Zinazobamba

ISOME MAKALA YA SAED KUBENEA KUHUSU UJIO WA LOWASSA CHADEMA,BOFYA HAPO

Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa alipokuwa anawasili Makao Makuu ya Chadema
Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa alipokuwa anawasili Makao Makuu ya Chadema

MJADALA juu ya Edward Lowassa, mbunge wa Monduli, kuhama Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), unaendelea kushika kasi. Anaandika Saed Kubenea … (endelea).
         Hili limetokea muda mfupi baada ya vyama vinavyounda Muungano wa Kutetea Katiba ya Wananchi (UKAWA), kunukuliwa wakimkaribisha Lowassa ndani ya umoja huo.
         Katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari, ndani na nje ya nchi, mjadala umekuwa ukarimu wa vyama vya upinzani kwa Lowassa. Wapo wanaohoji: Ni lini Lowassa amekuwa swahiba wa upinzani?
          Ni lini Chadema imeanza kuamini kuwa Lowassa ni mtu safi,  mwadilifu na mchapakazi? Ni lini kimeanza kuamini kuwa Lowassa amesafishika kutoka katika lindi la tuhuma za ufisadi? Lini Chadema kimeanza kuamini kuwa Lowassa alionewa katika sakata la kashfa ya Richmond?
Je, hatua ya Chadema kumbeba Lowassa inalenga nini? Haya ndiyo maswali ambayo wananchi wanajiuliza na ambayo yanastahili kupatiwa majibu.
            Akisoma tamko la vyama vinavyounda UKAWA – NCCR- Mageuzi, Chadema, Chama cha Wananchi (CUF) na National League for Democrats (NLD) – mbele ya waandishi wa habari, James Mbatia, mmoja wa wenyeviti wa UKAWA alisema, “…tunamkaribisha Lowassa UKAWA ili kukamilisha kazi ya kuing’oa CCM.”
          Mkutano kati ya waandishi wa habari na viongozi wakuu wa UKAWA, ulifanyika makao makuu ya CUF, Buguruni, jijini Dar es Salaam, Jumatatu wiki hii.
Hizi ndizo hoja ambazo wananchi wanataka ufafanuzi wake. Chadema na wale wote wanaomuunga mkono Lowassa kuamua kuondoka na minyororo ya utumwa ya CCM, wanatakiwa kuyatolea ufafanuzi.
           Kwa mfano, wananchi wanapaswa kuelezwa, hoja juu ya uadilifu wa Lowassa au uchafu, siyo hoja tena jambo la mjadala kwa sasa. Lowassa amekuwa kimya miaka saba, hawezi kuibuka na kusema leo akasikilizwa.
Hata wale wanaompinga nje ya Chadema na kumwita “fisadi,” hawawezi kuwa na hoja ambazo zitamuumiza Lowassa.
           Hapa hoja kuu ni ujio wake ndani ya Chadema na UKAWA, ikiwa ni mwanzo wa mafuriko au ukame.
Lakini kitendo cha Lowassa kukaribishwa UKAWA kuwa mgombea urais, kitasaidia kupatikana taarifa kuhusu ushiriki wa Lowassa katika sakata la umeme wa Richmond.
           Tutapata kufahamu nani aliyeisajili kampuni hiyo nchini? Je, ni kweli ilisainiwa na Samwel Sitta, wakati alipokuwa mkurugenzi wa kituo cha uwekezaji nchini (TIC)?
           Tutapata kufahamu kwa nini Bunge lilimtuhumu kuhusika katika kuingiza nchi kwenye mkataba huo? Kwa nini Dk. Harisson Mwakyembe, aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge, iliyochunguza mkataba wa Richmond, alidai kuwa Lowassa alihusika na mkataba huo?
             Pamoja na kwamba Dk. Mwakyembe ameshindwa kuthibitisha kuwa Lowassa amepokea rushwa ili kuipatia kazi kampuni hiyo, bado ni muhimu yeye akaeleza, sababu zilizoipa kazi ya kufua umeme Richmond, wakati haikufanyiwa uchunguzi.
        Nani aliyeamrisha kutoa mkataba kwa Richmond na sababu zake? Alilipwa kiasi gani? Je, akiwa waziri mkuu ambaye anatajwa katika Ibara ya 52 na 53 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano kuwa ndiye mwenye “udhibiti, usimamiaji na  utekelezaji” wa shughuli za kila siku za serikali alitenda yote hayo kwa maelekezo ya nani? Au aliagizwa na rais?
