SAKATA LA VYETI VYA KIDATO CHA SITA LAZIDI CHUKUA SURA MPYA,SOMA HAPO KUJUA
Baraza la Taifa la Mitihani (Necta), limeagiza kusitishwa kwa ugawaji wa vyeti vya kidato cha sita kwa wanafunzi waliohitimu mwaka 2015, huku vile vilivyokwisha gawanywa kwa watahiniwa hao vikitakiwa kurejeshwa kwenye chombo hicho.
Hali hiyo imeibua utata mkubwa, huku baadhi ya wadau wakiwamo maofisa elimu, wakihisi hatua hiyo ya Necta huenda inalenga kuvibadili vyeti hivyo kutoka kwenye mfumo wa wastani wa alama (GPA), kwenda kwenye ule wa jumla (division).
Ofisa Elimu Mkoa wa Dodoma, Juma Kaponda, alipoulizwa kama amepokea agizo hilo, alithibitisha kuwa shule zote za mkoa huo zenye kidato cha tano na sita zimepewa taarifa ya kutakiwa kurudisha vyeti hivyo Necta.
Alisema sababu ya kuvirudisha vyeti hivyo anadhani ni kufanya mabadiliko kutoka GPA na kurudi kwenye divisheni.
Ofisa Elimu Mkoa wa Arusha, Nestory Mloka, alisema amepata barua ya maelekezo hayo kutoka Necta ikimuelekeza kuwataka maofisa elimu wilaya wawasiliane na wakuu wa shule za kidato cha tano na sita wasigawe vyeti vya wanafunzi waliohitimu mwaka 2015.
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya St. Matthew iliyoko Kongowe, Mkuranga mkoani Pwani, Abraham Shafuri, naye alikiri kuwapo kwa agizo la Necta la kusimamisha utoaji wa vyeti hivyo kwa wahusika.
Alisema aliambiwa na maofisa wa Necta kuwa vyeti hivyo vinatakiwa kurejeshwa kwenye baraza hilo na kwamba sababu zilizotolewa ni kuwa kuna marekebisho kidogo yanapaswa kufanyika.
“Nilichoambiwa ni kwamba shule karibu zote za Dar es Salaam zimesharejesha vyeti hivyo na kwamba kwa sisi wa mkoa wa Pwani, maofisa hao watapita kuvichukua lakini hatujui ni lini watakuja,” alisema Shafuri.
Hata hivyo, Katibu Mtendaji wa Necta, Dk, Charles Msonde, alipoulizwa alikanusha vikali madai hayo, akisema vyeti hivyo havitabadilishwa kutoka kwenye mfumo wake bali vimesitishwa kugawanywa ili baraza lijiridhishe na baadhi ya vitu.
“Vyeti hivi baraza limevigawa hivi karibuni na lilichofanya sasa limezuia kwanza shule zisigawe mpaka litakapotoa maelekezo mengine, msingi huo wa kuzuia uko kwenye hoja ya kuhakikisha tu kwamba linajiridhisha kwenye takwimu zake kama zimekaa sawasawa katika vyeti vilivyokwenda kila shule.
“Baadhi ya vyeti kwenye mkoa wa Dar es Salaam vipo Necta, lakini kwenye mikoa mingine yote viko shuleni,” alisema Dk Msonde na kuongeza;
“Kama mkuu wa shule alikuwa amegawa vyeti viwili, vitatu kabla havijarejeshwa baraza ni suala jingine, lakini kiujumla kinachofanywa na baraza hapa ni kuhakiki cheti hiki, kama vimekaa kama utaratibu wetu ulivyo.”
Alisema suala la kubadilisha kutoka kwenye GPA kwenda kwenye divisheni halipo na kwamba matokeo yaliyotangazwa kwa utaratibu wa GPA vyeti vyake vitaendelea kuwa katika mfumo wa GPA na matokeo yaliyotangazwa kwenye utaratibu wa divisheni vyeti vyake vitabaki kuwa kwenye divisheni.
Alisema kwa wale ambao tayari wako nje ya nchi, hakuna atakayeathirika na kama baraza likihitaji cheti chake litafanya utaratibu wa kukipata.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni