UKAWA WAENDELEA KUMGOMEA SPIKA NDUGAI,SOMA HAPO KUJUA
Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani bungeni, Tundu Lissu amesema kambi hiyo haitaongoza kamati za Bunge za Hesabu za Serikali (PAC) na Hesabu za Serikali za Mitaa (Laac) hadi ofisi ya Spika itakapobadilisha uteuzi wa wajumbe wa kamati hizo.
Kwa mujibu wa mabunge ya Jumuiya za Madola, kamati hizo huongozwa na wapinzani, lakini tangu Spika wa Bunge, Job Ndugai afanye uteuzi wa wajumbe, kambi hiyo imesusia kushiriki uchaguzi kwa kile wanachokiita “kupangiwa wajumbe”.
Jana, Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel alisema mazungumzo kati ya ofisi ya spika na kambi hiyo bado yanaendelea na kusisitiza kwamba uteuzi huo unaweza kutenguliwa au kuachwa kama ulivyo.
Katika maelezo yake, Lissu alisema licha ya kambi hiyo kuwa katika mazungumzo na ofisi ya spika, suluhisho halijapatikana na kusisitiza kuwa msimamo wao upo palepale.
“Hatujafika popote. Msimamo wetu uko palepale na hatutakubali kuchaguliwa viongozi wa hizo kamati na CCM, kama wanafikiria ni lazima iwe wanavyotaka sisi hatutakubali,” alisema.
Joel aliwahi kunukuliwa na na vyombo vya habari akisema kuwa kama kambi hiyo itasusia uchaguzi, shughuli za kamati zitafanywa na makamu wenyeviti ambao wanatokea CCM.
“Ni bora tusiziongoze kabisa kamati hizi. Ukifuatilia utabaini kuwa katika PAC na Laac tuna wajumbe sita kila kamati kati ya wajumbe 23, wakati huohuo kamati ya Ukimwi tumepewa wajumbe 12 kati ya wote 23,”alisema Lissu.
Alisema wajumbe sita waliopo katika kamati ya Laac na PAC wameteuliwa na CCM na kama kamati hizo zinaongozwa na upinzani ni lazima wapinzani wajichagulie wajumbe wao, wakiwamo watakaochaguliwa kuwa wenyeviti. Alisema wabunge wana haki sawa, lakini hawana uwezo sawa.
Lissu ambaye pia ni mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), alisema uamuzi wa spika kuwapangia wajumbe katika kamati hizo hauna nia nzuri na kwamba, huenda ni mkakati wa ofisi hiyo kuifanya Serikali iwe inapitisha mambo yasiyofaa bungeni.
Februari Mosi mwaka huu, Kambi ya Upinzani bungeni ilisusia uchaguzi wa viongozi wa kamati hizo kwa maelezo kuwa Spika Ndugai alifanya uteuzi ‘kiholela’ na kuahidi kutoshiriki mpaka pale watakapopewa idhini ya kupendekeza wenyeviti.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni