MAGUFULI AENDELEA KUVIPOPOA VYAMA VYA UPINZANI,ASEMA KAMWE CCM HAIWEZI KUTOKA MADARAKIANI KWA KARATASI,SOMA HAPO KUJUA
JOHN Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania amefuta mawazo kwamba, nchi hii haiwezi kuongozwa na chama kingine
isipokuwa Chama Cha Mpinduzi (CCM) pekee. Anaandika Regina Mkonde.
Kauli hiyo inanonesha kwamba,
si yeye wala CCM iliyo tayari kuachia madaraka hata kama watashindwa na chama
cha upinzani kwa njia ya kidemokrasia.
Rais
Magufuli ametamka kauli hiyo huku kukiwa na mgogoro wa kisiasa visiwani
Zanzibar uliotokana na CCM kushindwa na Chama cha Wananchi (CUF) kwenye
uchaguzi uliofanyika tarehe 25 Oktoba mwaka jana na baadaye matokeo hayo
kufutwa.
Rais
Magufuli amesema hayo leo kwenye maadhimisho ya miaka 39 ya CCM katika viwanja
vya Namfua mkoani Singida.
“Wapinzani
wasitegemee siku moja watakuja kuiongoza nchi, marufuku! Na wananchi waache
kuwaza vyama vingine vya ovyo ovyo na ajabu bali watuamini kwa kuwa
tumejipanga,” amesema.
Rais
amesema kuwa, vyama vya upinzani visiweke matumaini ya kuishika nchi na kuwa,
CCM iko imara, jeuri na hakuna wa kuikwamisha.
Pia
kwenye mkutano huo, Rais Magufuli amesema kwamba, watendaji wa serikali kuanzia
ngazi ya chini hadi juu wasioweza kutekeleza Ilani ya CCM, waachie ngazi.
Amesema
“uongozi wa serikali yangu tumeamua kuitekeleza Ilani ya CCM kikamilifu ili
kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi. Watendaji wa serikali kuanzia ngazi
ya chini hadi juu wasioweza kutekeleza Ilani wakae pembeni.”
Pia
ameonya wakuu wa wilaya, mikoa, mawaziri, watumishi na watendaji wa serikali
kuwa watawajibishwa endapo watashindwa kutatua kero za wananchi ipasavyo
hasa zilizoandikwa kwenye Ilani ya CCM.
“Uongozi
wa serikali yangu unawathibitishia Watanzania kuondoa kero zao, tumedhamiria
kufanya kazi na tutaifanya kazi,” amesema.
Amesema
serikali yake itaendelea kutoa ushirikiano kwa CCM sababu hakuna serikali yenye
maendeleo bila ya uwepo wa CCM.
“Serikali
ninayoongoza itaendelea kuonesha ushirikiano na CCM kwasababu hakuna serikali
bila ya CCM. Nasisitiza tena, watakaoshindwa kuitekeleza Ilani ya CCM
watatupisha kwa nguvu ili waingie watakaoweza,” amesema.
Ameipongeza
CCM kwa kutoa msaada wa madawati 1,000 ambayo yatasambazwa kwenye Halmshauri za
Mkoa wa Singida na kwamba, itaondoa changamoto ya wanafunzi kukaa chini.
Amesema
serikali imejipanga kuondoa changamoto zinazojitokeza sasa, hasa ya ongezeko la
idadi ya wanafunzi walioandikishwa ambayo haiendi na idadi ya madarasa.
“Kila
jambo zuri lina changamoto zake, wananchi wameitikia wito wa serikali wa
kupeleka watoto shule, kitendo kilichopelekea idadi ya wanafunzi kuongeza
ukilinganisha na madarasa yaliyopo,” amesema na kuongeza;
“Serikali
iko mbioni kuondoa changamoto hiyo na nyingine zitakazojitokeza ili kufanikisha
adhma yetu ya kutoa elimu bure kwa wanafunzi kuanzia Darasa la 1 hadi Kidato
cha Nne.”
Kwenye
mkutano huo, Jakaya Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa CCM amesema Makamu wa Rais,
Samia Suluhu Hassan kuwa ana uwezo wa kutekeleza majukumu ya rais
inavyostahili.
Dk.
Kikwete ambaye ni Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne amesema,“CCM haikufanya makosa
kumchagua Samia Suluhu kuwa makamu wa kwanza wa rais mwanamke kwasababu ana
uwezo wa kutekeleza majukumu ya rais pale anapokuwa na udhuru.” amesema Dk.
Kikwete na kuongeza;
“Kama
una uwezo wa kutekeleza majukumu ya rais vilivyo anapopata udhuru, utashindwaje
kuyatekeleza utakapo kuwa Rais?,” amesema.
Amesema
kuwa CCM imefuata misingi ya usawa wa kijinsia kwa kumchagua mwanamke kuwa
makamu wa rais na kuvunja rekodi ya kuwa chama kinachothamini mchango wa
wanawake kwenye maendeleo ya Taifa.
Hata
hivyo amesema, amefurahishwa na utendaji kazi wa Serikali ya Rais Magufuli na
kuwa, awali chama kilikuwa kwenye wakati mgumu hivyo atakiimarisha na
kuwarudishia matumaini wananchi.
“Mimi
naamini viongozi wazuri wapo kwenye chama chetu, tuwashauri wagombee,
waliochokaa wakae pembeni ili wanaoweza wafanye kazi ya kuimarisha chama,”
amesema.
Habari hii kwahisani ya Mwanahalisi oline
Hakuna maoni
Chapisha Maoni