           Uhusika wa Rais Jakaya Kikwete, katika suala hilo ukoje? Je, pale aliposema, “hakuna jambo nililolifanya ambalo wewe Rais Kikwete hukulifahamu au hukunituma kuhusu Richmond/Dowans” alilenga nini?
           Aidha, Lowassa anapaswa kueleza kwa nini alinyamazia pendekezo la aliyekuwa waziri wa nishati na madini, Dk. Ibrahim Msabaha, kuwa Tanesco iingie mkataba na Richmond!
         Wala hajawahi kukana hadharani au kutoa maelezo ya kilichosababisha kampuni hiyo ya kitapeli kupata mkataba katika giza la upendeleo. Hajaeleza alihusika vipi na suala hilo na hatua alizochukua.
       Anapaswa kueleza hatua alizochukua kuhakikisha Sheria ya Manunuzi ya Umma (PPRA), inafuatwa.
Anapaswa kueleza kilichosababisha kujiuzulu uwaziri mkuu wakati anadai hakuwa na makosa. Je, alitaka kumfurihisha nani au alidaganywa na Kikwete?
Hili ni muhimu akalieleza kwa kuwa baadhi ya wafuasi wake wanaamini kuwa Lowassa hakujiuzulu kwa sababu ya kuwajibika kutokana na makosa ambayo yeye, akiwa kiongozi na ofisi yake, walifanya kuhusiana na Richmond. Au hakujiuzulu kwa sababu alikubaliana na madai yaliyotolewa na Dk.  Mwakyembe.
Je, alijiuzulu kwa sababu aliamini kulikuwa na mkakati wa kumuondoa katika kiti chake; mkakati huo ulisukwa kwa ustadi mkubwa na baadhi ya wakubwa serikalini, akiwamo Sitta. Alijiuzulu kwa sababu aliamini Kamati Teule ya Bunge, haikutoa nafasi ya kujitetea? Alijiuzulu kupinga kile alichoita, “kutotendewa haki.”
Tarehe 7 Februari 2008, Lowassa alisema, “…nimetafakari kwa makini sana jambo hili, nikajiuliza hivi kulikoni mpaka watu wazima wenye uwezo wao, watu maarufu wenye heshima zao, mpaka wafike mahali waache jambo la msingi kama hilo; kulikoni?”
Aliongeza, “mimi nadhani tatizo, ni uwaziri mkuu. Nadhani tatizo ni uwaziri mkuu. Kwamba ionekane waziri mkuu ndio amefanya haya, tumuondolee heshima au tumwajibishe.”
Kwamba Lowassa aliamua kujiuzulu badala ya kujitetea bungeni, ni fursa nyingine kwake kueleza kuwa akina Dk. Mwakyembe walisema “uongo” bungeni.
Anapaswa kuumbua uongo huo hoja kwa hoja ili kulipa taifa nafasi ya kuuona ukweli. Pamoja na yeye kujiuzulu, serikali imeshindwa kutekeleza maazimio 11 ya Bunge, likiwamo Azimio Na. 11, linalohusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma (1995).
Pamoja na kujiuzulu, bado viongozi waandamizi wenye dhamana ya kisiasa serikali wanaendelea na biashara zao binafsi wakiwa madarakani, jambo ambalo lina mgongano wa kimaslahi.
Pamoja na yeye kujiuzulu, kwa nini serikali imeshindwa kufanya maandalizi ya majadiliano ya kina kuhusu suala hilo ndani na nje ya Bunge? Kwa nini imeshindwa kuunda kikundi kazi kufuatilia hili?
Kwa nini waraka wenye mapendekezo ya kurekebisha sheria ya maadili ya viongozi wa umma, (Sura 398), ambao ulifikishwa hadi katika ngazi ya kujadiliwa na kamati ya makatibu wakuu (IMTC) haujakamilishwa?
Mapendekezo ya waraka huo yanadaiwa yangesaidia kuweka utaratibu mahsusi kwa viongozi waandamizi wenye dhamana ya kisiasa na watendaji wa ngazi ya juu katika utumishi wa umma, kutenganisha shughuli zao za biashara na uongozi wa umma. Lengo ni kuepusha migongano ya kimaslahi katika utendaji wao. Lakini hakuna kilichofanyika na waraka haujakamilika.

 makala hii kwahisani ya gazeti la Mawio

Hakuna maoni