana na kile alichoeleza kuwa ni kuwapo kwa kasoro nyingi
zilizouondolea sifa ya kuwa ‘uchaguzi huru na wa haki’.
Rais Ali Mohamed Shein
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) anatarajiwa kushinda kirahisi katika uchaguzi wa
leo baada ya mpinzani wake wa karibu, Makamu wa Kwanza wa Rais, Seif Shariff
Hamad wa Chama cha Wananchi (CUF) kususia uchaguzi huo kwa maelezo kuwa siyo halali
huku kikiitaka ZEC iendelee na mchakato wa majumuisho ya kura zilizotokana na
uchaguzi wa Oktoba na kumtangaza mshindi.
Katika taarifa yake
iliyodsambazwa kwa vyombo vya habari visiwani Zanzibar jana, Jecha alisema
waangalizi wa kimataiafa wakiwamo kutoka Jumuiya ya Ulaya (EU) hawatakuwapo
kushuhudia uchaguzi huo.
Badala yake, taarifa
hiyo ya Jecha ilieleza kwamba kutakuwa na waangalizi wa ndani pamoja na wengine
watokao Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).
Katika uchaguzi wa awali,
waangalizi karibu wote, kutoka ndani na nje ya Tanzania waliusifia uchaguzi huo
wa Zanzibar kwa kuulezea kuwa ulifanyika kwa uhuru na haki; baadhi yao wakiwa
ni kutoka EU, Jumuiya ya Madola, Umoja wa Afrika (AU), SADC, Jumuiya ya Afrika
Mashariki na Taasisi ya Uangalizi wa Uchaguzi Tanzania (TEMCO).
Hata hivyo, baada ya
Jecha kutangaza kufutwa kwa uchaguzi huo Oktoba 28 kwa kudai haukuwa huru na wa
haki, EU na Marekani zilipinga taarifa hiyo na hivyo haikutarajiwa kuwa
zingetuma wawakilishi wake katika uchaguzi wa leo ulioibua mgogoro mpya wa
kisiasa visiwani humo baina ya CCM na mahasimu wao, CUF.
UCHAGUZI PEKEE VYAMA
VINGI BILA CUF
Uchaguzi wa leo ni wa
kihistoria tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi visiwani Zanzibar kwa kuwa
unafanyika huku mgombea wa CUF, Maalim Seif akiwa siyo miongoni mwa wagombea na
pia wafuasi wa chama hicho wakitarajiwa kutoshiriki kwa wingi kama
ilivyozoeleka katika chaguzi zilizopita.
Tangu mwaka 1995, CUF
imekuwa ikichuana vikali na CCM huku vyama vingine vikiambulia jumla ya kura za
idadi ya chini ya asilimia moja.
Katika kuleta
maelewano visiwani Zanzibar, katiba ya mwaka 1984 ilifanyiwa mabadiliko na
kuanzishwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), lengo likiwa ni kuunganisha
nguvu ili kuimarisha umoja miongoni mwa Wanzanzibar ambao kwa kiasi kikubwa
wamegawanyika kiitikadi kupitia kambi za CCM na CUF.
Kwa mujibu wa katiba
ya sasa ya Zanzibar, ili chama cha siasa kipate sifa ya kuwamo katika kuunda
SUK, ni lazima kipate walau asilimia 10 ya kura zote halali zilizopigwa katikia
Uchaguzi Mkuu.
Kutokana na matakwa
hayo ya katiba, kuna kila dalili kuwa uchaguzi wa leo utaipa CCM mamlaka ya
kuongoza peke yake kwa kuwa vyama vingine, mbali na CUF ambayo imegomea
uchaguzi huo, havitarajiwi kuwa na uwezo wa kufikisha asilimia 10 ya kura zote.
ULINZI MKALI
Hadi kufikia jana
jioni, maeneo mengi ya Unguja visiwani Zanzibar yalikuwa na askari wenye
silaha wa vikosi mbalimbali wakiwamo wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),
huku wengi wao wakionekena kwenye maeneo nyeti kama ya Bandari, makao makuu ya ZEC
na Uwanja wa Ndege.
Aidha, upekuzi mkali
kwa kila abiria aliyekuwa akiingia Unguja kupitia bandarini ulikuwa ukifanyika
kwa siku nzima, huku taarifa zikidai kuwa ulinzi huo mkali umelenga kuhakikisha
kuwa amani inakuwapo muda wote na kuwapa fursa wananchi wote kujitokeza kwenda
kupiga kura pasi na bughudha.
WANAOCHUANA NA SHEIN
LEO
Baada ya wagombea wa
vyama vingine akiwamo Maalim Seif na chama chake (CUF) kutangaza kuwa
hawatashiriki uchaguzi huo, waliobaki kuchuana na Dk. Shein katika uchaguzi wa
leo ni Khamis Iddi Lila wa (ACT-Wazalendo), Juma Ali Khatib (TADEA), Soud Said
Soud (AFP), Hamad Rashid Mohamed(ADC), Issa Mohamed Zonga(SAU), Hafidh
Hassan Suleiman (TLP) na Ali Khatib Ali wa CCK.
MARAIS WALIOTANGULIA
ZANZIBAR
Katika historia ya
visiwa vya Zanzibar, marais waliowahi kuongoza ni Sheikh Abeid Amani
Karume aliyeongoza kuanzia Januari 12, 1964 hadi Aprili 7, 1972; Sheikh Aboud
Jumbe Mwinyi aliyeongoza Aprili 11, 1972 hadi Januari 30, 1984; Alhaji Ali
Hassan Mwinyi Januari 30, 1984 hadi Oktoba 24, 1985; Idris Abdul Wakil Oktoba
24, 1985 hadi Oktoba 25, 1990; Dk. Salmin Amour Juma Oktoba 25, 1990 hadi
Novemba 8, 2000; Amani Abeid Karume Novemba 8, 2000 hadi 2010 na kisha Dk.
Shein aliyeingia madarakani kwa mara ya kwanza Novemba, 2010.
SOURCE:
NIPASHE
Hakuna maoni
Chapisha Maoni