HABARI KUBWA LEO,KAMANDA MBOWE ATOKA WODINI,ASEMA MAPAMBANO YANAENDELEA,SOMA HAPO KUJUA
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe (katikati) akizungumza na waandishi wa habari juu ya afya yake, akiwa hospitali ya Muhimbili. Kushoto ni Mwenyekiti Mwenza wa UKAWA, James Mbatia |
“HAKUNA hali yoyote ya hofu,” anasema Mwenyekiti wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe akiwa amepata wasaa wa
kukutana na waandishi wa habari asubuhi leo, ndani ya Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili, Dar es Salaam. Anaandika
Pendo Omary …
(endelea).
Mbowe, mwenyekiti mwenza wa Umoja wa
Katiba ya Wananchi (UKAWA) na mgombea ubunge jimbo la Hai, mkoani Kilimanjaro,
amesema, “Ndugu wananchi nipo salama. Watanzania wasiwe na hofu. Kwa sasa
namalizia muda uliobaki wa saa 24 kati ya saa 48 niliopewa na madaktari kwa
ajili ya mapumziko.”
Ametoa kauli hiyo kwa waandishi wa
habari leo saa 5.17 asubuhi hospitali ya Taifa Muhimbili, katika ukumbi wa
mikutano wa jengo la Kitengo cha Moyo, kwenye hospitali hiyo ambako amelazwa
tangu kiasi cha saa 11 jioni jana, katika wodi Na. 2, Chumba Na. FF – 6 eneo la
wagonjwa wa hadhi kubwa.
Mbowe amelazwa kutokana na tatizo la
uchovu wa mwili lililotokana na kufanya kazi ngumu mfululizo, na kwa muda mrefu
bila ya kutumia muda wa kutosha kupumzika. Amekuwa akiendelea na uangalizi wa
madaktari wa kitengo cha moyo.
Daktari Tulizo Sanga akizungumza na
waandishi wa habari, amesema walimpokea Mbowe saa 11 jana baada ya kupata rufaa
kutoka Hospitali ya Doctors Plaza ya wilayani Kinondoni.
Hali ya Mbowe ilibadilika ghafla jana
akiwa kwenye gari eneo la Manyanya, na kulazimika kukatisha safari ya kwenda
viwanja vya Biafra kusalimia wananchi waliokusanyika kumsubiri mgombea urais wa
Chadema-Ukawa, Edward Lowassa aliyekuwa anatoka makao makuu ya Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) kuchukua fomu ya uteuzi. Ni hapo Mbowe alikimbizwa hospitali ya
Doctors Plaza.
Taarifa zilizochapishwa na gazeti la Mwananchi leo, zilisema Mbowe alijisikia afya
yake kubadilika ghafla wakati msafara wa mgombea ukiwa unaenda Biafra, ukiwa
umeahirishwa kwenda moja kwa moja makao makuu ya chama, mtaa wa Ufipa kwa kuwa
kulikuwa na umma wa wananchi Biafra, baada ya kuelekezwa kubaki huko kutokana
na ufinyu wa nafasi Ufipa.
“Baadae aliletwa kitengo cha moyo;
baada ya vipimo tuligundua kuwa anasumbuliwa na uchovu uliotokana na kufanya
kazi kwa muda mrefu bila kupumzika,” amesema Daktari Sanga ambaye amekuwa
akiongoza jopo la madaktari wanne wanaomhudumia Mbowe.
Akiambatana na baadhi ya viongozi wakuu
wa Ukawa na Chadema, Mbowe alifika kwa waandishi wa habari kwa kutembea bila
shida, na baada ya kuketi ukumbi wa mikutano wa jengo hilo la Kitengo cha Moyo
, alisema: “Nimekuja
kuzungumza ili kuwahakikishia Watanzania wote kwamba nipo salama. Hakuna hali
yoyote ya hofu kama ilivyojengeka kwenye mitandao ya kijamii.”
Alisema afya yake ni nzuri na kwamba,
“Namalizia tu saa nilizopewa na madaktari kwa ajili ya mapumziko.” Pembeni yake
alikuwepo Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti
Mwenza wa Ukawa pamoja na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na madaktari
Maneno Mlawa, Bashiri Nyangasa na Salome Kasanga.
Mbatia alisema wanashukuru Mola
kwamba hali ya Mbowe ni salama. “Tunamuombea aendelee hivyo,” alisema Mbatia,
akisisitiza kuwa shughuli za Ukawa hazijaathirika kwa kuwa viongozi wengine
wapo imara.
“Ukawa sio mtu mmoja, ni Watanzania
wote kwa hivyo ratiba itaendelea kama ilivyopangwa na yeye ataungana nasi baada
ya kutoka hospitalini,” amesema.
Kwa wiki kadhaa sasa, Mbowe
ambaye kwa nafasi yake ndiye muongoza vikao vyote vya juu vya Chadema, amekuwa
katika shughuli nzito mfululizo za ndani ya chama, huku akilazimika kushiriki
vikao vya mashauriano na wenyeviti wenzake katika UKAWA ili kukamilisha
taratibu za kupata mgombea mmoja wa urais.
UKAWA wenye pia vyama vya CUF na NLD
cha Dk. Emmanuel Makaidi, wamefanikiwa kumteua Lowassa, na mgombea mwenza wake
Juma Duni Haji kutoka Zanzibar, ambao wanatarajiwa kuanza safari ya kutafuta
wadhamini kabla ya kurudisha fomu Tume Agosti 21. Katika safari hiyo
watahutubia mikutano ya hadhara jijini Arusha, Mbeya, Mwanza, Zanzibar na
mwishowe Dar es Salaam.
Habari hii kwahisani ya Mwanahalis oline
Hakuna maoni
Chapisha Maoni