DC MAKONDA AWALIZA MISS IFM AWAINGIZA MJINI,SOMA HAPO KUJUA
MKUU wa Wilaya ya Kinondoni, mkoani Dar es Salaam, Paul Makonda
analalamikiwa kuwa amesaliti ahadi yake ya fedha kwa warembo watatu walioshinda
shindano la urembo la Miss IFM 2015 akilaumiwa kukwepa kuwajibika. Anaandika Yusuph Katimba …
(endelea).
Katika shindano hilo lililofanyika Mei
mwaka huu, Makonda aliyeteuliwa DC mapema mwaka huu, alialikwa kuwa mgeni rasmi
na alipohutubia hadhara baada ya washindi kutangazwa, aliahidi kuwapa zawadi ya
Sh. 500,000 kila mmoja.
Makonda alikuwa amebadili aina ya
ahadi kwani alitangulia kusema kwamba atampatia kila mrembo kompyuta moja.
Baadaye ndio akaueleza umma
uliohudhuria shindano hilo lililofanyika kwenye ukumbi wa jengo la PSPF Diamond
Jubilee, Ghorofa ya Tano, kuwa atampatia kila mrembo Sh. 500,000 na akaelekeza
warembo hao kumfuata ofisini kwake Jumatatu iliyofuata ili awakabidhi.
Zimepatikana taarifa kuwa Makonda
hajatimiza ahadi yake hiyo mpaka Jumanne siku ambayo Makonda alipigiwa simu na
kuulizwa msimamo wake kuhusu suala hilo.
“Kwani wewe inakuhusu nini,
waulize wenyewe,” ndivyo alivyojibu. Lakini alipoambiwa kwamba warembo ndio
wanaolalamika na wamejieleza, Makonda alikata simu na hakupatikana tena
alipopigiwa mara kadhaa.
Awali alikiri kualikwa na
wadhamini wa shindano la Miss IFM 2005 na pia kwamba alitoa ahadi ya kutoa
fedha.
Mtoa taarifa ambaye hakutaka
kueleza utambulisho wake, zaidi ya kusema, “nimezipata za uhakika kutoka ndani
ya familia ya mrembo mmoja,” alisema warembo hao wamefika mara kadhaa ofisini
kwa Makonda lakini badala ya kutimiza ahadi “anawasumbua kwa njia mbalimbali.”
“Baada ya kuwasiliana naye
alituambia twende na tulipoenda tukaambiwa hayupo. Tukaondoka, tulipowasiliana
naye tena na kumpata, akatuahidi, lakini kila tukifika pale ofisini tunaviona
viashiria vyote vya huyu mheshimiwa kutukwepa,” amenukuliwa mrembo mmojawapo.
Chanzo kingine kimesema
kimepata taarifa kwenye duru za habari ndani ya Chuo cha Usimamizi wa Fedha Dar
es Salaam zikimnukuu mrembo akisema, “Tumekata tamaa, hatujui hasa sababu za
mheshimiwa huyu kuahidi na kisha kushindwa kutekeleza ahadi yake. Naamini
anatukimbia.”
Kwa mujibu wa ofisa mmoja kati
ya walioratibu shindano hilo, ndiye aliyemshawishi kuhudhuria na kumpa heshima
ya kuwa mgeni rasmi katika shindano.
Ofisa huyo amekuwa
akiwasiliana na warembo hao kuwauliza kama wameshapata zawadi zao kutoka kwa
Makonda lakini anasikitika kujibiwa hawajapata.
“Ninasikitika kwamba
mheshimiwa mwenyewe aliahidi warembo wenyewe waende ofisini kwake kufuatilia
kesho yake, sasa inakuwa vigumu mtu mwingine kufuatilia,” amesema alipoulizwa
kama haoni anawajibika kuulizia kwa Makonda mwenyewe.
“Inakuwa vigumu kufuatilia
mimi binafsi, kwa sababu waliokuwepo ukumbini walisikia mwenyewe akitaka
warembo wafike ofisini kuchukua zawadi zao,” amesema.
Muongozaji shughuli siku ya
shindano la Miss IFM 2015 alikuwa msanii wa vichekesho wa kundi la Ze Comedy,
Mpoki ambaye alilinogesha vilivyo.
Habari hii
kwahisani ya Mwanahalisi oline
Hakuna maoni
Chapisha Maoni