KIFO CHA MTIKILA,POLISI WAMALIZA UBISHI KUHUSU CHANZO CHA KIFO CHAKE,INASIKITISHA,SOMA HAPO KUJUA
Gari alilopata nalo ajali Marehemu Mchungaji Christopher Mtikila |
BAADA ya kutokea kifo
cha Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila maeneo ya Msolwa, Chalinze,
mkoa wa Pwani, kuliibuka hisia nyingi kutokana na chanzo cha kifo hicho,
ifuatayo ni taarofa ya jeshi la Polisi mkoa wa Pwani:-
TAARIFA YA POLISI KUHUSU KIFO CHA MCHUNGAJI
MTIKILA
Mnamo tarehe
04/10/2015 majira ya saa 05:45hrs huko Msolwa Kata ya Bwilingu barabara kuu ya
Dar es Salaam – Morogoro, Wilaya ya Ki-Polisi Chalinze, Mkoa wa Pwani. Gari No.
T.189 AGM aina ya Toyota Corolla likiendeshwa na George Steven Ponera miaka 31,
mkazi wa Mbezi Mwisho Dar es Salaam liliacha barabara kisha kupinduka na
kusababisha kifo cha Christopher Mtikila miaka 62, mpangwa, mchungaji wa Kanisa
la Assemblies, na mwenyekiti wa Chama cha siasa DP mkazi wa Kinondoni “B” Dar
Salaam.
Katika ajali hiyo,
watu watatu waliokuwamo ndani ya gari hilo na marehemu Mchungaji Mtikila
walijeruhiwa ambao ni Ally Mohamed miaka 42 mkazi wa Mbezi Dar es Salaam, yeye
alipata maumivu shingo, mabegani na kifuani, mwengine ni Patrick Mgaya miaka 37
ambaye ni mchungaji wa Kanisa la Assemblies of God mkazi wa Mbagala Dar es
Salaam ambaye alikuwa na michubuko midogo usoni na kuumia kichwani, pamoja na
George Steven miaka 31 mkazi wa Mbezi Dar es Salaam ambaye alipata michubuko kidogo
eneo la mabegani. Majeruhi wote
walipatiwa matibabu katika Kituo cha afya Chalinze na badae wawili kati yao
katika Hospitali teule ya Tumbi na waliruhusiwa kutokana na hali zao kuendelea
vizuri.
Baada ya kutokea kwa
hiyo ajali, timu maalum ilifika katika eneo la tukio kwa ajili ya ufuatiliaji
wa ajali hiyo ikiongozwa na Mkuu wa utawala wa Traffic kuu Dar es Salaam SACP
J. Kahatano, pamoja na mimi mwenyewe, Mkuu wa Upelelezi Makosa ya Jinai Mkoa wa
Pwani na kuwashirikisha wataalamu wa Forensic Makao Makuu ya Polisi ACP
Kashindye na Dokta A. Makata.
Uchunguzi wa mwili wa
marehemu tayari umefanyika, na taarifa ya Daktari aliyefanya uchunguzi huo
katika Hospitali ya Rufaa tumbi Kibaha jana tarehe 04/10/2015 umeonyesha kuwa,
kifo cha marehemu kimesababishwa na kuvunjika kwa mbavu nane (8) upande wa
kushoto na kuingia kwa damu kwenye mfumo wa hewa na kusababisha kushindwa
kupumua.
Kabla ya ajali hiyo
kutokea marehemu na wenzake tarehe 02/10/2015 jioni waliondoka Dar es Salaam
kwenda Mkoa wa Njombe na kufika tarehe 03/10/2015 alfajiri kwa ajili ya kampeni
za Chama chao cha DP. Wakiwa huko walipata ajali kwa kugonga magari mawili
yaliyopata ajali na kusababisha uharibifu wa gari lao.
Kulingana na taarifa
ya Mkaguzi wa magari ya tarehe 03/10/2015 huko Njombe walishauriwa
walitengeneze kwanza kabla ya kulitumia tena.
Tarehe 03/10/2015 saa
21:30hrs waliondoka Njombe kwenda Dar es Salaam na ilipofika saa 05:45hrs
katika eneo la Msolwa ndipo wakapata ajali hii.
Uchunguzi uliofanywa
kwa kukagua tukio na kuwahoji majeruhi walionusurika (katika eneo hilo hakuna
watu wengine walioshuhudia tukio hilo kwa kuwa si eneo la makazi ya watu, ni
mbuga). Ajali hii imeonyesha kuwa imesababishwa na sababu zifuatazo:
1. Mwendo kasi, dereva mwenyewe anakubali kwamba
alikuwa mwendo kasi licha ya kuwepo kwa alama zinazooonyesha kwenda mwendo wa
Km 50 kwa saa. Aidha baada ya kuacha barabara kuu, gari hilo lilikwenda umbali
wa mita 125 kabla ya kupinduka hali inayoashiria kuwa lilikuwa kwenye mwendo
kasi.
2. Uchovu wa dereva kutokana na safari ndefu kwa
kuendesha gari mchana na usiku kucha kabla ya kuanza safari walikuwa
wakishughulikia matengenezo ya gari hilo ambapo hakupata muda wa kupumzika.
3. Kutofunga mkanda ya usalama. Katika uchunguzi
inaonyesha marehemu hakufunga mkanda kwa kuwa alirushwa nje kupitia kioo cha
mbele (wind screen).
4. Ubovu wa gari. Gari hilo lilipata ajali tarehe
03/10/2015 na moja ya sehemu muhimu iliyoharibika ni mfumo wa usukana (steering
system) yawezekana halikupata matengenezo kikamilifu na hivyo kuchangia kutokea
kwa ajali hiyo.
Hivyo nitumie fursa
hii kuwaomba wananchi kuwafichua maderva wanaokwenda mwendo kasi kupitia namba
08007575 ama 0715 009953 au 0658 376012. Aidha niwatake madereva kuzingatia
sheria za usalama barabarani na kwa wale watakao kaidi Jeshi la Polisi Mkoa wa
Pwani hatutasita kuwachukulia hatua kali za kisheria ili iwe fundisho kwa
wengi.
Asanteni kwa
kunisikiliza.
Imetolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani
Kamishina Msaidizi Jafari Ibrahim.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni