Zinazobamba

KIGOGO WA CCM ACHOCHEA VURUGU ZANZIBAR,YALIOSEMWA NA LOWASSA KUTUMIA,CUF YAONYA,SOMA



 Makamu wa pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi

MPASUKO wa kisiasa visiwani Zanzibar unazidi kushika kasi ambapo sasa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wameanza kutoa kauli zenye utata, anaandika Faki Sosi.

Sadifa Juma Khamis, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM ameibuka na kauli shawishi kwa vijana wa chama hicho kujiandaa na mapambano.

Kiongozi huyo wa vijana kwenye ukurasa wake wa Facebook jana ameandika ujumbe wa maneno unaoshawishi wanachama wa CCM hususan vijana kujiandaa kwa mapambano dhidi ya wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF).

CUF ndio chama kikuu cha upinzani visiwani humo kilichoeleza kupokwa ushindi kwenye uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba mwaka jana. Kimegomea uchaguzi wa marudio uliotangazwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) unaotarajia kufanyika tarehe 20 Machi mwaka huu.

Kwenye ujumbe huo wa Sadifa kwa vijana wa CCM ameandika “Waambie CUF tunapenda amani iendelee kuwepo. Wameishatuchomea nyumba zetu sana tunawavumilia, leo wamelipua nyumba ya kamishana wa polisi.


“Wamechoma matawi ya CCM, tumevumilia sasa nawambia vijana wa CCM inatosha, jiandaeni kupambana kwa vyovyote wanavyotaka, hii ni amri, sio ombi.”

Kauli ya Sadifa inakuja ikiwa ni siku moja kupita baada ya nyumba ya Hamdan Omar Makame, Kamishna wa Jeshi la Polisi visiwani Zanzibar kulipuliwa na bomu.

Kabla ya kulipuliwa kwa nyumba hiyo, matukio ya uchomaji moto ofisi za CCM na za CUF yameripotiwa kutokea hivi karibuni wakati ambao visiwa hivyo vinaelekea kwenye uchaguzi wa marudio uliotawaliwa na utata.

Abdul Kambaya, Naibu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano ya Umma wa CUF ameuambia mtandao huu kwamba, CCM inahangaika bure.

Amesema kwamba, Sadifa anajua vizuri mkakati huo unapangwa na watu gani na wanalipwa na nani lakini pia kwa malengo gani?

“Huyo anajua nini anachokifanya, anajua na kama hajui basi anapaswa kwenda kwa wakubwa zake kuuliza nini kinachoendelea?
“Lakini naamini anajua nani wanafanya upuzi huo, wanafanya kwa lengo gani na wanalipwa na nani?

“Hatupotezi muda kwa mambo ya kupuuzi kama hayo, yapo majukumu makubwa ya kuyashughulikia na kuyatoea ufafanuzi na si kauli za kipuuzi kama hizo lakini tunawaonya CCM kwa kila hatua wanayoichukua.”

Jecha Salim Jecha ambaye ni Mwenyekiti wa ZEC alifuta matokeo ya uchaguzi mkuu visiwani humo tarehe 28 Oktoba 2015 kwa madai ya kuwepo kwa kasoro kwenye uchaguzi huo na kuibua utata wa kisheria.
Kufutwa kwa uchaguzi huo kumesababisha mkwamo wa kisiasa na hata kuchochea matukio maovu visiwani humo.
Ugumu wa marudio ya uchaguzi huo unachagizwa zaidi na hatua ya CUF pamoja na vyama vingine tisa kugomea uchaguzi huo kutokana na kuitishwa kinyume cha sheria

Hakuna maoni