CHADEMA YATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KWA MSIBA WA LETICIA NYERERE,SOMA HAPO KUJUA
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wake wa Viti Maalum, Leticia Nyerere kilichotokea juzi nchini Marekani.
Leticia alifariki dunia katika hospitali ya Doctors Community iliyopo Lan ham, Maryland Jumapili saa 2 usiku wa saa za Afrika Mashariki alikokuwa amelazwa kwa matibabu.
Taarifa ya Chadema iliyotolewa na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa chama hicho, Tumaini Makene ilisema kuwa chama hicho kimepokea kwa masikitiko makubwa msiba wa Leticia Nyerere uliotokea nchini Marekani.
“Tunatoa pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki katika wakati huu mgumu wa kuondokewa na mpendwa wao, Mwenyezi Mungu awatie moyo wa ujasiri na subira katika wakati huu mgumu wa majonzi ya msiba huo,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo ya Makene.
Makene alisema Chadema watamkumbuka Leticia kwa mchango wake na ushiriki wake wakati wote alipokuwa mwanachama wao na akiwa miongoni mwa watu waliopata fursa za kuwa wabunge kupitia Chadema.
Msemaji wa familia ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku juzi alimueleza Rais Magufuli kuwa familia inaendelea na taratibu za kuusafirisha mwili wa marehemu kutoka nchini Marekani kuurejesha nyumbani kwa maziko.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni